Advertisements

Monday, April 21, 2014

UNAKUBALIKA KWENYE JAMII YAKO? - 3


LEO ni wiki ya tatu tunazungumzia kuhusu maisha. Tumehama kidogo kwenye mapenzi na kugeukia kwenye maisha maana yana umuhimu mkubwa kujadiliwa!

Safu inaitwa Love & Life ikimaanisha Mapenzi na Maisha, ndiyo maana tunakuwa na uwanja mpana. Nazungumzia kuhusu kukubalika. Hebu sasa tuendelee.

MTAANI
Unaishije na majirani zako? Inawezekana ukawa unajilaumu kwa kutokubalika kwako kumbe kuna maeneo ambayo kwa kujua au kutokujua huwa unakosea. Majirani ni watu ambao unapaswa kuwa nao karibu sana.

Baadhi ya watu huishi kwa maringo na kubagua wengine kwa sababu wanatofautiana hadhi, hili si jambo la busara. Kama unaishi nyumba moja na wenzako, halafu unaamka asubuhi hata ‘habari gani?’ huna, hilo ni tatizo na unaweza kuchukuliwa kama unayeringa.

Hata kama una heshima kubwa kazini kwako, lazima uishi na majirani zako kwa upendo na ushirikiano.
Kunapotokea matatizo ya msiba kwa jirani yako au kuugua, basi uwe mstari wa mbele kumfariji. Kuna wengine wanaishi mtaa ambao hata mwenyekiti wake hamjui, hafahamu majina ya watu anaoishi nao nyumba moja!

Ndugu yangu, hayo siyo maisha sahihi unayopaswa kuishi. Jiulize, ukizidiwa ghafla usiku utamwomba nani akusaidie wakati hata majina yao huyajui?
Kama upo katika mkumbo huu, badilika. Ishi na majirani zako kwa upendo, ikiwezekana uwe na namba za simu za baadhi ya majirani zako.

Hii itasaidia kukusogeza nao karibu na kukuona kama sehemu ya familia zao.
Hata kama huna mazoea ya kukaa vijiweni, siku za mapumziko yako unapaswa kupita japo mara moja na kupiga soga za siasa kisha unarudi zako nyumbani.

Si kila kijiwe kina watu wenye tabia za ajabu, kuna vijiwe vingine vinajenga. Nenda hata kwenye kawaha, ukae na vijana wa mtaani kwako na kuzungumza nao mawili matatu; hapo utakuwa karibu na jamii inayokuzunguka na utakubalika.

KAZINI
Kwa kawaida, kazini ndiyo sehemu ambayo unatumia muda mwingi zaidi kwa siku kuliko sehemu nyingine. Sehemu nyingi za kazi, watu huripoti kuanzia saa 2 – 3 asubuhi na kutoka kati ya saa 9 – 11 jioni na kuendelea.

Ukiweka na foleni za barabarani, wengi hufika nyumbani muda ukiwa umekwenda sana. Huonekana zaidi siku za mapumziko ya mwisho wa wiki ambapo hujifungia ndani wakijaribu kufidia usingizi wa wiki nzima.

Kazini ni sehemu unayopaswa kuishi na watu vizuri, ukae na wafanyakazi wenzako kama ndugu wa damu. Wiki ijayo tutajifunza zaidi katika sehemu ya mwisho ya mada hii, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.

No comments: