Advertisements

Saturday, April 26, 2014

Warioba: Matusi, uongo vinaniumiza

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba amesema baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wametumia vibaya Bunge hilo kwa kumshambulia na kumsingizia mambo ya uongo kwa makusudi, akisema matusi yanayotolewa dhidi yake yanamuumiza.
Aidha, Warioba amesema ingawa haelewi kwa nini wanaomshambulia wameamua kutumia lugha za matusi dhidi yake binafsi, hatajutia kuchaguliwa kuiongoza tume hiyo kwa kuwa ilikusudia kuwaletea maendeleo wananchi wote kwa kuwapatia Katiba wanayoitaka.
Kauli hiyo ya Jaji Warioba imekuja wakati baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na viongozi wa CCM wakiikosoa Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba kwa maneno makali,huku wakimshutumu na kumkejeli yeye na baadhi ya wajumbe wa tume aliyoiongoza.
Akizungumza kwa mifano katika mahojiano na gazeti hili jana, Warioba alisema kuwa anawashashangaa wajumbe hao na viongozi wa CCM kwa kuacha kuijadili Rasimu ya Katiba, badala yake wanamkosoa yeye na kumsingizia maneno yasiyo ya kweli.
“Bulembo (Abdallah Bulembo mjumbe wa Bunge na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM) amenitukana, amenitukana… amesema niliwahi kupokea rushwa huku akijua kabisa kuwa ni uongo. Yeye ni kiongozi wa Kamati Kuu ya CCM, anasema uongo akijua ni uongo. Kwanza mimi simjui wala sijawahi kumwona huyu mtu naambiwa tu anatoka Mara,” alisema Jaji Warioba kwa sauti ya upole iliyoashiria kuumizwa.
Aliongeza kwamba siyo mara ya kwanza kwa Bulembo kumshambulia kwa lugha za matusi, kwani aliwahi kufanya hivyo tena kwenye moja ya mikutano ya CCM mkoani Tanga.
“Alifanya hivyo Tanga, anachokifanya siyo kitu cha mzaha kwa sababu anafahamu kilichotokea,” alisema.
Akizungumzia kauli aliyoitoa Waziri Hawa Ghasia wakati akichangia mjadala wa Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba aliyemtaka Jaji Warioba kufunga mdomo kutokana na kazi yake ya kuwasilisha Rasimu kumalizika, Jaji Warioba alisema: “Wao wanataka waseme uongo, mtu mwingine asiseme kitu.”
Warioba alieleza kuwa tangu lugha za matusi na kejeli zilipoanza kutolewa dhidi yake, baadhi ya watu walimshauri kwenda mahakamani kufungua kesi, lakini alikataa kwa kile alichodai kuliheshimu Bunge.
Alisema Bunge ndiyo lenye mamlaka ya kufuatilia na kudhibiti kauli zinazotolewa bungeni, kama wahusika hawafanyi hivyo hawezi kuchukua hatua yoyote.
“Kama kinga ya Bunge inatumika vibaya unafikiri mimi nitafanya nini? Sina nia ya kuchukua hatua, watu walipendekeza niende mahakamani, kuna wanasheria walisema hata nisipokwenda, wao watakwenda mahakamani nikawazuia,” alisema Warioba ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu.
Akisimulia kuhusu uchaguzi wa ubunge wa mwaka 1995 ambapo aligombea na kutuhumiwa kupokea rushwa na kufungiwa kwa miaka minne, Warioba alisema taarifa hizo siyo sahihi kwa kuwa aliyepokea rushwa ni aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya NCCR Mageuzi (wakati huo), Stephen Wassira ambaye sasa yuko CCM na ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu.
“Uchaguzi ule ulikuwa umejaa sana rushwa, tukaenda mahakamani, Wassira akafungiwa asigombee,” alisema.
Akizungumzia maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Warioba alisema: “Mimi ni muumini wa muungano, kwa miaka 50 taifa limekaa kwa amani, mshikamano na umoja. Ni kweli tumekuwa na matatizo lakini yanaweza kutafutiwa ufumbuzi.”
MWANANCHI

3 comments:

Anonymous said...

CCM ni chafu. ..huwezi kuwa ndani ya uchafu ukasema umsafi Judge Warioba...hongera kwa kutukumbusha rushwa aliyofanya Wassira...Nashindwa kuelewa alisafishika vipi na mahakama gani ilimuachia huru baada ya dhambi ya rushwa! Lakini tunarudi pale pale..CCM ni chafu na hata wewe Warioba umchafu ukiwa ndani ya umchafu:(...Rushwa imegeuzwa kuwa halali halafu tunashangaa maajabu ktk kila sekta:(...Binafsi nakuhurumia kwa sababu unaogopa Mamlaka..Kama ni matusi alianzisha mkuu wa nchi pale alipokwenda bungeni nakukosoa rasimu ya kazi aliyokutuma...wengine ni vidagaa tu usiumize kichwa. .Toka ndani ya uchafu! CCM si babio wala si mamio.

Anonymous said...

Mheshimiwa WARIOBA asante kwa maneno mazuri. Hakuna mTanzania na Mu Afrika mashariki asiyekubaliana na yote hayo. Warioba umekuwa kiongozi wa nyota ya pekee navuongozi wako wa utulivu una umri wa kutosha na busara ya kupumzika hivyo hawa wanaokutukana ni ukosefu wa nidhamu na kutokuwa na elimu ya uongozi sanasana wamejawa siasa ambayo nayo wanaitumia vibaya. Hongera tumia muda wako wa kustaafu uishi kwa amani.

The Inc said...

Waliomkashifu Warioba tatizo lao ni kutokuwa na elimu ya kutosha. Wanaishi maisha kama ya bendera, ambayo ni kufuata upepo tu. Hapo ndipo jkweli unapokuja kujidhihirisha kwamba nchi hii tumeikabidhi kwa viongozi walio wengi wasiokuwa na uweledi unaokidhi haja. Ukiitazama tume alokuwa akiongoza Jaji Mstaafu Warioba wajumbe wake na ukajaribu tu kuwalinganisha na asilimia 94 ya wajumbe wa Bunge maalum la katiba utaona mizania imeegemea wapi kiupeo na kimawazo vilevile. Tatizo ni uweledi wa wajumbe wa Bunge hili walio wengi ni mdogo mno.