Monday, May 19, 2014

FUKUZENI OKWI,NIYONZIMA NA KIIZA

Msola ndiye kocha pekee Mtanzania ambaye sasa ni daktari na aliyezinoa Taifa Stars na Kilimanjaro Stars na kumaliza muda wake akiwa na heshima kwa mashabiki.
KOCHA mzalendo ambaye ni msomi zaidi nchini,Mshindo Msola ametamka maneno ambayo viongozi wa kamati ya usajili ya Yanga wakisikia hata kama walikuwa na mpango wa kumpa kibarua kwenye benchi la ufundi watachanachana mkataba wake.
Msola ndiye kocha pekee Mtanzania ambaye sasa ni daktari na aliyezinoa Taifa Stars na Kilimanjaro Stars na kumaliza muda wake akiwa na heshima kwa mashabiki.

Kocha huyo ambaye hapendi kumung’unya maneno, ameiangalia Yanga ya sasa hususan wachezaji wao wa kigeni akatamka kwamba angembakiza beki Mbuyu Twite pekee na kusitisha mikataba ya wachezaji wengine wa nje kwa vile hawana hadhi ya Yanga na wala hawajitambui.

Msimu uliopita Yanga ilikuwa na wachezaji watano wa kigeni ambao ni Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza wote wa Uganda, Didier Kavumbagu wa Burundi (aliyehamia Azam FC), Haruna Niyonzima na Twite wote wa Rwanda.

Msola ambaye aliwahi kuinoa Reli ya Morogoro alisema amewafuatilia kwa karibu wachezaji wa kigeni walioichezea Yanga msimu uliopita, lakini ni Twite pekee aliyeonyesha mchango kwa timu hiyo.

“Kuna huyu Kavumbagu aliyejiunga na Azam ukweli ni kwamba hana uwezo wa kupambana kama mshambuliaji anavyotakiwa kuwa, huwa tunawaona akina Didier Drogba ambaye anaweza kukabwa na mabeki zaidi ya watatu lakini akafunga.

“Ukija kwa Kiiza leo utamwona amecheza vizuri kesho hovyo, kifupi si mchezaji ambaye unaweza kumtegemea wakati wote ni kama ana homa ya vipindi bado mchango wake ni duni sana kwa Yanga,”alisema Msola ambaye aliwahi kutishia kujiuzulu mwaka 2003 Taifa Stars iliposhindwa kufuzu Mataifa ya Afrika kutokana na sapoti ndogo ya Shirikisho na Serikali.

“Mwangalie Haruna Niyonzima mambo yake mengi anayofanya uwanjani si kwa faida ya timu ni kwa ajili ya kuwafurahisha mashabiki majukwaani,” aliongeza kocha huyo.

Kuhusu Twite ambaye ni kiraka, Msola alisema ndiye mchezaji pekee ambaye kiwango chake kimekuwa hakishuki na mchango wake umekuwa mkubwa kwenye kikosi cha Yanga kwa msimu mzima na anastahili kupata mshahara wa maana.

“Kama ningekuwa kocha wa Yanga leo hii, mchezaji ambaye ningembakiza katika usajili ni Twite, huyu kiwango chake kila siku utaona ni cha juu yaani huyu kweli ni mchezaji wa kulipwa,” alisema huku akimbeza Okwi aliyesajiliwa kwa Sh160 milioni kwenye usajili wa dirisha dogo.

“Okwi ni mchezaji mzuri lakini naye ningemwondoa kama ningekuwa kocha wa Yanga kwa sababu ya matatizo ya kukosa nidhamu ambayo kimsingi ni kitu muhimu kama unataka mafanikio ya jambo lolote, huwezi kumwendekeza mtu ambaye hana nidhamu ya kazi,”alisisitiza.

Yanga iko katika mzozo na straika wake, Okwi ambaye anashinikiza kumaliziwa dola 40,000 za usajili wake arudi uwanjani ingawa uongozi umesisitiza kwamba lazima wakae chini wapeane masharti mazito kwa vile wameingia gharama kubwa na mchezaji huyo hajafanya chochote kipya.
Credit:Mwanaspoti

No comments: