GIZA nene linazidi kujitokeza katika sakata la mapato yanayotokana na faini za bodaboda wanaoingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam kinyume na amri ya Mkuu wa Mkoa, kutokana na mapato hayo kutojulikana yanaingia katika mfuko upi hasa.
Uchunguzi na Tanzania Daima umebaini kuwa kuna stakabadhi halali za Jiji ambazo hazitumiki kutoza faini kwa wanaokamatwa kwa makosa hayo, badala yake zinatumika stakabadhi za zamani ambazo ukomo wake uliishia mwaka 2012.
Alipotafutwa kufafanua utata huo wa stakabadhi zinazotolewa mahakamani, ambapo licha ya kuwa ni feki na hata viwango vinavyoandikishwa sivyo vinavyolipwa, Mkurugenzi wa Jiji, Wilson Kabwe aliitupia lawama kwa idara ya mahakama kuwa wao ndio waulizwe stakabadhi hizo wanazipata wapi?
“Nenda kamuulize hakimu mahakama inazitoa wapi hizo stakabadhi, mimi sifahamu,”alijibu Kabwe.
Mahakama kwa upande wake, nayo ilijitoa katika lawama hiyo kwa kufafanua kuwa “katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive ina wafanyakazi tisa, wapo wanaotoka Ilala, Temeke na Kinondoni. Mahakimu wako wawili ila anayetoza malipo hayo anatoka ofisi ya Jiji na vitabu vya stakabadhi anavitoa huko”.
Mtoa stakabadhi hizo mahakamani ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, alipobanwa alisema stakabadhi hizo amekabidhiwa ofisi ya mkurugenzi wa Jiji ambaye hata hivyo alikuwa tayari amejivua lawama hizo na kutaka iulizwe mahakama.
Tangu gazeti hili lianze kuandika sakata hili, wamejitokeza watu wengi wenye ushahidi wa kutosha wanaolalamika juu ya suala hilo, huku mamlaka husika zikikwepa kujibu juu ya uhalali na adhabu wanazopewa waendesha pikipiki wanaoingia katikati ya Jiji.
Katika sakata hili, pia imebainika kuwa hata mali zinazokamata kwa wafanyabiashara huuzwa mapema kwa amri ya mahakama kama mali zilizookotwa kabla ya walionyang’anywa kulipa faini kwa kosa hilo.
Gazeti hili limearifiwa juu ya baiskeli 26, zilizokamatwa Kata ya Mchikichini mbele ya duka la mfanyabiashara, kisha zikauzwa kama mali iliyookotwa wakati wanafanya utaratibu wa kulipa faini.
Stakabadhi halali za Jiji la Dar es Salaam ambazo gazeti hili limeziona, zina nembo ya jiji, na upande wa chini kulia zina stika iliyoandikwa NPC KIUTA genuine, wakati stakabadhi halali za serikali kuu, zina nembo mbili za taifa na stika.
Hata hivyo, wakati mkuu wa mkoa akizuia pikipiki za biashara kuingia katikati ya jiji, imebainika kuwa ofisi ya mkurugenzi wa Jiji ilikuwa ikiendelea kutoa vibali kwa pikipi binafsi kuingia katikati ya jiji kwa malipo ya sh.360,000 kwa miezi sita, utaratibu ambao umesitishwa kwa tangazo la Mei 12, mwaka huu.
Mwanasheria ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake, alifafanua kuwa kazi ya kutoa vibali kwa matumizi ya vyombo vya moto kisheria hufanywa na Mamlaka ya Mapato kitengo cha kodi za ndani kwa vyombo vya moto vyenye namba zisizosajiliwa nchini.
Gazeti hili liliandika juu stakabadhi halali za serikali zinazotumika Mahakama kuu kuwa zina stika, nembo ya taifa juu katikati na nyingine chini upande wa kulia wa stakabadhi, alama ambazo hazionekani katika stakabadhi za malipo za mahakama ya hakimu mkazi Sokoine Drive kwa watuhumiwa waliokamatwa na kuhukumiwa kwa makosa ya kuingiza pikipiki katikati ya jiji.
Stakabadhi za mahakama kuu zinazotumika mwaka huu zinaanzia na namba 0808… na stika zake zina namba 19911….huku stakabadhi halali zinazotolewa na mahakama ya Ilala ambayo Sokoine Drive iko chini yake zinaanza na namba 0267… na stika zake zina namba 1241… wala hazianzi na namba 4321…zinazotumiwa mahakamani hapo kisha kuwaandikia walipaji kiwango pungufu na malipo yaliyofanyika.

No comments:
Post a Comment