ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 24, 2014

Vigogo ‘watosana’ ufisadi Escrow

KASHFA ya ufisadi wa dola za Marekani milioni 122 (sawa na sh. bilioni 200) katika akaunti ya Escrow ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imewaweka njia panda vigogo wa Serikali wanaotuhumiwa kuhusika kufuja fedha hizo, na sasa baadhi yao wamefikia hatua ya kutajana kama njia ya kukwepa mkono wa sheria.
Hatua hiyo, inatokana na mataifa makubwa yanayoifadhili Tanzania hususani katika sekta ya nishati ikiwemo serikali ya Uingereza, kufuatilia sakata hilo kwa ukaribu ili kuhakikisha ukweli unapatikana.

Katika kujaribu kuvuruga mjadala wa kashfa hiyo, wiki iliyopita ulisambazwa ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu za baadhi ya wabunge, ikimtuhumu mbunge wa Musoma mjini, Nimrodi Mkono (CCM) na Balozi wa Uingereza hapa nchini kuwa wanatembeza rushwa kwa wabunge ili wasiipitishe bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.

Hata hivyo, ujumbe huo ambao baadhi ya wabunge walidai kutumiwa na Waziri wa Nishati, Prof. Sospeter Muhongo, uliibua mgongano makali huku akitakiwa kuthibitisha tuhuma hizo kwa madai kwamba imekuwa kawaida yake kuzua uongo wa tuhuma za rushwa kila wizara yake inapobamwa.

Nao Ubalozi wa Uingereza nchini, umekanusha vikali tuhuma za kuhusishwa na mkakati wa kuwahonga wabunge ili wakwamishe bajeti, ukisema hauna sababu ya kufanya hivyo, japo wanafuatilia kwa umakini kashfa hiyo ili kuhakikisha ukweli unawekwa wazi.
Katika mbinyo huo, Tanzania Daima limedokezwa kuwa, tayari baadhi ya vigogo wanaotuhumiwa wameanza kujinasua huku kila mmoja akimnyooshea kidole mwenzake, akidai ndiye alihusika.

“Hali imekuwa tete, kila mmoja anajaribu kujinasua. Yuko waziri ameamua kumtosa katibu mkuu wake akidai ndiye alihusika kwa kushirikiana na ofisi ya mtuhumiwa mwingine (anamtaja) na kwamba yeye anaonewa kwa kuingizwa katika tuhuma hizo.

“Pia kuna kigogo mwingine ambaye katika kutaka kuzima sakata hili ameamua kutembeza fedha kwenye baadhi ya vyombo vya habari ili viache kabisa kuandika habari inayohusiana na kashfa hii au visafishe wizara yake,”kilidokeza chanzo hicho.

Pia kashfa hiyo inadaiwa kuitikisa zaidi Wizara ya Nishati na Madini ambapo baadhi ya watu wasiofahamika kutoka ndani ya wizara hiyo, wamekuwa wakisambaza ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, wakidai Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Regnald Mengi na Mkono ndio wanaeneza kashfa hiyo kwa lengo la kuwachafua Waziri Sospeter Muhongo na Katibu mkuu wake, Eliakim Maswi.

Kashfa hiyo iliibuliwa bungeni na mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), akiwataja vigogo sita wa serikali wakiwemo mawaziri kadhaa aliyodai wamehusika na ufisadi wa fedha hizo zilizokuwa zimewekwa katika akaunti ya Baraza la Usuluhishi la Migogoro ya Kibiashara (Escrow) BoT.

Kafulila aliwataja Waziri Muhongo, Maswi, Waziri wa Fedha Saada Mkuya, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Beno Ndullu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba.

Licha ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza suala hilo, Kafulila na wadau wengine wanataka iundwe Kamati Teule ya Bunge kwa kuwa linagusa mamlaka kubwa katika dola.

Ujumbe ambao unasambazwa kwenye simu za wabunge sasa unasomeka hivi; “Mhe Spika wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania. Sisi wabunge waadilifu tunakiri kwamba mhe Mkono ametufuata na kutupatia fedha kila mmoja milioni 3 ili tukwamishe Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini. Yupo hapa Dodoma anagawa fedha.

“Ametueleza kwamba tukifanikiwa, Balozi wa Uingereza atatuongezea sh milioni 5 kila mmoja. Balozi anapigania kesi ya IPTL na Standard Chartered ya UK. Mwanasheia wa Benki hiyo ni rafiki wa mhe Mkono. Waadilifu”.

Tayari Mkono amekiri kuwa amelalamika kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na kwamba amemwachia ashughulikie suala hilo.

Serikali ya Uingereza nayo kupitia kwa Balozi wake hapa nchini inafuatilia kwa ukaribu sakata hilo ambapo imetishia kusitisha msaada wa Euro milioni 71 kwa Tanzania ambao unalenga kuinua sekta ya umeme hadi ukweli uwekwe wazi.

Ni wazi kuwa Prof. Muhongo atakuwa kwenye mgogoro mkubwa na Bunge kwani itakumbuka kuwa Julai 28 mwaka 2012, wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara yake, aliwatuhumu baadhi ya wabunge kuwa walihongwa na makampuni ya mafuta ili kukwamisha bajeti yake.

Waziri Muhongo alitoa tuhuma hizo baada ya kubanwa pamoja na Katibu Mkuu wake, wakituhumiwa kutoa zabuni kinyemera kwa Kampuni ya Puma Energy ya kuiuzia Tanesco mafuta mazito.

Prof. Muhongo alidai kuwa Tanesco ilinunua misumari kwa pauni 50,000 badala ya spea. Kwamba baadhi ya wabunge wakiwamo wale wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wanafanya biashara na Tanesco, ambapo kampuni ya mbunge mmoja ililiuzia shirika hilo mataili mabovu.

Hata hivyo, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyochunguza tuhuma hizo, ilithibitisha kwamba hakukuwa na jambo kama hilo isipokuwa Waziri Muhongo alisema uongo.

Kashfa hiyo ya Escrow huenda ikakipa taabu na hata kuking’oa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama ilivyotokea kwa chama tawala cha KANU cha nchini Kenya mwaka 2002.

Mmiliki wa Kampuni ya PAP inayodai kuinunua Kampuni ya IPTL yenye mgogoro na Tanesco, Habinder Singh Sethi anatajwa kuhusika katika kashfa kubwa ya ufisadi nchini Kenya ya Goldenberg, uliogharimu takribani dola milioni 600.

Ufisadi huo pia ulihusisha mahakama, watendaji, viongozi na wanasiasa wakubwa nchini humo, ikiwemo familia ya aliyekuwa Rais wa wakati huo, Daniel Arap Moi.

Akaunti hiyo ilifunguliwa mwaka 2004 kutokana na mgogoro wa kibiashara kati ya IPTL na Tanesco ambapo Tanesco ilipeleka shauri hilo kulalamikia gharama kubwa wanazotozwa na IPTL.

PAP inadai kuinunua IPTL kutoka kwa Merchar iliyokuwa ikimiliki asilimia 70 ya hisa na VIP iliyokuwa na umiliki wa asilimia 30.

Mbatia amuonya Muhongo

Mbunge wa kuteliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), amemtaka Waziri Muhongo kutotumia ugomvi wake binafsi na Mengi kulivuruga Bunge.

Mbatia alitoa kauli hiyo bungeni jana mara baada ya kipindi cha maswali na majibu wakati akiomba muongozo kuhusu majibu ya swali lake la nyongeza aliyojibiwa na Prof. Muhongo.

Mbatia alisema wakati anauliza swali lake kuhusu serikali kuwawezesha wachimbaji wa chumvi, Prof. Muhongo alijibu swali hilo kwa kuingiza ugomvi wake na Mengi.

“Kanuni zinasema Waziri anayeulizwa swali atakuwa na wajibu wa kujibu swali kwa uadilifu. Kanuni ya 64 (a) inayohusu mjadiliano ndani ya Bunge inaeleza kwamba majadiliano hayo yatahifadhi uhuru wa mawazo,” alisema.

Mbatia alisema kanuni hiyo inaleza kwamba mbunge hatatoa taarifa zisizo na ukweli na hatatumia lugha ya kuudhi ya kuwadhalilisha watu wengine.

“Niliuliza swali kuhusu kuwawezesha wakulima wadogo wa chumvi wa Singida na Uvinza, ni wakulima wadogo sikutaja mtu.

“Ipo sheria ya kuwawezesha wazawa na ndo maana tukawa na mabilioni ya JK, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi pia inazungumzia kuwawezesha wazawa wa nchi hii, Rais anasema kila mara kuhusu kuwawezesha wazawa watanzania wa kawaida ili wanyanyuke vizuri.

“Prof. Muhongo wakati anajibu swali langu ametumia lugha ya kuudhi, mimi nilikuwa nikijadili hoja siyo mtu, kama ana ugomvi binafsi na Reginald Mengi, ugomvi wao usisababishe amani na utulivu ndani ya Bunge ikaondoka,”alisema Mbatia.

Mbatia alisema hata hivyo, Mengi ana haki kama Watazania wengine wa kuwezeshwa akiwa kama mzawa.

Awali akijibu swali la nyongeza la Mbatia, Prof. Muhongo alisema serikali imekuwa ikiwawezesha wazawa wakiwemo wazalishaji wa chumvi. Alisema wazawa hao wamekuwa wakipewa ruzuku kupitia vikundi vyao kwa kupitia Benki ya Uwekezaji TIB.

“Kwa hiyo hili suala lisikuzwe kwa kuwa tu yupo mtu fulani analalamika kwamba hakusaidiwa, serikali imekuwa ikiwawezesha wazawa ikiwemo kuwapatia ruzuku kupitia TIB,” alisema.

No comments: