Dar-Es-Salaamu yapendeza kwa vile bahari ya hindi ya pendezesha jiji hili linye raha na karaha za kidunia.
WAHENGA wanasema, penye raha na karaha ipo. Ni ukweli usiopingika kwamba watu wengi wanapenda maisha ya mjini kuliko maisha ya kijijini lakini kwa mitazamo tofauti waliyonayo.
Kuna baadhi ya watu wanatamani kuishi mijini kwa sababu ya kunapatikana huduma nyingi za kijamii kama vile shule, hospitali, usafiri wa uhakika, masoko pamoja na upatikanaji wa mahitaji mengine ya maisha ya kila siku. Lakini mjini ndiko kuna idadi kubwa ya watu kuliko kijijini.
Mjini pia kupatikana ajira mbalimbali kutokana na ukweli kwamba viwanda vingi hujengwa mjini au nje kidogo ya mji na kuajiri wafanyakazi ambao wengi wanaishi mjini. Hii nayo ni sababu moja inayofanya mjini kuvutie zaidi kuliko vijijini. Lakini baadhi ya watu wenye mitazamo tofauti na hayo niliyosema hapo awali. Wao wanaona kwamba pamoja na mazuri yaliyopo mjini lakini bado mjini kuna kero nyingi kuliko vijijini.
Penye mengi pana mengi. Hii inatokana na kwamba jamii kubwa inayoishi pamoja kwa muda mrefu ni dhahiri kwamba kuna mambo mengi mabaya yanatokea ikiwamo ukabaji, ubakaji, uporaji, utapeli, pamoja na mambo mengine yasiyopendeza. Hali hii ni tishio kwa watu waliozoea maisha ya utulivu na amani japokuwa wanakosa starehe zinazopatikana mjini.
Dar es Salaam ni jiji la raha na starehe za kila aina, lakini ni sehemu iliyojaa maovu, vituko na mikasa ya kila aina. Jiji hili limepambika vilivyo katika maeneo yenye majengo marefu(maghorofa), barabara za lami na maduka aliyojaa bidhaa kama vile nguo za kiume na za kike, viatu nk. Kuna kumbi za starehe katika kila wilaya za jiji hili ambazo ni Ilala, Kinondoni na Temeke.
Bendi nyingi za muziki wa kila aina zipo Dar es Salaam pamoja na miziki ya kizazi kipya inayosikika kwenye redio na televisheni mbalimbali. Pia kuna fukwe za kupumzikia zinazovutia watalii. Lakini pia ipo bandari kubwa inayojaza meli nyingi za abiria na za mizigo ya ukubwa mbalimbali zinazotoka sehemu mbalimbali dunia. Tunapozungumzia Dar es Salaam hakika hatuwezi kusahau kuutaja uwanja wa ndege wa kimataifa unaoruhusu kutua ndege kutoka nchi mbalimbali.
Ni uwanja mkubwa unaojulikana kwa jina la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Kuwapo kwa uwanja huu kumerahisisha usafiri wa anga kwenda na kutoka mahali popote kuja Dar es Salaam. Ukiachilia raha zinazopatikana katika jiji hili, lakini kuna baadhi ya watu wanalichukia licha ya kuwa raha.
Kuna mambo mengi yanayochukiza pamoja na kero nyingi kama uporaji wa vitu mbalimbali kutoka wa wananchi, kwani kuna vibaka ambao wao kumkaba na kumnyang’anya mtu kitu alichokuwa nacho iwe ni pesa au simu wao hawaoni shida.
Mtu anapokuwa amebeba mkoba wake au pochi mkononi basi huwa amejitangazia vita na vibaka hata kama begi hilo lina makaratasi au vitu vingine visivyo na maana yoyote. Lakini si hayo tu, bali kuna balaa kubwa pale mtu anapokuwa kashika simu ya gharama anazungumza huku anatembea hasa sokoni kariakoo au mtaa wa kongo ujue kitakachofanyika ni kuibiwa.
Ukikabidhi pesa au kitu chochote kwa mtu unayemuamini ili amfikishie mtu fulani, basi usishangae kuona kuwa hakuna kitachofika pale palipo kusudiwa kifike. Baadhi ya wafanyabiashara ndogondogo nao wana mambo yao ya ajabu yasiyoelezeka kwani wao hufukuzana na askari kila siku kuhusiana na kutouzia biashara zao eneo husika.
Wafanyabiashara hao hupanga bidhaa zao sehemu zilizopigwa marufuku hali inayosababisha askari wa jiji kuwafukuza lakini kesho yake wafanyabiashara hao hupanga pale pale walipokatazwa jana. Tunapoangalia hali ya mazingira katika jiji hili utaona kwamba hali ni mbaya. Takataka zimezagaa sana mitaani kiasi cha kuonekana kama kuna madampo barabarani.
Harufu mbaya ya takataka hizi pamoja na mitaro ya maji machafu yanayotoka kwenye makaro ya vyoo, inakuwa ni kero kubwa kwa wakazi wa jiji. Baadhi ya nyumba zilizojengwa maeneo ambayo si katika kati ya jiji hazina mpangilio tunaweza kusema ni vurugu tupu.
Kila mtu kajenga kimpango wake. Haishangazi kuona mtu anajenga nyumba yake lakini sehemu ya choo chake ipo karibu na baraza au chumba cha kulia chakula.

No comments:
Post a Comment