ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 1, 2014

JK kuhutubia wafanyakazi, Tucta yalilia mishahara

Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolas Mgaya.PICHA|MAKTABA

Dar na mikoani. Wakati Rais Jakaya Kikwete akitarajiwa kuhutubia wafanyakazi katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), limeitaka Serikali kupandisha kima cha chini hadi kufikia Sh750,000.
Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolas Mgaya alisema jana kuwa wanahitaji kuona wafanyakazi wakipata kiwango cha mshahara kinachokidhi mahitaji.
Alisema kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi na mfumuko mkubwa wa bei uliopo kwa sasa, kiwango hicho angalau kinaweza kukidhi mahitaji muhimu ya wafanyakazi wa kima cha chini, ikiwamo malazi, mavazi, chakula na mahitaji ya afya.
“Katika hali halisi, tunaona namna bei za vitu muhimu ikiwamo umeme, maji, mafuta, gharama za vifaa vya ujenzi, nyumba vyakula na gharama nyingine za maisha zimekuwa zikipanda maradufu katika miaka ya karibuni, lakini hakuna namna inayofanyika kuleta unafuu kwa wafanyakazi.
Kimsingi kima cha chini lazima kiongezwe ili kikidhi mahitaji ya maisha ya wakati huu,” alisema.
Dar mwenyeji
Akizungumzia sherehe hizo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema kabla ya Rais Kikwete kulihutubia taifa, atapokea maandamano ya wafanyakazi yatakayoanzia Viwanja vya Mnazi Mmoja saa 1:00 asubuhi.
Alisema maadhimisho ya mwaka huu yenye kaulimbiu ya ‘Utawala Bora utumike kutatua kero za wafanyakazi’, yatatoa fursa kwa wafanyakazi kujumuika pamoja na wenzao duniani.
Sherehe Pwani
Mwenyekiti wa Tucta Mkoa wa Pwani, Paulo Msilu alisema maadhimisho hayo yanafanyika huku Serikali ikiwa bado si sikivu kwa kushindwa kutekeleza ahadi mbalimbali kwa wafanyakazi.
“Licha ya kuwekwa bayana, lakini yamekuwa hayatekelezwi zaidi ya ahadi za kupatiwa ufumbuzi,” alisema.
Aliyataja baadhi ya madai ya msingi ya wafanyakazi kuwa ni stahili za walimu ikiwamo malimbikizo ya likizo, na kupandishwa madaraja... “Tunakwenda kwenye Mei Mosi lakini wafanyakazi wamekata tamaa,” alisema Msilu.
Msilu alisema, kimkoa wamejiandaa vyema kushiriki sherehe hizo zitakazofanyika kwenye Viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha.
Maadhimisho Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera atapokea maandamano ya wafanyakazi kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Katibu wa Tucta, Mkoa wa Morogoro, Charles Luvunzu alisema maandamano ya maadhimisho hayo yataanzia katika Ofisi za Tucta Mkoa wa Morogoro zilizopo Barabara ya Reli.
“Kutakuwa na utoaji wa vyeti na zawadi mbalimbali kwa wafanyakazi bora wa mwaka ambazo zitatolewa na vyama husika,” alisema. Aliwataka wafanyakazi wote wa Morogoro na wananchi kujitokeza kushuhudia maonyesho hayo yatakayohusisha vifaa vinavyotengenezwa na mashirika, taasisi na kampuni mbalimbali.
Moshi watimuana
Katibu wa Kanda ya Kaskazini wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Habari na utafiti (Raawu), Thomas Kasombwe amesimamishwa kazi ghafla na uongozi wa juu.
Kasombwe, ndiye aliyekuwa akiratibu maadhimisho ya Mei Mosi Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuwa Raawu ndicho kilichoteuliwa mwaka huu kuratibu maadhimisho hayo. Habari za uhakika zilizopatikana jana, zilieleza kuwa katibu huyo alipokea barua ya kusimamishwa kazi Jumatatu wiki hii, taarifa ambazo zilisababisha kikao cha maandalizi ya siku hiyo kuvunjika.
Alipoulizwa jana, Kasombwe alikiri kusimamishwa kazi lakini akasema atatoa ufafanuzi juu ya sakata hilo baadaye akisisitiza hadi sasa bado hajui msingi wa kisheria wa hatua hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Raawu ya Wanawake Kanda ya Kaskazini, Immaculate Mrema, alithibitisha kusimamishwa kazi kwa katibu huyo lakini hakuwa tayari kuzungumzia zaidi suala hilo.
Akizungumzia maandalizi ya Mei Mosi, Mrema alisema maandamano ya wafanyakazi pamoja na vitendea kazi vyao yataanzia Jengo la Kahawa saa 1:00 asubuhi na yataishia Uwanja wa Ushirika.

Mei Mosi Iringa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma anatarajiwa kuongoza maadhimisho hayo kwenye Viwanja vya Kanisa Katoliki, Isimani.
Mratibu wa maadhimisho hayo Mkoa wa Iringa, Hillary Kitipwi alisema mwaka huu, sherehe hizo zitafanyika kimkoa katika Tarafa ya Isimani yakishirikisha viongozi wote wa vyama vya wafanyakazi kutoka katika matawi mbalimbali na wanachama wao.
Alisema sherehe hizo zitatanguliwa na maandamano ambayo yatapokewa na Mkuu wa Mkoa kabla ya kutoa zawadi kwa wafanyakazi bora kutoka katika sekta mbalimbali.
Imeandikwa na Andrew Msechu (Dar), Fina Lyimo na Daniel Mjema (Moshi), Geofrey Nyang’oro (Iringa) na Julieth Ngarabali (Pwani).
Mwananchi

No comments: