ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 22, 2014

Kamati ya Bunge yataka fungu maalum kuondoa foleni Dar

Mtutura Abdallah Mtutura
Kamati ya Bunge ya Miundombinu imetaka kutenga kwa fungu maalum kwa ajili ya kutatua msongamano wa magari jijini Dar es Salaam kuliko kutegemea fedha kutoka kwenye bajeti ambazo ni ndogo na zimeshindwa kuutatua.

Akisoma taarifa ya kamati kwa niaba ya Kamati, Mtutura Abdallah Mtutura, alisema kwa miaka kadhaa wameshauri jinsi ya kutatua tatizo la msongamano Dar es Salaam kutokana na ukubwa wa jiji ambalo linachangia asilimia 75 ya mapato.

Alisema nchi nyingi duniani ikiwamo Kenya wametatua tatizo la msongamano wa magari katika miji mikubwa kwa kutenga fedha maalum na kujenga barabara za juu kwenye maungano ya barabara muhimu za ndani ya jiji zinazokwenda nje ya jiji.


“Ni muhimu serikali ikaamua sasa kwa sababu kadri inavyochelewa gharama za utatuzi wa msongamano zinaendelea kuongezeka,” alisema.

Mtutura alisema licha ya kuwapo kwa barabara nyingi za mzunguko, lakini serikali ina wajibu wa kutilia mkazo barabara za pete (ring roads) ili kufungua Jiji la Dar es Salaam kwa maeneo mengi ambayo yana tatizo la msongamano.

Alisema kamati inakubaliana na kuanzishwa kwa usafiri wa boti kutoka Bagamoyo hadi Dar es Salaam, lakini hauwezi kutatua kero za msongamano wa magari katika maeneo yote ya jiji.

Aidha, alisema kamati inasisitiza upanuzi wa daraja la Salender, Gerezani na makutano ya barabara ya Nyerere na Chang’ombe, Ubungo, Fire, Morroco, Mwenge na nyingine na kwamba iende sambamba na kutengenezwa kwa barabara za pete na barabara mlishon (feeder roads).

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: