ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 5, 2014

Kocha asema Azam imechemsha kumsajili straika Kavumbagu.

Didier Kavumbagu.
Hivi karibuni Azam ilimsajili Kavumbagu kwa mkataba wa mwaka mmoja na kiungo Frank Domayo pia kutoka Yanga kwa mkataba wa miaka miwili, hata hivyo kwa Domayo amesema Azam imelamba dume.
KOCHA Charles Kilinda, amechambua usajili unaoendelea kufanywa katika timu za Ligi Kuu Bara kwa ajili ya msimu ujao na hasa ule wa mabingwa wapya, Azam FC, akisema ‘wamebugi’ kwa mshambuliaji Mrundi Didier Kavumbagu aliyekuwa Yanga.

Hivi karibuni Azam ilimsajili Kavumbagu kwa mkataba wa mwaka mmoja na kiungo Frank Domayo pia kutoka Yanga kwa mkataba wa miaka miwili, hata hivyo kwa Domayo amesema Azam imelamba dume.

Kilinda aliliambia Mwanaspoti kuwa anamfahamu Kavumbagu tangu alipoanza kuichezea Yanga misimu miwili iliyopita na kudai hakuwa mshambuliaji wa kuisadia timu hasa katika michuano ya kimataifa.

“Sikutarajia kama Azam wangefanya usajili wa Kavumbagu, kwa fedha walizonazo, walitakiwa watafute mshambuliaji mahiri kuliko yeye,” alisema Kilinda ambaye ni kocha wa zamani wa JKT Ruvu.

“Kavumbagu ameshindwa kuisadia Yanga kipindi chote alichokuwapo sasa ataweza kwa Azam? Kiwango chake cha sasa siyo kiwango kile cha zamani, Azam walitakiwa kutoka nje na si kumchukua mchezaji hapa hapa Tanzania kwa nafasi hiyo. Ila kwa Domayo wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa na atawasaidia.”

Akifafanua zaidi kuhusu Domayo, Kilinda alisema: “Namfahamu Domayo na mimi ndiye niliyemwibua nikiwa na JKT Ruvu, ana kipaji, anajituma mazoezini, ana nidhamu ndani na nje ya uwanja na umri wake bado mdogo, hivyo atafika mbali zaidi.”

Kilinda ameishauri Azam kuhakikisha inajiandaa vizuri katika michuano ya kimataifa hasa Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Wametwaa ubingwa ambao walijiandaa kuusaka kwa kipindi kirefu, wamepata nafasi ya kushiriki michuano ya Afrika, sasa wanahitaji kufanya maandalizi mazuri na ya muda mfupi, Yanga na Simba wameshindwa hivyo tunatarajia kuona mabadiliko kutoka kwao,” alisema Kilinda.

No comments: