ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 21, 2014

KUAMBIANA AZIKWA NA MASWALI MAGUMU 5


ADAM Philip Kuambiana amezikwa jana kwenye Makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam huku akiacha maswali magumu matano kuhusu maisha, mazingira na hatimaye kifo chake, Risasi Mchanganyiko linakupa moja kwa moja.
Mwili wa marehemu Kuambiana ukiwasili kaburini tayari kwa shughuli za kuusitiri.
Marehemu Kuambiana alifariki dunia Jumamosi iliyopita asubuhi akikimbizwa kwenye Hospitali ya Mama Ngoma, Mwenge jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu baada ya kuugua tumbo ghafla.
MANENO KUTOKA KWENYE MIDOMO YA WATU
Baada ya kifo chake, maneno kutoka kwenye vinywa vya watu yalionesha ni maswali magumu ambayo majibu yake yangepatikana kama marehemu angekuwa hai.
Hata hivyo, Risasi Mchanganyiko lilifanya kazi ya ziada kuhakikisha maswali hayo yanapata majibu kwa ndugu au watu wa karibu na marehemu.
Jeneza likishushwa kaburini.
MASWALI MAGUMU MATANO
Maswali ya watu kuhusu marehemu Kuambiana yako matano ambayo baadhi ya wasomaji walitoa ombi kwa Magazeti Pendwa ya Global kuyafanyia kazi na kutoa majibu yake kwa vile uwezo huo kwa Global upo.
SWALI LA KWANZA
Inadaiwa kuwa asubuhi ya kifo chake, marehemu na wasanii wenzake walikuwa kambini, Sinza jijini Dar. Wasanii hao walimgongea mlango kwa sababu walitakiwa kwenda kurekodi filamu wakakuta mlango uko wazi, wakaingia.
Mke wa marehemu Janeth Rithe ambaye ni Diwani Kata ya Kunduchi (Chadema), akiweka shada la maua kwenye kaburi la mumewe.
Je, ni kwa nini marehemu aliacha mlango wazi wakati kuna maelezo kwamba alikuwa akilala na vifaa vingine vya kufanyia kazi?
Stara Thomas ambaye amewahi kuwa mchumba wa marehemu, anajibu hili:
“Ninavyojua mimi Kuambiana alikuwa anavuta sana sigara. Mara nyingi akitaka kuvuta alikuwa akitoka nje. Sasa huenda alfajiri ya siku hiyo alifungua mlango akatoka kuvuta aliporudi hakuufunga tena.”
SWALI LA PILI
Yapo madai kwamba, siku hiyo marehemu alikuwa na fedha nyingi. Hilo linaweza kuthibitishwa na rafiki wa karibu wa marehemu ambaye alisema kuwa, Ijumaa, yaani siku moja kabla ya kifo, Kuambiana alikuwa na fedha nyingi.
Davina akibebwa baada ya kuzidiwa wakati wa kuuaga mwili wa marehemu Adam Kuambiana kwenye Viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar.
Kuhalalisha hilo, hata mhasibu wa Gesti ya Silvarado, Sinza jijini Dar ambayo marehemu na wasanii wake waliitumia kupiga kambi kwa ajili ya kurekodia filamu alisema walikuwa wakimdai shilingi milioni mbili na siku hiyo ya Ijumaa alilipa keshi.
Swali ni je! Kama marahemu alikuwa na fedha nyingi japokuwa hakijajulikana kiasi, baada ya kifo chake zilichukuliwa na nani na ameziweka wapi?
NDUGU WA MAREHEMU ANAJIBU
Ndugu wa marehemu ambaye alisema si msemaji wa familia na akaomba jina lake lisitajwe, alisema anachojua yeye marehemu hakukutwa na hata senti tano mfukoni.
Msanii wa Filamu Bongo, Jini Kabula akiaga mwili kwa machungu.
“Hilo la kusema alikuwa na fedha siku hiyo hata sisi tunasikia tu. Lakini sisi kama familia tunajua hakukutwa na pesa licha ya kwamba tumesikia alikuwa akiwapa ofa watu kwenye mabaa. Kuna mtu nasikia alitoweka nazo, tunamsaka kila kona.”
SWALI LA TATU
Wengi wanatatizwa na makazi ya marehemu kwamba mtu angetaka kumpata Kuambiana angekwenda wapi maana mara nyingi alikuwa akionekana kwenye baa mbalimbali za jijini Dar hasa maeneo ya Sinza.
“Mimi nimewahi kusikia kwamba, Kuambiana alikuwa hana makazi. Alipokutana na Stara Thomas ndiyo akawa anaishi kwake, walipomwagana ikawa mwendo ni uleule.
“Nimewahi kusikia kuwa alipokuwa akipewa tenda ya filamu ndiyo makazi yake yalikuwa kambini. Lakini sina hakina sana makazi yake japokuwa  na mimi ni msanii wa filamu kama alivyokuwa yeye,” alisema mwigizaji mmoja akiomba asindikwe gazetini.
Msanii wa filamu, Richie Richie akiweka udongo kwenye kaburi la marehemu Kuambiana
STARA ATAJA MIKOCHENI
Risasi Mchanganyiko lilizungumza tena na Stara ambaye alijibu:
“Mimi aliniambia makazi yake yalikuwa Mikocheni (Dar) lakini sikuwahi kufika. Lakini ninavyojua ni Mikocheni.”
Akizungumza na gazeti hili msibani kwa mke wa marehemu, Bunju jijini Dar, ndugu mmoja alisema anavyojua yeye marehemu alikuwa akiishi Bunju B.
SWALI LA NNE
Baadhi ya mastaa walisikika wakisema baada ya kuachana na Stara, marehemu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na msanii wa filamu anayeitwa Lulu Jumanne ‘Selina’ Lakini swali likawa je, ni kweli?
Kaburi la marehemu Adam Philip Kuambiana, muda mfupi baada ya shughuli za maziko kukamilika.
RISASI LAMSAKA, LAMPATA SELINA
“Ni kweli mimi na Kuambiana tulikuwa wapenzi. Baada ya kuachana na mke wake wa ndoa (Janeth) alikuja kwangu tukaishi wote, lakini baadaye tukaachana, nikasikia yuko na Stara.
“Hata hivyo walikorofishana na kurudi tena kwangu,” alisema Selina ambaye ndiye mpenzi wa marehemu hadi kifo chake.
SWALI LA TANO
Swali la tano ni kuhusu filamu aliyokuwa akiishuti marehemu ambayo kaiacha katikati inayoitwa Jojo. Marehemu alisema ni yake lakini kuna madai kwamba, Stara Thomas naye anadai ni ya kwake.
Risasi Mchanganyiko lilimsaka Stara juzi kuhusu madai hayo ambapo alisema:
“Mimi sina tatizo, kama marehemu alisema ni yake sawa tu. Ila ilikuwa ya kwetu sote. Hata ikijulikana ni yake sidhani kama ni tatizo.”
Adam Philip Kuambiana enzi za uhai wake.
AZIKWA
Marehemu Kuambiana alizikwa jana katika Makaburi ya Kinondoni, Dar ikitanguliwa na misa iliyosomwa katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni ambapo aliagwa.
Mastaa kibao walifurika viwanjani hapo lakini wengi waliishiwa nguvu, kuanguka na kupoteza fahamu.
Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya shujaa Kuambiana – Amina.

No comments: