ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 6, 2014

Mabasi yaendayo kasi kuanza kazi mwakani

Serikali inatarajia kuanza kutoa huduma za awali katika mradi wa mabasi yaendayo kasi (Dart) kutoka Kimara Mwisho hadi Kivukoni, jijini Dar es Salaam baada ya miundombinu yake kukamilika mwaka ujao.

Hayo yalisemwa na Meneja Uhusiano wa Dart, William Gatambi, wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Alisema mara baada ya kukamilika kwa miundombinu ya mradi huo awamu ya kwanza mwishoni mwa mwaka 2014, itasadia kufanikisha usafiri wenye tija kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam na vitongoji vyake.

Alisema miundombinu hiyo inajumuisha barabara ya kilomita 20.9 kuanzia Kimara Mwisho hadi Kivukoni, barabara ya Kawawa kutoka Morocco hadi Magomeni na barabara ya Msimbazi hadi eneo la Gerezani Kariakoo.

Gatambi alisema mradi huo utakuwa na vituo vidogo 27, vituo vikuu vitano, vituo mlisho vine, karakana mbili na njia za waenda kwa miguu na baiskeli.

Akifafanua, Gatambi alisema mradi wa majaribio utaanza na mabasi 20 yatakayokuwa na uwezo wa kuchukua abiria kati ya 145 hadi 160 kwa wakati mmoja, hali itakayosaidia kuondoa kabisa kadhia ya usafiri kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

Aidha, katika mradi huo wa majaribio Gatambi amesema kutakuwa na mabasi mengine 10 yenye uwezo wa kuchukua abiria kati ya 50 na 60 ambayo yatatumika kuchukua abiria kutoka pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam kwenda katika vituo vikuu vya mabasi yaendayo kasi.

Kwa upande wake, Meneja Usimamizi wa Barabara wa Dart, Mohamed Kuganda, alisema mradi huo utasaidia kuondoa tatizo la foleni jijini Dar es Salaam na wananchi kupata huduma ya usafiri yenye kukidhi viwango vya kimataifa.

Pia Kuganda alisema Dart kwa kushirikiana na halmashauri za jiji la Dar es Salaam inafanya maandalizi ya kuboresha barabara mlisho (feeder roads) katika maeneo yatakayotumiwa na mabasi mlisho.

Katika mradi wa mabasi yaendayo kasi kutakuwa na vituo vikuu (terminals) vitano 5 katika, maeneo ya Kimara, Ubungo, Morocco, Kariakoo na Kivukoni na katika vituo hivyo ndiko mabasi yatakakokuwa yanaanzia na kumalizia safari kubadilishana abiria kati ya njia kuu na njia mlisho.

Vituo hivyo pia vitakuwa na huduma mbalimbali ikiwamo maeneo ya kukatia tiketi na vyoo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: