Friday, May 30, 2014

Mnyika kumburuza Maghembe kortini

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika, anakusudia kumshitaki Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, kwa madai ya kumnyima nyaraka zinazohusiana na miradi ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mnyika amesema kuwa anataka mahakama imlazimishe Waziri Maghembe, azitoe nyaraka hizo ili mbunge huyo azifanyie kazi anayokusudia.
Akizungumza na Tanzania Daima, wakili wa Mnyika, John Mallya, alisema amepokea maelekezo kutoka kwa mbunge huyo kufungua kesi hiyo.

Alibainisha kuwa Mnyika anataka nyaraka hizo zimsaidie kuwakilisha wananchi, kuisimamia na kuishauri serikali.

Kwa mujibu wa wakili, wengine watakaojumuishwa katika kesi hiyo ni pamoja na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Fredrick Werema.

Wakili Mallya, alisema mteja wake aliomba nyaraka hizo na kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge, alishafuata taratibu zote husika, lakini Waziri Maghembe hakumpa nyaraka hizo.

Mallya, alisema Mnyika alishamuandikia barua Prof. Maghembe, kuomba nyaraka hizo tangu Januari 3 mwaka 2013 kisha kumkumbusha tena Mei mwaka huu, lakini hatoi majibu.

Mnyika pia anataka mikataba yote ya maji inayotekelezwa katika jimbo la Ubungo ikiwa pamoja na fedha za mikopo ya ndani na nje pamoja na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali za mwaka 2010 hadi 2013, zilizokaguliwa.

Januari mwaka huu, mbunge huyo alimtaka Prof. Maghembe ajiuzulu kutokana na kujirudia rudia kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar es Salaam kinyume na maelezo yake aliyoyatoa bungeni Februari 4 mwaka jana.
CREDIT:MTANZANIA DAIMA

No comments: