Friday, May 30, 2014

Bunge lawaka moto


WABUNGE wa Kambi Rasmi ya Upinzani wakitoka nje ya ukumbi wa Bunge

WABUNGE wa Kambi Rasmi ya Upinzani, jana walitoka nje ya ukumbi wa Bunge, kususia uhitimishaji wa mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.

Wabunge hao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), waliamua kususia mjadala huo kwa madai ya kutoridhishwa na ulivyokuwa ukiendeshwa kwa mikakati waliyowekeana wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kufukia kashfa nzito ya IPTL inayoikabili wizara hiyo.

Kabla ya kutoka nje ya Bunge, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe (CHADEMA), alisema hawako tayari kuendelea kushirikiana mjadala huo wakati tayari CCM na serikali yake wameshaweka msimamo wa kuwazomea na kupinga kila hoja ya wabunge wa upinzani.

Mbowe, alisema amefuatilia mjadala huo, lakini kwa bahati mbaya umegubikwa na minyukano ya kiitikadi na makundi.

Alisema wabunge wanajadili kwa kujaribu kufukia mambo mazito kwa sababu ya mitazamo ya makundi na kiitikadi, hivyo sio busara kuendelea kushiriki.

“Mheshimiwa Spika, nashawishika kabisa kusema kuendelea kushiriki mjadala huu ni sawa na kutowatendea haki wananchi wetu, sina matatizo na Waziri Muhongo, wala katibu wake, tatizo langu ni mfumo. Waheshimiwa wabunge, hebu someni hotuba yetu mjue tunasema nini.

“Watu hamsomi, hamfanyi utafiti, lakini mmeshaweka misimamo kwa kutumia uwingi wenu, hatuwezi kushiriki mjadala kama huu tunapoona mambo yanachakachuliwa waziwazi, kuendelea kushiriki mjadala huu ni kulinajisi taifa, ni bora tuwaachie mjadala huu muhitimishe nia yenu kwa raha,” alisema Mbowe.

Huku akizomewa na wabunge wa CCM, Mbowe alisema wizara hii ina kashfa kubwa ya IPTL, na kuna ripoti nyingi ya tume zilizoundwa na maazimio ya Bunge, lakini yameendelea kukaliwa bila sababu.

Baada ya kauli hiyo, Mbowe, alianza kutoka nje na kufuatiwa na wabunge wote wa kambi rasmi ya upinzani bungeni.

Wakati wanatoka, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema wabunge hao wametoka kuhofia majibu ya Waziri Muhongo.

“Wao wanasema sisi tumepanga mikakati, sio kweli, wao ndio waliopanga mchana huu kwamba watoke kumhofia Muhongo,” alisema Lukuvi.

Nje ya Bunge

Akizungumza na waandishi katika Ukumbi wa Pius Msekwa, Mbowe alisema wametoka kwa sababu tatu ambazo ni pamoja na CCM kupanga mkakati wa kuwazomea wakati Waziri Muhongo atakapokuwa anahitimisha hoja yake.

Pili alisema wabunge wa upinzani John Mnyika na David Kafulila, walipojaribu kuibua hoja ya kashfa ya ITPL, walilazimishwa kutoa ushahidi hapo hapo kwa lengo la kuwatisha, na wamepanga kukataa hoja ya kutaka iundwe Kamati Teule kuchunguza kashfa hiyo.

Kwa mujibu wa Mbowe, sababu ya tatu ni wizara hiyo kukalia ripoti za tume na maazimio mbalimbali ya Bunge.

Alisema Bunge limekalia ripoti ya Jairo, ripoti ya tume iliyoenda kuchunguza vurugu Mtwara, imezima utekelezaji wa maazimio ya kashfa ya Richmond.

Kutokana na hali hiyo, Mbowe, alisema hawako tayari kuendelea kushiriki kwenye mjadala huo na wametoka ili kuionyesha dunia kwamba kuna tatizo ndani ya Bunge.

Hata hivyo, alisema leo wataendelea na mjadala wa Bunge la Bajeti kwani walitaka kupitisha ujumbe wao kupitia wizara hiyo ya Nishati na Madini.

Juzi usiku, CCM walikuwa na kikao na kukubaliana kuilinda wizara hiyo kwa gharama zozote.

Hata hivyo, wakati wa majumuisho ya hoja za bajeti hiyo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Stephen Masele, alimlaumu balozi wa Uingereza hapa nchini kuendesha vitendo vya kuihujumu, ikiwemo kuzungumza na wadau mbalimbali ili wazuie Tanzania isipate misaada.

Alisema kuwa wana ushahidi mzito kuwa balozi huyo amekuwa akiitaka serikali ilipe deni la benki ya Standard Charter inayoidai kampuni ya kufua umeme wa dharura ya IPTL, lakini Tanzania imepinga malipo hayo.

Alibainisha kuwa serikali inamtaka balozi huyo afike Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kujibu tuhuma hizo na ajipime kama anafaa kuendelea kutumikia nafasi hiyo hapa nchini.
CREDIT:MTANZANIA DAIMA

No comments: