ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 26, 2014

Pingamizi Simba ngoma ngumu

Damas Ndumbaro

Wakati Kamati ya Uchaguzi ya Simba ikitarajia kufanya usaili wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kesho, mambo yameonekana magumu baada ya zoezi la kusikiliza pingamizi kutokamilika kwa wakati jana.

Kamati ya uchaguzi huo inayoongozwa na mtaalam wa sheria, Damas Ndumbaro jana iliendesha zoezi la kusikiliza pingamizi za baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali wakiwamo Evans Aveva na Michael Wambura wanaoutaka urais wa klabu hiyo.

Walipotafutwa na NIPASHE kwa simu jana jioni kuzungumzia zoezi hilo, Ndumbaro na Khalid Kamguna, Katibu Msaidizi wa Kamati ya Uchaguzi, walikataa kuzungumza chochote kwa madai kuwa bado walikuwa kwenye kikao cha kusikiliza pingamizi.

"Mpaka sasa (jana saa 11:57 jioni) bado tunasikiliza pingamizi. Hatuwezi kuzungumza lolote kwa sasa hadi pale tutakapokamilisha kikao hiki," alisema Kamguna kisha akakata simu.

Hata hivyo, mmoja wa wagombea waliokuwa wametinga kwenye maeneo ya Gymkhana jijini Dar es Salaam jana kujibu pingamizi (jina tunalihifadhi), alisema zoezi hilo halikukamilika kwa wakati kutokana na baadhi ya pingamizi kuchukua muda mrefu wa kusikilizwa.

Waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuwapo kwenye eneo lililokuwa limetengwa kwa ajili ya kikao hicho jana.

"Sidhani kama leo (jana) wataweza kusikiliza pingamizi zote maana kuna wagombea wanachukua muda mrefu wanapoingia kujibu pingamizi zao.

Mgombea kama Swedi Nkwabi (anayewania umakamu wa rais) ana pingamizi nane na kila pingamizi inachukua zaidi ya robo saa," alisema.

Lakini, wagombea wote wenye makosa ya kimaadili watafikishwa mbele ya kamati mpya ya maadili ya klabu hiyo.

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Juni 29 mwaka huu, kesho kamati ya uchaguzi itawafanyia usaili wagombea ambao watapita kwenye zoezi la pingamizi na matokeo ya usaili yatatangazwa Alhamisi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: