Friday, May 30, 2014

Prof Tibaijuka asalimu amri Kigamboni

Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka juzi aliwekwa kitimoto na wabunge waliotishia kuondoa shilingi kukwamisha bajeti ya wizara yake kiasi cha kumlazimisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuingilia kati na kuokoa jahazi.
Pinda aliokoa jahazi baada ya mbunge wa Kigamboni, Dk faustine Ndungulile kukataa kurudisha shilingi akieleza kuwa Serikali haijashirikisha wadau katika mradi huo utakaogharimu Sh11.7 trilioni utakapokamilika.
“Nimeona kuna tatizo la elimu kwa umma kuhusu mradi huu na ushirikishwaji,” alisema Pinda baada ya mbunge wa viti maalum (CCM), Esther Bulaya kumuomba aingilie kati ili kuondoa aibu kwa Serikali.
“Serikali tunaomba tuachiwe suala hili. Wizara itaanza kutoa elimu kuhusu mradi huu.”
Awali Tibaijuka, ambaye alikuwa na kazi ya kujibu tuhuma za ufisadi wa kutumia madaraka vibaya katika mgogoro wa Chasimba na kiwanda cha saruji cha Wazo Hill jijini Dar es salaa, alijitahidi kupangua hoja za kambi ya upinzani na wakati mwingine kumshambulia mbunge wa Kawe, Halima Mdee aliyeshikia bango mgogoro wa wananchi wa Chasimba na kiwanda cha saruji cha Wazo Hill.
Tibaijuka, ambaye alikuwa mkurugenzi wa Shirika la Makazi ya Umoja wa Mataifa (UN-Habitat), baadaye alisema anakubaliana na mawazo ya wengi kuhusu hali na mazingira ya mji wa Kigamboni uliopo jijini Dar es Salaam hivyo kwa kuwa kuna kasoro na kwamba suala la ushirikishwaji linawezekana.
Sakata hilo, ambalo lilionekana kumnyima raha Waziri Tibaijuka kadri mjadala ulivyokuwa unaendelea, lilitokea wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha vifungu vya bajeti hiyo ya Sh88.9 bilioni.
Mbunge wa Kigamboni, Dk Ndungulile aliondoa shilingi katika mshahara wa waziri akipinga namna Serikali inavyoutekeleza mradi wa uendelezaji wa wa mji wa Kigamboni bila ya kuwashirikisha wakazi wa Kigamboni.
Dk Ndungulile alisema kuwa wananchi hawashirikishwi katika mradi huo wala hawaelewi hatima ya malipo ya fidia ya nyumba zao.
Badala yake, mbunge huyo alisema, wananchi wanalazimishwa kununua hisa kwa ajili ya umiliki wa mradi huo, kitu ambacho alikipinga.
“Suala la kuwa na hisa si la lazima ni hiari, kwanza waziri anazidi kuwachanganya wananchi wa Kigamboni ambao hawajaelimishwa kuhusu suala hilo, hivyo naondoa shilingi katika bajeti yako,” alisema Dk Ndungulile.
Mbunge huyo aliungwa mkono na wabunge wengine akiwamo mbunge wa viti maalum (CCM), Esther Bulaya, mbunge wa Temeke, Zuberi Mtemvu na mbunge wa viti maalumu (CCM), Zarina Madabida.
Mtemvu alisema mradi huo utasababisha balaa na akamshauri Waziri “aupeleke katika Jimbo lake la uchaguzi la Muleba Kusini”.
“Hatuwezi kuwa na mradi unaoendeshwa kimya kimya huku wananchi wakiwa hawaelezwi kinachoendelea,” alisema Mtemvu.
Kwa upande wake, Bulaya alisema Serikali haiwatendei haki wakazi wa Kigamboni kwani tangu mwaka 2008, hawatakiwi kujenga, kukarabati wala kuuza nyumba zao.
“Waziri Mkuu ingilia kati mgogoro wa Kigamboni. Mgogoro huu unaitia aibu Serikali yako. Wananchi hawashirikishwi… waziri anafanya kazi bila kuwashirikisha wananchi,” alisema Bulaya.
Naye, Madabida alisema kama serikali imeshindwa kuutekeleza mradi huo, ni bora iuache na ifanye mambo mengine ili kuwapa uhuru wakazi wa Kigamboni.
Akijibu hoja hizo, Profesa Tibaijuka alisema kuanzia sasa atakuwa karibu na Ndungulile na wakazi wa Kigamboni ili waweze kufahamu kila kitu kinachoendelea.
Hata hivyo, Dk Ndungulile aliendelea na msimamo wake wa kuondoa shilingi katika fungu la mshahara wa waziri katika bajeti hiyo akisema maneno ya waziri huyo yamekuwa yakitolewa kila mwaka katika bajeti yake.
Baadaye Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema tatizo lililopo ni ukosefu wa elimu na ushirikishwaji wa wananchi katika mradi unaowahusu na kuomba serikali iachiwe ili ishughulikie suala hilo kwa kushirikisha wananchi.
Baada ya Pinda kutoa kauli hiyo, Dk Ndungulile alipokubali kuachia shilingi na baadaye bajeti hiyo kupitishwa.
MWANANCHI

No comments: