ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 30, 2014

Takukuru sasa yatinga Simba

Michael Wambura aliyeenguliwa kugombea urais wa katika Uchaguzi Mkuu wa Simba, akisalimiana na mashabiki wake waliojitokeza kupinga kuenguliwa kwake. Picha na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Usaili wa wagombea uongozi wa Simba, ulichukua sura mpya baada ya jana maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuchukua vyeti vyote vya wagombea na barua tatu za Michael Wambura  alizokuwa ameziwasilisha katika Kamati ya Uchaguzi wa klabu hiyo kama vielelezo.
Maofisa hao walitinga kwenye ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay wakati usaili kwa wagombea ukiendelea na kuchukua vyeti na barua hizo kwa ajili ya kuzichunguza.
Habari za uhakika ambazo gazeti hili ilizipata zinasema kuwa hatua ya Takukuru kuingilia kati ni baada ya  mmoja wa wagombea kuwasilisha taarifa katika taasisi hiyo kudai baadhi ya wanachama wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi kudaiwa kuwasilisha vyeti ‘feki’ na madai mengine mbalimbali.
 Barua za Wambura ambazo waliondoka nazo ni ile aliyowasilisha kwa  kamati ya uchaguzi ya wekundu hao wa Msimbazi akikiri kuipeleka Simba mahakamani na kuiomba kamati hiyo kumaliza suala lake na kuahidi hatarudia tena kufanya kosa kama hilo. Kosa hilo ni kupingana na Katiba ya Simba, TFF na Fifa.
Barua nyingine za Wambura  ni zile alizoziwasilisha kwa Kamati ya Uchaguzi zikiwa mbili tofauti kutoka  ya kwanza ikiwa ya Novemba 6 mwaka 2012 mgombea huyo akitaka kujua uhalali wa uanachama wake na nyingine ya Septemba 15 ikijibu kuwa Simba haina tatizo lolote na yeye. 
Hata hivyo, maofisa hao wa Takukuru baada ya kuondoka saa 6:45 mchana, kamati hiyo ya uchaguzi ilikaa zaidi ya dakika 20 ikijadiliana kabla ya kuendelea na usajili wa  wagombea hao.
Chanzo hicho kimedai kuwa kamati hiyo ya uchaguzi chini ya Damas Ndumbaro huenda ikajiuzulu kutokana na mashinikizo mbalimbali ambayo wamekuwa wakiyapata kutoka kwa baadhi ya watu ikiwamo serikali ikiwa ni pamoja na ujumbe mfupi wa vitisho ambavyo baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wamekuwa wakitumiwa na baadhi ya wanachama.
“Kamati inaweza kujiuzulu endapo italazimishwa kufanya uamuzi kinyume na kanuni na Katiba ya Simba.” Pia, kila mjumbe aliyekuwa anatoka katika usaili huo alieleza kwamba wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa viongozi wa serikali watakapohitajika kufanya hivyo.
Wakati huohuo, aliyekuwa mgombea wa urais Simba, Michael Wambura amekata rufaa kupinga kuenguliwa kwenye mchakato huo wa uchaguzi.
“Nina imani na Kamati ya Rufaa Uchaguzi ya TFF, ni watu makini, uamuzi wowote watakaotoa nitakubaliana nao na naamini haki itatendeka.”alisema Wambura.
Uchaguzi wa klabu hiyo umepangwa kufanyika Juni 29, mwaka huu.
MWANANCHI

No comments: