Waombolezaji wakijiandaa kushusha kaburini jeneza la aliyekuwa Meneja Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Julius Gashaza aliyezikwa kijijini kwao Mulukulazo, Ngara mkoani Kagera jana. Picha na Shaaban Ndyamukama
Ngara. Simanzi, majonzi na kila aina ya huzuni vilitawala makaburini pamoja na minong’ono ya hapa na pale kuhusu mazingira ya kifo cha aliyekuwa meneja wa biashara ya petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Julius Gashaza.
Gashaza aliyefariki Mei 18 mwaka huu katika mazingira ya kutatanisha jijini Dar es Salaam muda mfupi akitokea Dodoma kikazi, alizikwa jana nyumbani kwao katika Kijiji cha Mulukulazo.
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costa Kanyasu ni miongoni mwa mamia ya waombolezaji, wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki, viongozi wa dini na vyama vya siasa waliojitokeza kumzika Gashaza.
Akiongoza ibada ya mazishi hayo, Mchungaji Philipo Mvunyi wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kagera, alisema wanafamilia, ndugu na jamaa wachukulie msiba huo kama mapenzi ya Mungu kwa kuwa kila mwanadamu kapangiwa mazingira ya kuondoka duniani.
Alisema kila mmoja katika familia, Serikalini alikokuwa akifanya kazi na hata watumishi wenzake na marafiki watakuwa na maswali mengi kuhusu kifo hicho, lakini wamtumaini Mungu.
Mkurugenzi wa mafuta wa Ewura, Godwin Samwel alisema kutokana na kifo cha mtumishi huyo, ofisi ya Ewura kwa kushirikiana na vyombo vya dola wanashirikiana kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo hicho.
Kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alitangaza kuunda jopo hilo litakaloongozwa na mkuu wa upelelezi wa kanda hiyo, Jaffary Mohamed atakayeshirikiana na wataalamu wa Maabara Kuu ya Polisi, daktari bingwa wa polisi na maofisa wa Serikali.
Alisema uchunguzi unafanyika ili kuondoa utata ulioanza kujitokeza kuhusu kifo hicho.
MWANANCHI

No comments:
Post a Comment