Na Anna Nkinda – Maelezo
Wilaya
ya Kinondoni kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
wanaandaa mkakati wa kusafirisha wanafunzi kwa vitambulisho maalum vya
wanafunzi kwa bei naafuu kwa kutumia mabasi ya UDA kwenda shule za
pembezoni.
Hayo
yamesemwa hivi karibuni na Afisa Elimu Sekondari wilaya ya Kinondoni
Omath Sanga wakati akisoma taarifa ya Idara ya Elimu kwa Mke wa Rais
Mama Salma Kikwete alipoitembelea shule ya Sekondari ya Kata ya Salma
Kikwete iliyopo Kijitonyama wilayani humo.
Sanga
alisema wanafunzi hao ambao wanatumia usafiri wa mabasi zaidi ya moja
kwenda shule kwa siku kutoka majumbani kwao kuelekea maeneo ya Goba,
Fahari, Kinzudi, Mabwe, Kisauke, Njechele, Mabibo, Malambamawili,
Hondogo, Gogoni, Kibwegere na Kibweheri mara baada ya kukamilika kwa
vitambulisho bivyo watalipa nauli ya shilingi 200 kwenda na 200 kurudi.
“Mwanafunzi
atatumia kitambulisho maalum ambacho kitamuwezesha kupanda zaidi ya
basi moja la UDA kutoka nyumbani hadi kufika shuleni kwa gharama ya
shilingi 400 kwa siku hii ni kwenda na kurudi tofauti na ilivyo sasa
wanatumia fedha nyingi katika nauli kwani tatizo la usafiri kwa
wanafunzi limekuwa ni moja ya changamoto inayoikabili wilaya yetu”,
alisema Sanga.
Aidha
alisema changamoto zinazoikabili idara hiyo ni upungufu wa vifaa vya
kujifunzia na kufundishia, walimu wa masomo ya sayansi kwa shule za
sekondari, vyumba vya madarasa, madawati na maabara kwa baadhi ya shule
za msingi na Sekondari na ukosefu wa usafiri kwa wanafunzi wanaosoma
shule za pembezoni.
Alisema
mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo ni wilaya hiyo imekuwa
ikitenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa madawati, ujenzi wa
vyumba vya madarasa pamoja na kukabiliana na uharibifu wa miungombinu.
Vilevile wanashirikiana na wanajamii kwa ajili ya kuchangia ununuzi wa
madawati.
Kwa
upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake
na Maendeleo (WAMA) aliwataka wanafunzi hao kuitumia Sayansi na
Teknolojia kutafuta elimu na siyo tofauti kwani Dunia ya leo inahitaji
mtu mmoja kuwa na utaalam wa namna nyingi ili aweze kufanikiwa na kuwa
kivutio katika soko la ajira na kujiajiri.
Vilevile
kuweza kwenda na wakati kulingana na mabadiliko jambo la muhimu ni
kutokata tamaa mapema na kutojiweka nyuma kwenye elimu yoyote yenye
faida maishani.
Mama
Kikwete alisema lengo kuu la elimu ni kuhakikisha mwanadamu anapata
maendeleo endelevu katika maisha yake ya uzima wa sasa na wa abaadaye,
ili kuweza kulinda na kudumisha utu wake pamoja na kuendelea kuimarisha
hazi zake za msingi kwani maisha ya mtu aliyesoma ni tofauti na maisha
ya mtu asiyesoma.
“Kila
mtu anapaswa kuhakikisha kuwa elimu anayoipata inamsaidia kuchangia
maendeleo ya jamii husika, sanjari na kukua uelewano, uvumilivu na
urafiki kati ya watu wa mataifa mbalimbali na kwa njia yah ii wau
wanaweza kujenga misingi ya haki na amani”, alisema Mama Kikwete.
Akiongea
kwa njia ya simu Mwenyekiti Mtendaji wa UDA Robert Kisena alisema
vitambulisho hivyo ni maalum kwa ajili ya wanafunzi kutoka wilaya zote
za Mkoa wa Dar es salaam ambazo ni Ilala, Temeke na Kinondoni wanasoma
shule za Sekondari zilizopo pembezoni mwa mji.
“Wanafunzi
watakaotumia vitambulisho hivi ni wale wanaotoka umbali wa km 30 hadi
km 60 kutoka nyumbani hadi shuleni ingawa katika makubaliano ya awali
ilikuwa ni walipe nauli ya shilingi 200 na kwa wanafunzi wasio na uwezo
wasilipe nauli lakini kampuni yangu itaangalia kama ikiwezekana
wasilipe nauli kabisa.
Tatizo
la usafiri kwa wanafunzi wanaotoka Buguruni hadi Ubungo ni tofauti na
kwa mwanafunzi anayetoka Buguruni hadi Chanika hawa wa chanika wanatumia
mabasi zaidi ya moja na kulipa nauli kubwa, lakini mwanafunzi akiwa na
kitambulisho hiki ataweza kupanda mabasi ya UDA hata matatu kwa gharama
ya shilingi 200 tu”, alisema Kisena.
Kisena
alisema wanafunzi hawa watatumia vitambulisho hivyo wakiwa wamevaa nguo
za shule hata kama ni mwishoni mwa wiki na tayari picha za wanafunzi
13,000 kutoka wilaya zote tatu zimeshapokelewa katika ofisi za UDA kwa
ajili ya utengenezaji wa vitambulisho.
Alisema
gharama za utengenezaji wa vitambulisho ni za aina 2 kuna vya
shilingi 1000 na 4500 wanachosubiri ni jibu kutoka Serikali ya mkoa ili
iweze kuchagua aina gani ya vitambulisho vitengenezwe kwani gharama ya
utengenezaji wa vitambulisho siyo za UDA.
Wilaya
ya Kinondoni ina jumla ya shule za Msingi 236 kati ya hizo 140 ni za
Serikali ambazo zinawanafunzi 152,426 na shule binafsi 96 zenye
wanafunzi 29,101. Shule za Sekondari ni 137 kati ya hizo 46 ni za
Serikali na 91 ni za binafsi. Idadi ya wanafunzi katika shule zote za
Serikali ni 44,621 kati ya hao wavulana ni 23,466 na wasichana ni
21,155.

No comments:
Post a Comment