Mwenyekiti wa CHADEMA Mbeya Mjini John Mwambigija akielezea azma yao ya kutangaza mkutano wa UKAWA unaotarajia kufanyika Mei 22 |
Katibu Mwenezi wa CHADEMA Mbeya Mjini Baraka Mwakyabula akitoa msimamo wa UKAWA kuhusu kuwa na gari la (PA) juu ya mkutano wa UKAWA jijini Mbeya Mei 22 |
Baadhi ya waandishi wa Habari waliokuwepo kwenye kikao hicho |
Katibu wa Chama Cha Wananchi CUF Zacharia Mwidunda akizungumzia mkutano wa UKAWA utakaofanyika Mei 22, utakaohutubiwa na Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahimu Lipumba |
Umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA)
Mbeya imekumbana na kikwazo kutoka Halmashauri ya Jiji la Mbeya baada ya
kudai kuwa wamezuiwa kutangaza ujio wa mkutano wa hadhara
utakaohutubiwa na viongozi wa Kitaifa Jijini Mbeya MEI 22.
UKAWA wamedai kukumbana na vikwazo
hivyo katika ofisi ya Ofisa Utamaduni wa Jiji ambaye alikataa kupokea
hela kwa ajili ya kupita na matangazo barabarani maarufu kama PA kwa nia
ya kuwajulisha wananchi mkutano wa UKAWA.
Akizungumza katika kikao na waandishi
wa Habari kwenye Hotel ya Mbeya Peak leo mchana Mwenyekiti wa CHADEMA
Mbeya mjini John Mwambigija alisema kuwa pamoja na kupata vikwazo hivyo
wao watazunguka na gari la matangazo kote mjini huku wakisindikizwa na
Blue Guard wao ambao watalinda vurugu zozote zitakazosababisha wao
wasifanye matangazo hayo.
''Tumefuata taratibu kihalali
tumeenda Ofisi za Ofisa Utamaduni kulipia matangazo kama yanavyofanyika
matangazo mengine Jijini, Ofisa Utamaduni amekataa hela yetu na
kutunyima kuwajulisha wananchi juu ya Mkutano wetu, sisi tutafanya
mkutano kama tulivyopanga, tutasindikizwa na Blue Guard wetu katika gari
nyuma,''alisema Mwambigija.
Katika taarifa yake juu ya mkutano
huo Mwambigija alisema kuwa viongozi wa Kitaifa wa UKAWA wakiongozwa na
Profesa Ibrahimu Lipumba watafanya mkutano katika Viwanja vya Ruanda
Nzovwe ambapo pia atakuwepo Said Mohamed(Makamu Mwenyekiti CHADEMA
(Zanzibar) Danda Juju wa NCCR Mageuzi na Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph
Mbilinyi(SUGU).
Aidha alisema kuwa ili kuepuka
mamluki wanaopandikizwa katika mikutano hiyo na kuweka mabango, wao
UKAWA hawatakuwa na bango hata moja hivyo mamluki yoyote atakayejitokeza
na bango atashughulikiwa ipasavyo.
''Tumepata taarifa mamluki wa (chama
kimoja cha siasa) wamejipanga kuwa na mabango sisi hatutakuwa na
mabango, tunawaonya watakaokuja na mabango wasimlamu mtu kwa yale
yatakayowapata" alionya Mwambigija.
Mkutano huo na waandishi wa habari
uliwahusisha pia viongozi wa CUF, na NCCR Mageuzi ambao walisisitiza
kuwa mkutano huo umelenga kuwazindua wananchi waidai Tanganyika yao
ambayo imepotezwa kwa maslahi ya wachache.
''Mkutano wetu una nia ya kuwazindua
wananchi waidai Tanganyika yetu na kuhitaji serikali tatu,nia yetu ni
kufanya mkutano wa amani na utulivu pamoja na kunyimwa kibali cha
Maandamano na Jeshi la polisi,''alisema Zacharia Mwidunda Katibu wa CUF
Mbeya mjini.
Kwa upande wake Katibu wa NCCR
Mageuzi Mbeya mjini George Mbogela alisema kuwa wameamua kuunganisha
nguvu kujenga umoja na mshikamano ili kudai uhuru wa maoni ya wananchi
yaliyotolewa juu ya uhitaji wa serikali tatu usihodhiwe na chama tawala.
''Tumeamua kwa pamoja kutetea
Utanganyika wetu, tumedhamiria kuwakumbusha wananchi juu ya mtazamo wa
UKAWA kuhitaji kuwepo kwa serikali tatu,''alisema Mbogela.
No comments:
Post a Comment