Vyama hivyo vimesema kwamba vitashiriki katika uchaguzi huo kupambana na chama tawala.
Viongozi wa Ukawa walisema kususia uchaguzi mkuu ambao utamchagua rais, wabunge na madiwani na kuiachia CCM pekee yake itakuwa ni sawa na kumuachia fisi bucha ambaye ataweza kula nyama yote.
Ukawa unaundwa na vyama vya CUF, NCCR- Mageuzi na Chadema ambavyo viliamua kususia Bunge la Katiba kupinga uendeshaji wa Bunge hilo hususani kupuuzwa kwa mapendekezo ya Tume ya Warioba kuhusu muundo wa Muungano.
Vyama hivyo pia kwa kufanya mikutano nchi nzima kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema hayo juzi katika mkutano wa hadhara jijini Arusha baada ya kuulizwa na wananchi waliotaka kujua kama vyama hivyo vitasusia uchaguzi mkuu wa 2015 kama CCM wataichakachua rasimu ya katiba mpya na kuipitisha kimabavu.
“Kwa Tanzania kususia uchaguzi ni sawa na kumuachia fisi bucha, hata kama watatumia mabavu kuipitisha rasimu kwa kuondoa maoni ya wananchi tutapambana nao kwenye uchaguzi kwani sisi tunategemea nguvu ya umma,” alisema.
Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, alisema Sh. bilioni 27 zilizotumika katika Bunge Maalum la Katiba hazina tofauti na ufisadi kwa sababu hazikuidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama taratibu na sheria zinavyoelekeza.
Alisema serikali ya CCM imekuwa inavunja taratibu za kutumia fedha za umma.
“Kiutaratibu kodi zote zinazokusanywa zinaingizwa katika mfuko mkuu wa taifa, hakuna pesa inayoweza kutumika bila kuidhinishwa na Bunge, lakini fedha zilizotumika wakati wa Bunge la Katiba hazikuidhinishwa na Bunge, sijui walizitoa wapi,” alisema.
Ndesamburo ambaye aliwasili katika uwanja huo saa 10:13 jioni kwa helkopta na kusababisha mkutano kusimama kwa muda na kukatiza hotuba ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi, Hemed Msabaha, alisema kiutaratibu fedha yeyote ya serikali haiwezi ikatumika bila kuidhinishwa na Bunge, lakini hali hiyo ilikuwa tofauti katika Bunge la Katiba.
Alisema wabunge wa Ukawa waliamua kutoka ndani ya Bunge Maalum la Katiba baada ya kubaini kuwa wabunge wa CCM waligeuza bunge hilo kama Kamati ya CCM kwa kubadilisha baadhi ya vipengele kinyemela vilivyopo katika rasimu ya katiba mpya.
Msabaha alisema ni lazima CCM wakubali mabadiliko kwa kukubaliana na mapendekezo ya Jaji Warioba kuhusu muundo wa serikali tatu.
Ndesamburo alisema katika kuonyesha jinsi serikali ya CCM isivyokuwa na nia nzuri na katiba, hata suala la uteuzi wa wajumbe 201 walioteuliwa na Rais, kati ya hao 160 ni makada wa chama hicho.
JESHI KUPINDUA NCHI
Wakati huo huo, Ukawa wamesema nchi ikipinduliwa na Jeshi hakutawaathiri wananchi kwa sababu inawezekana kukawa na unafuu wa maisha kwa Watanzania.
Kauli hiyo ilitolewa umoja huo jana jijini Arusha katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Kilombero.
Msabaha alisema CCM wamekuwa wakitisha wananchi kwamba kama muundo wa serikali tatu utapitishwa kuna uwezekano Jeshi likaasi na kuchukua nchi.
“Jeshi likichukua nchi wananchi wataahirika nini, tena nawaambia hali inaweza ikawa nzuri kuliko hivi sasa ambapo CCM imetawala nchi kwa zaidi ya miaka 50, lakini hali za maisha ya Watanzania zimezidi kuwa mbaya,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo hakuna sababu kwa serikali na wana CCM kuendeleza propaganda hizo za kuwatisha wananchi ili wajenge chuki dhidi ya Jeshi lao wakati wanaliamini kutokana na umuhimu katika kulinda uslama wa nchi.
Msabaha alisema hofu ya jeshi kuchukua nchi haina maana kwani inawezekana jeshi likatawala vizuri.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Mustapha Wandwi, alisema kauli za viongozi wa CCM kwamba muundo wa serikali tatu ukipitishwa Jeshi litachukua nchi ni uchochezi ambao unaweza kuhatarisha usalama wa nchi.
Wandwi alisema Watanzania waunge mkono Ukawa ili kutetea ipatikane katiba bora itakayoleta maendeleo kwa wananchi wote badala ya hivi sasa kutokana na katiba iliyopo kulinda maslahi ya watu wachache.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment