
Na Mwandishi wetu
Walio wengi tumesikia
na kusikitiswa na habari za utekwaji wa
wasichana wanafunzi nchi Nigeria. Wengi tunakubaliana kwamba ni jambo baya, la
kusikitisha na inabidi likemewe kwa
nguvu zote. Tukiendelea kufuatiliana kwa karibu suala hilo kupitia vyombo vya habari mbali mbali, tunaona juhudi
zinazofanywa ili kuwanusuru wasichana hao kutoka mikononi mwa waliowashikilia
yaani kikundi cha Boko Haram.
Juhudi nyingi
zinafanywa na mataifa yaliyopo nje ya Afrika tumesikia Rais wa Marekani Baraka
Obama akituma kikosi cha wataalamu wa Kijeshi
na wataalamu wa utafiti katika mambo ya utekaji. Tumesikia China nao
wametuma wataalamu wao kwenda Nigeria, tumesikia waziri mkuu wa Uingereza David
Cameroon akitoa msimamo wake kuhusu kukamatwa waliowateka na kutokomeza kabisa
kikundi cha Boko Haram
Zaidi tumeshuhudia maadamano makubwa katika miji mbali mbali nchini
Marekani, Uingerereza na Nageria watu wakitoa hisia zao kuhusu kurudishwa kwa
hao wasichana. Kweli dunia yote imeamuka kuhusu suala hili. Jambo ambalo ni
zuri kuona dunia inalipa kipaombele na kuliongelea kwa namna ya pekee hasa
kwenye hizo nchi za dunia ya kwanza.
Tumeshuhudia mke wa
Rais wa Marekani Michelle Obama amebeba bango lililoandikwa “Bring Back Our
Girls” na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mama Hillary Clinton
ameungana na dunia nzima kupaza sauti akiomba wasichana warudishwe.
Bahati mbaya sisi ambao
tunakaa na hawa (wazungu) ambao kama nilivyowaeleza jinsi walivyoonesha kuguswa
na jambo hili, hapa wanatuuliza uko wapi
msimamo wa waafrika katika jambo hili. Ni swali ambalo najaribu kulipoza kidogo
kwani nikiliuliza kama walio wengi wanavyoliuliza wengine mtatamani kurusha
ngumi. Swali hili lina ukweli kwa asilimia kubwa tu kadiri ya muono wangu.
Kwanza kabisa tuanze na
Nigeria yenyewe, juzi tumeshuhudia Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan akiomba
msaada kutoka Marekani, Uingereza na nchi nyingine za Magharibu hakutaja nchi
yeyote ya Afrika. Kipi kinachoendelea kichwani mwake, ni kwamba msaada daima
utoka Magharibu na kwa suala hili ni lazima nchi za magharibi zipewe namba
moja.Hii hali imeendelea kuitesa Afrika miaka nenda rudi. Kabla ya Rais wa
Nigeria kuomba msaada kutoka Magharibi Rais wa Tanzania ndugu Jakaya Mrisho
Kikwete alikuwa naye Ikulu ya Nigeria, na baadhi ya Marais wa Afrika wapo
Nigeria kwa Mkutano Mkuu wa Kiuchumi. Lakini ni nchi za Magharibi zinazopewa
kipaumbele.
Pili ni asili ya tatizo lenyewe, watekaji ambao ni
kikundi cha Boko Haramu chini ya kiongozi wao Abubakar Shekahu wamekuwa
wakipinga kila kitu chenye viashilia vya Kimagharibu hasa vile vinavyoshikamana
na utamaduni wa magharibu. Katika hali hiyo Boko Haram wanasema na elimu ina
viashiria vya Magharibi. Na sasa tunawaleta watu wa Magharibi ndio waje kuwaambia
kwamba lazima mfuate mambo yetu kwa nguvu. Na Rais wa Nigeria kasema wazi
kwamba huu ndio utakuwa mwisho wa Boko Haram. Yahani mwisho wao ni mpaka wateke
Wasichana? Kuna watu wengi wameuwawa Nigeria na hakuna mtu aliyeangazia suala
hilo mpaka nchi za magaharibi zilipolishupalia.
Kwa hili waafrika tuna
maswali mengi ya kujiuliza na kubwa zaidi ni
kwamba ‘tutaendelea kutegemea usaidizi wa Magharibi mpaka lini?’ je sisi
wenyewe tunaaaminiana? Tutajenga uwezo lini wa kutatua matatizo yetu wenyewe.
Haya mambo si mageni sana ndugu zangu, watu wanaoishi katika nchi za magharibu
wanayajua haya, mwafrika anaweza kuona ugumu wa kukueleza kitu wewe mwaafika
mwenzake na akaona ni rahisi kumweleza mzungu, wakati mzungu hawezi hata siku
moja kufanya hivyo. Tatizo ndugu zangu waafrika lipo wapi?
Sisi ni mashuhuda siku
ya Sherehe za Muunganao ncini Tanzania, jeshi letu lilionesha ukuaji na uwezo
mkubwa, sio kwamba uwezo hatunao bali kujiamini na kuondoa dhana ya utegemezi.
Angalau jana vikundi vya kupigania haki za bibadamu nchini Kenya vililifanya
maandamano mpaka ubalozi wa Nigeria nchini Kenya na kutoa hisia zao. Lakini
wapi viongozi wetu wa Afrika jamani? Jambo hili limetokea Nigeria na kesho
laweza kutokea Tanzania, Uganda, Malawi, Zambia, Kenya, Rwanda je tutaendelea
kuomba msaada wa kijeshi waafrika?
No comments:
Post a Comment