ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 11, 2014

3BOYS WAWATESA WAZEE CCM


 
MAPACHA watatu, maarufu kwa jina la 3boys, wameanza kuwatia hofu makada wazee ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), waliojipanga katika mitandao ya kuusaka urais wa 2015 kupitia chama hicho.
Habari za uhakika zilizopatikana kutoka ndani ya
mitandao kadhaa ya kusaka urais wa 2015 ndani ya CCM, zimewataja mapacha watatu hao kwamba ni Dk Emmanuel Nchimbi, William Ngeleja na Mwigulu Nchemba.
Watatu hao wametajwa kuwa chaguo la wapiga kura walio wengi nchini, ndani na nje ya CCM, ambao wanaangukia katika kundi la vijana wa umri kati ya miaka 18 na 50.
Kwa mujibu wa habari hizo, yeyote kati ya mapacha hao watatu atakayeamua kujitosa katika kinyang’anyiro hicho na hatimaye kupitishwa kupeperusha bendera ya CCM, atakihakikishia chama hicho kikongwe nchini na barani Afrika, ushindi wa kishindo hata kabla ya saa nne asubuhi siku ya upigaji kura.
Habari kutoka ndani ya mtandao wa urais wa 3boys hao, zinasema upo mkakati wa chini chini wa kutaka kuunganisha nguvu zao ili kukabiliana na mitandao ya wakongwe wa siasa za ndani ya CCM, ambao wametajwa pia kuutamani urais wa nchi hii.
Miongoni mwa wakongwe wa siasa za ndani ya CCM wanaotajwa kuunda mitandao tayari ya urais, ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani, ambaye pia ni mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa na ambaye pia ni mbunge wa Mtama, Lindi, Bernard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na pia mbunge wa Urambo Mashariki, Samue Sitta. 
Mitandao ya urais ya wakongwe hao, imetajwa kuwa mbali katika maandalizi hayo ya urais, hali inayowalazimu wapinzani wao wenye ndoto kama hizo za urais 2015, kutafuta mbinu za ziada, na moja ya mbinu hizo ni kuunganisha nguvu za vijana ndani ya CCM dhidi ya wazee wa chama hicho. 
Itakumbukwa kwamba mwaka 1995, makada wawili vijana ndani ya CCM, Jakaya Kikwete na Edward Lowassa, waliunganisha nguvu zao na kupewa jina la 2boys, na wote wawili wakajitosa katika kinyang’anyiro cha urais kwa kupanda ndege moja kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kuchukua fomu ya kuomba uteuzi wa chama chao.
Katika kinyang’anyiro hicho cha mwaka 1995 ndani ya CCM, jina la Lowassa lilikuwa miongoni mwa majina ya mwanzo kabisa kutoswa, lakini jina la Kikwete lilikwenda hadi duru ya mwisho ya upigaji kura wa marudio baada ya duru ya kwanza iliyowakutanisha Kikwete, Benjamin Mkapa na Cleopa Msuya kushindwa kupata mshindi. 
Zipo habari kwamba baada ya jina la Lowassa kukatwa mapema, mtandao wake uliamua mara moja kujiunga na mtandao wa Kikwete na kuanza kuratibu kila mipango ya kampeni kuhakikisha mmoja wao anaukwaa urais na hatimaye wakumbukane huko mbele ya safari. 
Hata hivyo, kama alivyosema mwenyewe Kikwete mwaka 2005 mara baada ya kuteuliwa na chama chake kupeperusha bendera, mwaka 1995 kura za 2boys hao hazikutosha, na badala yake Mkapa, ambaye wanamtandao wake ulimpachika jina la ‘Mr Clean’ aliibuka kidedea katika duru la pili.
Kama ilivyokuwa kwa Kikwete na Lowassa mwaka 1995, habari zinasema mitandao ya 3boys 2015, imejipanga kuunganisha nguvu endapo mmoja wao atabahatika kupenya katika tano bora, ambao majina yao yatapelekwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa ajili ya upigaji kura ili kupata majina matatu yatakayopelekwa katika Mkutano Mkuu kwa hatua ya mwisho. 
3boys hawa ni nani? Dk Nchimbi, ambaye ni mbunge wa Songea Mjini, anatajwa kuwa mmoja wa wanasiasa vijana ndani ya CCM mwenye uzoefu mkubwa wa kiuongozi. Kwa miaka zaidi ya 15 sasa, Dk. Nchimbi amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM.
Aidha, Nchimbi amewahi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM kwa kipindi chote cha miaka 10, kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri na baadaye Waziri kamili kiasi cha kuaminiwa kuongoza wizara nyeti za Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na ile ya Mambo ya Ndani. 
Hata hivyo, pamoja na kuongoza wizara zake kwa mafanikio makubwa, Nchimbi alijikuta akilazimika kujiuzulu uwaziri kwa kuwajibika kisiasa baada ya watendaji wa wizara yake waliohusika na Operesheni Tokomeza kudaiwa kutenda vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika operesheni hiyo. 
Baada ya kuwajibika kisiasa hadi sasa, Nchimbi amekuwa mkimya akitimiza majukumu yake ya kibunge na kichama bila kinyongo, hali inayoelezwa na wachambuzi wa mambo kwamba ni ukomavu wa kisiasa na uongozi.
Lakini pia, Nchimbi anatajwa kuwa mmoja wa mihimili mikuu katika mtandao uliomwingiza Rais Kikwete madarakani mwaka 2005, wakati huo akiwa Mwenyekiti wa UVCCM taifa kwa kuwaunganisha vijana wote wa jumuiya yake kuwa na sauti na kauli moja juu ya mgombea wao huyo.
Aidha, Nchimbi ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 43, anaelezwa kuwa mmoja wa viongozi wa UVCCM aliyewashawishi na kuwahimiza vijana wa jumuiya yake kuongeza ujuzi wa elimu zaidi kwa ajili ya kujiandaa kuwa viongozi wa chama chao na Serikali yao. 
Kwa upande wake, Ngeleja ambaye ni mbunge wa Sengerema, anatajwa kuwa mtoto wa Azimio la Arusha kutokana na kuzaliwa kwake mwaka 1967 na hivyo kumwezesha leo kuwa na umri wa miaka 47. Wengi wa marais barani Afrika walioingia Ikulu wakiwa na umri wa kati ya miaka 30 na 50 wamefanya vizuri katika nchi zao ukiwalinganisha na marais walioingia madarakani wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 60. 
Ngeleja ingawa hakushika nafasi za juu za uongozi ndani ya CCM, lakini anatajwa kuwa kiongozi makini na mwenye uchungu na umasikini wa Tanzania na wananchi wake. Alikuwa katika baraza la kwanza la mawaziri wa Rais Kikwete mwaka 2006 akianzia na naibu waziri kabla ya kupanda na kuwa waziri kamili, na hasa katika wizara nyeti yenye changamoto nyingi, ya Nishati na Madini.
Mwanasiasa huyo anatajwa kuwa waziri pekee katika wizara hiyo, ambaye ameacha mipango mikakati ya kumaliza tatizo la uhaba wa umeme nchini, ambayo ndiyo inayotekelezwa kwa sasa na wizara hiyo, na hasa kupitia mashirika yake ya Tanesco inayohusika na usambazaji wa umeme na TPDC ambayo kwa sasa imejikita katika kuhakikisha kwamba Tanzania inafaidika kutokana na uchumi wa gesi na mafuta.
Kama ilivyotokea kwa Dk.  Nchimbi, Ngeleja naye alijikuta akilazimika kujiuzulu uwaziri wa Nishati na Madini. 
Mwigulu Nchimba, ambaye pamoja na Katibu wa NEC (Itikadi na Uenezi), Nape Nnauye wanatajwa kuwa viboko vya wapinzani nchini, ni mwanasiasa ambaye nyota yake ya kisiasa inazidi kuimarika kila siku, ingawa pia anatajwa kuwa na uzoefu kidogo wa uongozi ndani ya CCM. 
Kwa sasa mwanasiasa huyo ndiye Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), lakini pia akiwa Naibu Waziri wa Fedha (Sera). Mara kadhaa ameaminiwa na chama chake kuongoza operesheni za uchaguzi mdogo katika majimbo na kata, na kukihakikishia ushindi mkubwa chama chake.
Alizaliwa Januari 7, 1975, na kwa hiyo mwakani atakuwa na umri wa miaka 40, umri ambao kikatiba unamruhusu kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, kitaaluma ni mchumi, hali inayomwongezea sifa zaidi kutokana na ukweli kwamba uchumi ndiyo siasa inayotawala dunia hii kwa sasa. 
Wakati 3boys hao wakidaiwa kuwa na mikakati hiyo kuelekea 2015, mwanasiasa mwingine anayetajwa kuwa nyuma ya vijana hao, ni mbunge wa Mvomero, Morogoro, Amos Makalla, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji. 
Ingawa Makalla hatajwi katika kundi hilo kama mwanasiasa anayeutaka urais wa 2015, lakini anatajwa katika timu ya 3boys hao, akielezwa kuwa bingwa wa mikakati ya kujenga mahusiano baina ya mgombea wake na vyombo vya habari pamoja na jamii kwa ujumla.
Aidha, umahiri wa Makalla katika kazi hiyo ya kuwa kiungo kati ya wanamtandao na vyombo vya habari, aliweza kuudhihirisha mwaka 2005 baada ya kufanya kazi hiyo kwa weledi  mkubwa katika kuwaunganisha wanamtandao waliomhakikishia ushindi mkubwa Rais Kikwete.
Juhudi za gazeti hili kuwapata 3boys hao, ili pamoja na mambo mengine, waweze kuzungumza juu ya taarifa hizi, hazikuzaa matunda hadi tunakwenda mitamboni. Hata hivyo, watu walio karibu na wanasiasa hao wamelihakikishia TAZAMA Tanzania kwamba vijana hao wanayo nia hiyo ila kinachotafutwa kwa sasa ni mbinu za kuweza kupenyeza mmoja wao hao ndani ya NEC na Mkutano Mkuu kwa ajili ya uteuzi.
Chanzo:Tazama(10/06/2014)

No comments: