ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 11, 2014

PICHA ZA MFANYABIASHARA ALIYEJIUA KWA KUJIPIGA RISASI JIJINI ARUSHA


Mfanyabiashara wa madini, Richard Lucas (29) anadaiwa kujiua kwa kujipiga risasi kichwani baada ya kusababisha ajali mbili tofauti. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema alijipiga risasi juzi saa 12:45 jioni nyumbani kwake eneo la Kimandolu. Alitumia bastola aina ya Luger yenye namba B136986 . Alisema uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kuwa Lucas alitokea Tengeru akiwa na gari aina ya Toyota Rav 4 yenye namba za usajili T 494 CKY alikokuwa amemfuata rafiki yake aliyekuwa amepata ajali ya kugongwa na gari.


Alipofika eneo la Sekei Darajani, alimgonga mwendesha pikipiki na kuendelea na safari. Mbele kidogo, kwa mujibu wa polisi, aligonga daladala lenye namba za usajili T 636 CUR aina ya Nissan iliyokuwa inachukua abiria. 

Baada ya hapo gari ya Lucas ilipinduka na waliokolewa kwa kupitia dirishani na wananchi.
Inadaiwa alitoka eneo la tukio kwa pikipiki ya kukodi kwenda nyumbani kwao Kimandolu huku akimwacha Vick Mchuma kwenye eneo la tukio.

Alisema baada ya muda, Mchuma ambaye waliongozana naye kwenda kumsaidia rafiki yao aliyepata ajali Tengeru, alipata taarifa kuwa Lucas amejipiga risasi na mwili upo Hospitali ya Mount Meru. Polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo. 

Wakati huo huo, polisi imetoa taarifa ya kifo cha mpanda mlima, Denis Joeli aliyeuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali chini ya bega la kulia karibu na moyo alipotofautiana na mtu aliyekuwa akimdai Sh 40,000.

Kamanda Sabas alisema tukio hilo ni la juzi saa 8:30 asubuhi kwenye kitongoji cha Olturei-Moivo wilayani Arumeru. 

Alisema uchunguzi wa awali wa polisi umebaini Denis alichomwa na Solomon Lembris, waliyetofautiana kauli wakati wakidaiana fedha.

Alisema kuwa baada ya tukio hilo, Lembris alitokomea kusikojulikana juhudi za kumtafuta zinaendelea huku mwili ukiwa umehifadhiwa hospitalini.

No comments: