Advertisements

Monday, June 16, 2014

BARUA KWENDA KWA MHE. RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE UMETISHA SANA KWA HILI

Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete – natamani ningeonana na wewe ana kwa ana ili nikupe shikamoo yako nzito kwakuwa shikamoo ya kuandika siku zote huwa naiona ni yenye mapungufu. Heshima yako mkuu. Mimi kijana wako naliendeleza gurudumu la ujenzi wa taifa katika upande huu wa burudani kama kawaida. Upande ambao mheshimiwa umekuwa ukiuangalia kwa jicho la kipekee na lenye nia njema ya kuuletea neema. Upande ambao kwa viongozi wengi waliopita, ulikuwa ukichukuliwa kama wa anasa na wa kupoteza muda tu hivyo kushindwa kuupa heshima na ‘attention’ inayostahili.
Tangu uchukue madaraka, Mheshimiwa ulionesha nia njema na ya dhati ya kuwasaidia vijana walioamua kujiajiri kwa kutumia vipaji vyap walivyopewa na mwenyezi Mungu asiye mchoyo wa fadhila. Wengi walikuwa wamekwama kuendelea na masomo kutokana na sababu mbalimbali lakini kutokana na kuwa na kipawa cha kuimba ama kuigiza waliamua kutumia sauti zao kuwaburudisha watu kwa kutunga nyimbo.


Burudani ambayo kwa wengine wenye umri kama wako na waliopata nafasi kubwa serikalini wamekuwa wakiichukulia poa na kuiona kama aina moja miongoni mwa aina ya nyingi za uhuni zinazowatawala vijana wengi, imegeuka kuwa ajira muhimu kwa vijana wengi ambao maisha yao yamekuwa mfano kwa vijana wengine pia.


Mheshima Rais, tangu mwanzo, umekuwa karibu mno na vijana wanaofanya muziki wa Bongo Flava na kwao wewe ni kipenzi chao. Katika nchi hii ambayo kutokana na shida zetu, tumejikuta tukiona mabaya zaidi na kuwa watu wa kulalamika na yale mazuri tukijifanya hatuyaoni, hiki unachokifanya kwa vijana wetu kinaweza kionekane kwao cha kawaida tu. Mimi nakichukulia kwa mkazo mkubwa.


Nina imani kubwa, tasnia za burudani za majirani zetu zinatamani pia zingekuwa na Rais kama wewe, ambaye anaufahamu umuhimu wa msanii na kwa moyo mmoja amekuwa akiwajali. Naamini mheshimiwa Rais una imani kama niliyonayo mimi kuwa, wasanii wamekuwa wakitimiza wajibu muhimu katika jamii kwa kutuburudisha tuwapo na mawazo, furaha, huzuni na hali mbalimbali, kutuliwaza pale ya mambo ya dunia yanapotuelemea na kutusemea pale tunaposhindwa kuwasilisha nia zetu. Haipendezi kumuona mtu anayeitumikia jamii kwa hali hii, kuishi maisha ya tabu na ya kudharauliwa.


Na ndio maana umekuwa bega kwa bega kujaribu kuwapa ‘mashavu’ vijana wako ili maisha yao yawe mazuri. Ni ngumu kutimiza matakwa yao yote lakini ile hali tu ya kuwaweka karibu, kuwapa connection, imekufanya uonekane kuwa wewe ni rais wa pekee na ambaye umekuwa na mchango mkubwa kwenye kiwanda cha burudani.


Mheshimiwa Rais, nimeandika barua hii kwa lengo kuu la kukupongeza kwa hotuba yako inayotia moyo uliyoitoa Jumamosi iliyopita mjini Dodoma katika tamasha la uzalendo. Ile ni miongoni mwa hotuba zilizonifurahisha mno mheshimiwa. Ilinionesha jinsi ambavyo unafuatilia kwa ukaribu industry ya muziki duniani. Nilifurahi kukusikia mwenyewe jinsi ambavyo kutumia connection zako mwenyewe, umemtambulisha Diamond Platnumz kwa mdau mkubwa na muhimu katika muziki wa Marekani, Kevin Liles.


Kiukweli mimi Kevin nilimfahamu kupitia makala ya Trey Songz iliyorushwa miaka kadhaa kupitia MTV ambapo yeye alikuwa akiongea kama meneja wake. Nilivutiwa na jinsi alivyo na mchango mkubwa kwa Trey na hivyo nikaamua kumsoma zaidi kwenye mitandao. Niligundua kuwa alikuwa kuwa Rais wa Def Jam Recordings (pamoja na vyeo vingine) ambayo ni miongoni mwa label kubwa na zenye mafanikio nchini Marekani. Naamini kuwa maongezi yako na Kevin kuhusu Diamond yatazalisha kitu kikubwa hapo baadaye. Nilipenda pia uliposema kuwa unajivunia kwa hatua aliyofikia.


Ulitisha zaidi mheshimiwa pale ulipodai kuwa ulizungumza pia na meneja wa Ludacris, Chaka Zulu. Na zaidi pale ulipodai kuwa Usher na mtangazaji wa zamani wa kipindi cha 106 & Park cha BET, Terrence J ambaye kwa sasa ni mtangazaji wa E!News, watakuja Tanzania na kwamba ikiwezekana Trey Songz naye ataibuka.


Hawa watu ni muhimu mno katika burudani duniani hivyo wakija Tanzania kuongea na wasanii kuhusu masuala mbalimbali, watapandikiza masuala mengi ya muhimu kwao. Wasanii wa nyumbani watajifunza mengi kutoka kwao.


Mheshimiwa nimependa ulivyojiongeza hapa kwamba ni vyema ukamfundisha mtu kuvua samaki kuliko kumpa samaki ambao akiwala atapata njaa tena na ataendelea kuhitaji. Ungeweza kusema uwape fedha baadhi ya wasanii lakini fedha hizo zisingewasaidia kwa lolote. Kuwaleta akina Usher nchini kwetu itakuwa ni zawadi kubwa na muhimu kwa wasanii sababu watajifunza mbinu nyingi za kuboresha biashara ya muziki nchini ambayo kama ikitambuliwa kama ajira rasmi na serikali, itawanufaisha wengi.


Naamini kuna wengi watabeza, wataponda na wataongea kuchafua hatua hii lakini jambo unalopaswa kukumbuka kuwa hata Yesu Kristu licha ya kuja duniani kuwaokoa wanadamu dhidi ya dhambi, walimkejeli na kumsulubu bila huruma. Ungekuwa Rais usiyejali kama marais wengine madikteta duniani basi ungetumia uwezo wako kuwaleta wasanii hao waje wakuburudishe kwenye sherehe zako binafsi. Lakini unawaleta hawa kwa madhumuni na nia halisi ya kuwasaidia wasanii wa nyumbani. Hilo si la kupuuzwa.


Na pia wale ambao wataponda hatua hii, ndio walewale ambao bado wanauchukulia muziki kama anasa, uhuni, starehe na masuala ya kupoteza muda wakati kwa nchi zilizoendelea, muziki na filamu vinachangia pato kubwa katika serikali.


Nausubiria sana ujio wa watu hawa muhimu na bila shaka wasaidizi wako watakuwa werevu wa kutosha kutualika pia sisi waandishi kujifunza yanayotuhusu katika ziara hiyo. Wasiwasi wangu ni kuwa Rais atakayechukua nafasi yako atafuata nyayo zako? Anyway, nisikuchoshe kwa maneno mengi mheshimiwa, nakutakia majukumu mema.


Wako katika ujenzi wa taifa, Sky.

1 comment:

Anonymous said...





Are you serious? Really? This is what a president of a country does? Please!