ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 25, 2014

CUF wabadili Katiba ili kuungana na Ukawa

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF), kimefanya mabadiliko ya Katiba yake ikiwa ni maandalizi ya kushirikiana na vyama vingine vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika uchaguzi ujao.
Katika mabadiliko hayo, chama hicho kinakusudia kuingiza jimbo katika mfumo wake wa utawala ili uweze kufanana na wa vyama vingine vya upinzani, hasa Chadema na NCCR-Mageuzi.
Hoja ya mabadiliko hayo iliwasilishwa jana katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho unaoendelea Dar es Salaam ili ijadiliwe na kupitishwa.
Akizungumza na wanahabari jana, Naibu Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Abdul Kambaya alisema hivi sasa Katiba ya chama hicho inatambua kuwapo kata na wilaya lakini haitambui jimbo na kwamba mabadiliko hayo ni maandalizi ya chama hicho katika kushirikiana na Ukawa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu unaofuata.
“Haya ni maandalizi tu ya chama lakini ushirikiano huo utakuja baada ya kuruhusiwa na vikao vyenye mamlaka ya kuruhusu jambo hilo lifanyike,” alisema.
Uchaguzi wa chama
Wakati leo ni siku ya uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa CUF, kampeni za chinichini zimetawala mkutano huo huku maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wakionekana katika eneo la Hoteli ya Blue Pearl unakofanyika.
Wanaowania nafasi za juu katika uchaguzi huo ni Profesa Ibrahim Lipumba anayepambana na Bakari Mbezi na Lutayosa Yemba katika nafasi ya uenyekiti, Juma Hadi Duni na Haji Komba wanaowania umakamu mwenyekiti na Maalim Seif Shariff Hamad anayewania ukatibu mkuu peke yake.
Wajumbe wa mkutano huo huku wengi wao wakiwa wanawake walionekana wakipita huku na kule wakiwaombea kura wagombea wanaowaunga mkono.
Katika uchaguzi wa mwisho miaka mitano iliyopita, Profesa Lipumba aliibuka kidedea kwa kura 600 akiwashinda Profesa Abdallah Safari aliyepata kura sita na Stephen Masanja, kura 10. Wakati huo, Maalim Seif ambaye aliwania nafasi hiyo peke yake, alipata kura 657 sawa na asilimia 99.5.
CUF kuanzisha redio
Katika taarifa yake ya utendaji wa chama hicho katika kipindi cha miaka mitano, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alisema chama hicho kinajivunia mafanikio mengi ikiwamo kuendelea kumiliki kampuni ya kuchapisha magazeti ya Fahamu na Gazeti la Fahamu.
“Baada ya kuliendesha gazeti hilo kwa mafanikio makubwa, kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015 tutaanzisha vituo vya redio vya CUF,” alisema.
Vitisho
Maalim Seif alisema viongozi na wanachama wa chama hicho wamekuwa wakitishwa na kubambikiwa kesi na vyombo vya dola, hali ambayo imekuwa ikiwakatisha tamaa watendaji wa ngazi mbalimbali.
Alisema kuna viongozi na wanachama wake ambao walibambikiziwa kesi na wengine kufungwa kwa sababu za kisiasa.
“Tunasikitishwa na hali hiyo na tunajiuliza kwani nini tunawekewa vikwazo vya aina hii... Wanachama wetu wamekosa nini? Kwetu hii ni changamoto kubwa,” alisema Maalim Seif.
MWANANCHI

No comments: