ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 26, 2014

JWTZ KUANIKA TENA ZANA ZAKE ZA KIVITA JIJINI DAR KATIKA KONGAMANO KUBWA LA KIJESHI



JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linatarajiwa kufanya maonesho ya zana zake za kivita zinazotumiwa na askari wa nchi kavu kuanzia Julai 14 hadi 16, mwaka huu wakati wa kongamano kubwa la kijeshi ambapo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa jeshi hilo nchini.
 
Kampuni zaidi ya 30 zinazotengeneza silaha na vifaa vya kijeshi kutoka ndani na nje ya nchi zitaonyesha bidhaa zao katika Kongamano hilo.
 
Akizungumzia kongamano hilo litakalofanyika kwenye Ukumbi wa wa Milimani City, Dar es Salaam, Julai 14 hadi 16, mwaka huu, mkuu wa kamandi ya Jeshi la Nchikavu, Meja Jenerali Salim Kijuu alisema jana kuwa viongozi mbalimbali wakiwemo wadau wa jeshi watashiriki.
 
“Kampuni 32 za kimataifa zinazozalisha na kuuza silaha na vifaa vya kijeshi zimethibitisha kushiriki katika maonyesho hayo. Viwanda vyetu vya kijeshi na vile vya kiraia vinavyozalisha silaha za kijeshi pia vitashiriki,” alisema Kijuu.
 
Alibainisha kuwa Tanzania itatumia fursa hiyo kulitangaza jeshi lake katika jumuiya za kimataifa, hasa katika kipindi ambacho linaelekea kwenye maadhimisho ya miaka 50 tangu lilipoanzishwa.
 
Alisema majeshi yatakutana kujadili jinsi ya kukabiliana na changamoto za sasa za ulinzi na usalama hasa eneo la Afrika Mashariki ambalo linakabiliwa na changamoto ya uvuvi haramu, uharamia na jinsi ya kulinda maliasili za Taifa.
 
Brigedia Jenerali Simon Mumwi alisema ingawa maonyesho hayo yanahusu silaha na zana za kijeshi, hayana lengo la kuzitisha nchi jirani, bali kuimarisha uhusiano.
 
“Tunawaalika wenzetu ili waje tupeane ujuzi na uzoefu wa changamoto za kiusalama na siyo kuwaonyesha kwamba na sisi tupo,” alisema Mumwi.
 
Kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya JWTZ Agosti, mwaka huu, kutafayika mazoezi makubwa ya kijeshi Arusha.

1 comment:

Anonymous said...

Nadhani wakati umefika kwa nchi yetu kuachana na dhana hii ya kikomunisti ambayo pengine ili work wakati wa cold war lakini kwa karne hii zoezi hili halina tija kwa mwananchi wa kawaida.Dunia imebadilika na teknologia imekuwa kiasi kwamba kama mwananchi anapenda kujua ni aina gani na kwa wingi upi wa vifaa vya kijeshi TPDF inavyo aningia mtandaoni na kupata kila kitu.
Gharama zinazo tumika ku-organize sherehe hizi ni kubwa na zingeweza kutumika katika kutatua matatizo ya wananchi ambayo ni more pressing.
Tunachotaka kukiona kutoka kwa serikali ni
-Kuimarisha sekta za afya,miundombinu,elimu,ukusanyaji wa kodi na kuweka mikakati ya kulinda maliasili zetu na sio kutupa changa la macho kurusha Mig-21 tatu then waseme wametumia Bilioni xy katika sherehe hizo.
Maonyesho haya ,issue ya kukimbiza mwenge wa Uhuru yamepitwa na wakati.Panatakiwa kiongozi jasiri kama Hayati Moringe Sokoine alivyo simamisha zoezi la wananchi kuacha shughuli zao na kujipanga barabarani siku nzima kuwalaki viongozi wa kitaifa walipokuwa wanatembelea maeneo mbalimbali cnhini.