ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 27, 2014

Lipumba,Maalim Seif,Duni ni noma


Wakati Mkutano Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) ukiwarejesha madarakani Profesa Ibrahim Lipumba, na Maalim Seif Sharif Hamad, kwa kishindo, Waziri wa Afya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar, Juma Duni Haji, amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti mpya wa chama hicho.

Kabla ya Duni kuchaguliwa juzi, nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Machano Khamisi Ali, aliyeamua kutoitetea kutokana na sababu za kiafya.

Duni akiwa mgombea pekee, alichaguliwa na Mkutano Mkuu kushika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, baada ya kujizolea kura 662 sawa na asilimia 99.25 kati ya kura 667 zilizopigwa, huku kura tano (asilimia 0.75) zikimkataa.


Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na Mwanasheria, Awadh Ali Said, Profesa Lipumba alichaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa CUF Taifa kwa kupata kura 659 (asilimia 95.5) na kumshinda mpinzani wake, ambaye ni Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Shinyanga Mjini, Chifu Lutalosa Yemba, aliyepata kura 30 (asilimia 4.3).

Mgombea mwingine wa nafasi hiyo, M’bezi Adam, alijitoa dakika chache kabla ya kura kupigwa, kwa madai kwamba, tathmini imemuonyesha kuwa nafasi aliyotaka kuigombea ni mzigo mkubwa kwake kuubeba na kubaki wagombea wawili; Profesa Lipumba na Yemba.

Pia Maalim Seif alichaguliwa tena kuendelea na wadhifa wa katibu mkuu wa chama hicho kwa kupata kura 675 (asilimia 99.5) kati ya kura 678, huku kura tatu zikimkataa.

Awali, kabla ya uchaguzi huo, Profesa Lipumba alisema akichaguliwa atahakikisha anatembelea nchi nzima kuimarisha chama kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Pia atafanya juhudi za ziada kuona kuwa Tanzania inakuwa na Muungano wa kuheshimiana baina ya pande mbili za Muungano (Tanzania Bara na Zanzibar).

Vilevile, wanawake watapewa nafasi ndani ya kamati tendaji ya chama kuondosha dhana ya mfumo dume unaodaiwa kuwepo katika ngazi za juu za uongozi.

Maalim Seif alisema aliamua kugombea ili ashirikiane na wenzake kushika hatamu za dola Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema mwaka 1989, yeye na wenzake walifukuzwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwalimu Julius Nyerere kwa sababu walionekana kuwa ni wapinzani na kutakiwa upinzani wao wakaufanye nje ya CCM.

“Ndiyo maana mpaka leo niko upinzani. Na mpaka kufa kwangu nitaendelea kuipinga CCM,” alisema Maalim Seif.

Naye Duni alisema iwapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo atashirikiana na viongozi wengine wa kitaifa pamoja na wananchi kuhakikisha kuwa chama kinapata maendeleo zaidi.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: