Akitoa taarifa kwenye mkutano wa wananchi wa kitongoji hicho juzi, Mwanaharakati wa Ansaf, Deogratius Chaze, alieleza kuwa, jumla ya Sh. milioni 48 kati ya Sh. milioni 67 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya mradi huo zimetumika kinyume na utaratibu.
Chaze, ambaye alikuwa akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Katibu Mtendaji wa Jukwaa la Kilimo, Audax Rukonge, wataalamu wa kilimo wilayani humo na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo, alidai kuwa asilimia 52 ya fedha hizo ndizo zilizotumika kwa mujibu wa sheria na kwamba asilimia 48 hazifahamiki zilipo.
Alisema gharama halisi ya mradi huo ni Sh. milioni 45.4 pamoja na ujenzi wa mfereji na Sh. milioni 5 kwa ajili ya utafiti, lakini imebainika kuwa miongoni mwa matumizi yalikiuka taratibu.
Aidha alitoa mfano wa ukiukwaji huo kuwa ni matumizi ya Sh. milioni 10 kwa ajili ya utafiti badala ya Sh. milioni 5 zilizopashwa kutumika, pamoja na malipo ya malazi kwa wataalamu visivyostahili na kusababisha matumizi yasiyo halali kufikia kiasi hicho cha fedha.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa mradi huo, Yassin Bayn, alitaja miongoni mwa mambo yaliyosababisha kuzorota kwa mradi huo kuwa ni kushindwa kufanyakazi kwa mashine ya kusaga na kukoboa nafaka na Power Tiller, ambavyo tangu vinunuliwe havijawahi kutumika kutokana na kutofaa.
Bayn alisema zana hizo walizinunua kwa maelekezo ya wataalamu wao wanaosimamia mradi huo, lakini licha ya kuonyesha uwezo mdogo wa kufanyakazi, hakuna jitihada zozote zilizochukuliwa kuhakikisha zinatumika na mradi huo kutekelezeka.
Akionyesha kushtushwa na taarifa hiyo, Gambo, alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Lucas Mweri, kufuatilia tuhuma hizo na kuagiza hatua za kinidhamu kuchukuliwa kwa watu waliohusika na hujuma hiyo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment