ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 19, 2014

Posho ya kina Chenge balaa

  Kila mjumbe analamba Sh. 500,00 kwa siku
  Bajeti safari za Rais yazidi kuhojiwa
Mbunge wa Bariadi Magharibi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Andrew Chenge

Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Andrew Chenge imetajwa kwamba wajumbe wake wanalipwa posho ya kutisha kwa siku.

Siri hiyo imeibuliwa bungeni na na Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali akisema kwamba kila mjumbe analipwa Sh. 500,000 wanapokuwa katika vikao.

Akichangia Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/15 bungeni, Mkosamali aliiponda kamati hiyo kuwa haifanyi kitu cha maana, badala yake inafanya vikao visivyoisha na mashirika kuhusu namna yatakavyolipa kodi wakati wajumbe wake hawana utalaamu huo na baadaye kupokea posho hiyo kubwa.

“Kamati ya Bajeti inalipwa posho ya Sh. 500,000 kila siku, ni kutafuna fedha tu hapa, hakuna kitu, ni kutengeneza rushwa…wanaita mashirika kukubaliana nayo,” alisema na kuhoji: “Kamati inajua kukadiria mambo ya kodi?”

Kamati hiyo ina wajumbe 14. Wajumbe hao ni Christine Lissu, Kidawa Hamii Saleh, Mansoor Shaniff Hiran, Amina Abdallah Amour, Joseph Selasini na Josephat Kandege.

Wengine ni Dk. Cyril Chami, Dk. Bulugu Limbu, Mwigulu Nchemba, Assumpter Mshama, James Mbatia, Beatrice Shellukindo na Hamad Rashid Mohamed.

Kwa mana hiyo, kamati hiyo inapokutana kwa siku jumla ya Shilingi milioni saba zinalipwa kwa wajumbe hao.

Kiasi hicho cha posho ni kikubwa sana kulipwa kwa wabunge wa Bunge hilo na hata Bunge Maalum la Katiba.

Bunge Maalum la Katiba kila mjumbe analipwa Sh. 300,000 kwa ajili ya vikao na posho ya kujikimu.

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano walikuwa wanalipwa posho ya takribani Sh. 250,00 kwa siku kwa ajili ya kujikimu na vikao kabla ya kuongezewa hivi karibuni.

Wakati huo huo; wabunge wameishambulia serikali bungeni wakiilalamikia kutenga fedha nyingi katika bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2014/2015, kwa ajili ya ziara za Rais, huku ikiyapa kisogo mambo ya msingi ya taifa.

Wabunge hao ni Halima Mdee (Kawe) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), ambao wote kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

MDEE ATEMA CHECHE
Mdee alisema anashangazwa na hatua ya serikali kutenga mabilioni ya shilingi kwa ajili ya safari za nje za Rais na kuzitengea fungu finyu baadhi ya wizara.

“Mimi ni miongoni mwa wabunge wakongwe. Maana niko humu bungeni tangu 2005. Ninaelewa jukumu la Bunge siyo kuisifia serikali, bali kuikosoa kwa kutotekeleza mambo ya msingi. Baadhi yetu tumelisahau hilo,” alisema Mdee.

Aliongeza: “Sote tunatambua watu waliokuwa upande wetu (upinzani) waliokuwa wakijipendekeza CCM, sasa wanapigika. Kama kuna mbunge anafikiri kujipendekeza CCM aachie ngazi ili ateuliwe na Jakaya (Kikwete) kushika nafasi anazoona zinamfaa.”

Alisema anashangaa kuona baadhi ya wabunge wanaunga mkono bajeti hiyo licha ya kutambua kwamba, haitekelezeki.

Aliongeza: “Tumewadharau wakulima. Bajeti ya miradi ya maendeleo ya kilimo Sh. bilioni 51. Lakini safari za Rais Sh. bilioni 50. Ndiyo maana anakuja kukutana na wasanii hapa, pesa hazina pa kwenda.”

Mdee aliihoji serikali kwa kushindwa kudhibiti upotevu wa Sh. trilioni tatu kila mwaka kwa kupelekwa kwa wawekezaji wasio waaminifu.
Alisema Sh. trilioni 1.4 kwa mwaka zinapotea kutokana na misamaha ya kodi kwa wafanyabiashara, matajiri wakubwa na vigogo.

Mdee alisema Kamati ya Bajeti mwaka wa pili inalalamika kwamba, inatoa mapendekezo kwa serikali kuhusu vyanzo mbadala vya mapato vinavyopotoea, lakini inaipuuza.

“Mtuambie hivi vyanzo mbadala vinavyozungumzwa mmevifanyia kazi vipi?” alihoji.

Alisema kama Kamati ya Chenge imelalamika kwa asilimia 90 kwenye bajeti hiyo halafu inaunga mkono Watanzania wanaambiwa nini.

Mdee alisema serikali inapatoeza mabilioni ya shilingi kwa sababu ya kulinda wavuvi wakubwa kwenye bahari kuu

“Nilimnukuu naibu waziri wa fedha akisema anataka kutoa fedha kwenye viburudisho, visodasoda. Mbona haionyeshi kwenye bajeti yenu vipo wapi?” alihoji.

Alisema Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ana ripoti ya ukusanyaji wa fedha kila mwaka na misamaha ya kodi, hivyo kuwaambia Watanzania kuwa hawalipi kodi ni kuwadharau.

“Viroba, pombe kali, sigara wanazovuta kwa sababu ya stress (msongo wa mawazo) maji, wanalipa Watanzania maskini indirect tax (kodi isiyo ya moja kwa moja), wanalipa kodi kubwa kuliko watu wote kwenye kila bidhaa wanayotumia,” alisema.

Alisema serikali haikutoa taarifa za kweli kuhusu mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi 43 katika shule ya msingi na mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi 28 katika shule ya sekondari.

Alisema ripoti ya utekelezaji ya mwaka jana inasema kilimo kimepewa Sh. bilioni 51 kwa mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), lakini bajeti ya Rais ni Sh. bilioni 50. Wakati kilimo kinachoajiri asilimia 75 ya Watanzania na kusaidia ukuaji wa uchumi imepewa Sh. bilioni 51 tu.

Mdee alisema Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani analalamika fedha anazozipata ni pungufu ya Sh. bilioni 20.

MSIGWA APIGILIA MSUMARI WA MOTO
Mchungaji Msigwa aliishauri serikali kuleta wataalamu wa masuala ya fikra kwa ajili ya kuwanoa viongozi mbalimbali wa taifa, ambao alidai uwezo wao wa kufikiri umefikia kikomo.

Alisema haiungi mkono bajeti hiyo kwa kuwa haitekelezeki na imeandaliwa kwa ajili ya kuwahadaa wananchi.
Alilitaka Bunge kuwa makini katika kujadili mambo ya msingi kwa taifa na kuwachukulia hatua stahiki watendaji wa serikali wasiotekeleza wajibu wao.

“Mnasimama hapa na kutoa majibu ya kisiasa. Mnaonekana sasa mmefika baa. Mmetuletea 'slogans' (sera) nyingi; Mkurabita, Mkukuta na sasa BRN. Tunapigiana makofi wakati bajeti ya ujenzi haipo hapa kwa sababu kuna madeni na pesa iliyotengwa itaishia kuyalipa. Tuna matatizo ya kifikra,” alisema Msigwa.

Aliongeza: “Ninafikiri tutafute wataalamu wa fikra wakae na uongozi kuupa mawazo mapya. Haiingii akilini umtengee kiongozi wa nchi Sh. bilioni 50 kwa ajili ya safari za nje halafu Wizara ya Afya uitengee Sh. bilioni 46 za miradi ya maendeleo. Tutafute wataalamu maana watu wanaonekana wamegoma kufikiri.”

“Ninaamini wataalamu hawa watatupa mawazo mapya maana hata BRN mmeiiga kutoka kwao. Waiteni hawa watu na tumrudie Mungu, maana kila kitu sasa hakiendi,” alisema Msigwa.

Imeandikwa na John Ngunge, Sanula Athanas na Beatrice Bandawe, Dodoma.
CHANZO: NIPASHE

No comments: