ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 27, 2014

Mamia wauaga mwili wa Sista aliyeuawa


Masista wakitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza lenye mwili wa Sista Cresensia Kapuli aliyeuawa kwa kupigwa risasi na majambazi Juni 23, 2014.

Mamia ya waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Makoka wamejitokeza kuuaga mwili wa marehemu Sista Crensensia Kapuli, aliyefariki dunia Juni 22, mwaka huu, baada ya kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi maeneo ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Akisoma mahubiri katika ibada iliyohudhuriwa na maaskofu, mapadri, masista na viongozi wa serikali na wananchi, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda, Gervas Nyaisonga, alisema kanisa linapaswa kuwasamehe watu waliomuua kikatili sista huyo na kuomba Mungu ili kuepusha vitendo vya watu kutafuta mali kwa njia ya udhalimu.


Alisema vitendo vya mauaji vinavyotokea nchini vinapaswa kudhibitiwa kuanzia ngazi ya familia, ambako ndiko wanakotokea wahalifu badala ya kuliachia Jeshi la Polisi pekee ili kudhibiti vitendo hivyo, huku akiwataka watawa kutokakata tamaa katika kazi wanayoifanya ya kutumikia jamii.

“Tumesikitishwa kuona sista, ambaye amejitolea maisha yake kwa ajili ya kuitumikia jamii anauawa kinyama namna hii,” alisema.

Aliongeza: “Kinachotakiwa kufanyika ni familia kuimarisha malezi ndani ya familia na sisi kanisa hatuna budi kusamehe watu hawa kama kristo yesu alivyotufundisha, kwani tumaini letu kubwa ni Mungu.”

Alisema tukio la wahalifu hao limekutanisha kundi la watu wengi, hivyo jamii inapaswa kujifunza kwa kujenga misingi bora ndani ya familia.

Aliwataka waumini kutokuchoka kuwaombea watu waliohusika ili wabadilike na wanaoendelea kufanya hivyo wakose amani maishani mwao milele.

Awali, akiongoza ibada hiyo ya kuuombea mwili ya marehemu Sista Crensensia, maaskofu wasaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, na Titus Mdoe, waliitaka jamii kubadilika na kuendelea kumuomba Mungu dhidi ya vitendo vya uhalifu nchini.
 

CHANZO: NIPASHE

No comments: