Mwenyekiti wake Butiama apigwa risasi na kufa
Polisi wanaofukuzwa kazi wahofiwa kuchochea uhalifu
Polisi wanaofukuzwa kazi wahofiwa kuchochea uhalifu
Kuuawa kwa kiongozi huyo wa CCM, Willison Opiyo (60) kumetokea takribani siku tano baada ya mtawa wa Kanisa Katoliki, parokia ya Makoka jijini Dar es salaam, Sista Clecensia Kapuli (50), kuuawa kwa kupigwa risasi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Samson Winani, amethibitisha kuwa mwili wa marehemu Opiyo umefikishwa na kuhifadhiwa kwenye hospitali ya mkoa iliyo mjini Musoma.
Kwa mujibu wa Dk. Winani, taratibu za uchunguzi na masuala mengine yatakayohitaji ushiriki wa madaktari, vitafanyika baada ya vikao na uamuzi kati ya ndugu ya marehemu na jeshi la polisi waliomfikisha hospitalini hapo.
Kama ilivyokuwa kwa Sista Kapuli, kifo cha Opiyo kinaelezwa kusababishwa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi.
Mbali na Sista Kapuli na Opio, kumekuwapo matukio kadhaa ya watu kuuawa kwa kupigwa risasi, huku kukiwa hakuna matokeo ya kuridhisha katika jitihada za kukabiliana na tatizo hilo.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa majambazi hao, yalimpiga Opiyo risasi moja kichwani na ‘kukisambaratisha’.
Mauaji hayo yalifanyika majira ya usiku wa jana, ambapo majambazi hao yalivunja mlango wa nyumba aliyokuwa amelala kiongozi huyo na familia yake huko katika kijiji cha Kwikuba.
Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa (RCO) wa Mara, Kamishna Msaidizi wa Polisi Robert Mlashan, alisema majambazi hao walivunja milango miwili ya nyumba hiyo, kisha kupiga risasi tatu ambapo moja ilimpata kichwani kiongozi huyo wa CCM na kufa papo hapo.
Inaelezwa kuwa, baada ya kufanya mauaji hayo, walimtoa nje mke wa marehemu, Agnes Wambura, huku wakimpiga kwa kutumia bapa za panga na kumlamisha awaonyeshe mahali zilipo fedha.
Hali hiyo ilimlazimu Agnes kuwapa Sh. 400,000 alizozikopa kutoka taasisi moja ya mikopo, wakatoweka nazo.
Hata hivyo, RCO Mlashan, alisema jeshi la polisi litafanya kila liwezavyo kuhakikisha wale wote waliohusika katika mauaji hayo, wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Pia aliwaomba raia wenye taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa washukiwa wa tukio hilo, kuisaidia polisi ili kuleta ufanisi katika kuwatia nguvuni.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Busambala, Hamis Nyakulinga, aliitaka polisi kuendesha msako ambao utawezesha kukamatwa kwa wahusika ili kuondoa hofu wananchi.
Mmoja wa mashuda wa tukio hilo, Mkama Magambo, alisema waliamushwa usingizini kwa milio ya risasi, kisha milango kuvunjwa na baada ya muda mfupi kukatokea majibizano kati ya marehemu na majambazi hao wanakisiwa kuwa zaidi ya wawili.
Magambo ni mmoja wa watu waliolala kwenye nyumba ya marehemu Opiyo wakati tukio hilo likitokea.
“Nilisikia watu wanasema fungua mlango haraka, marehemu akawauliza, niufungue mlango kuna nini,baada ya hapo nikasikia milio ya risasi, kisha walianza kumpiga bapa za panga shangazi ambaye ni mke wa marehemu,” alisema.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Busambala, Abed Makamba, alithibitisha kuisikia milio ya bunduki na yowe, akawa miongoni mwa waliochukua silaha za jadi kwenda kusaidia.
Alisema, baada ya kufika eneo la tukio, alikuta watu wakiwa wamejumuika huku mwili wa Opiyo ukiwa chini ukivuja damu na taarifa ikatolewa kwamba ameuawa.
POLISI WAHUSISHWA KUCHOCHEA UHALIFU
Wakati huo huo, hatua ya jeshi la polisi nchini, kuwataka askari wanaodaiwa kugushi vyeti vya shule ‘kujifukuzisha kazi’ kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria, imetajwa kuchangia ongezeko la uhalifu nchini.
Vyanzo tofauti vimeeleza kuwa, hatua hiyo ilistahili kuchukuliwa katika hatua za awali za kujiunga katika jeshi hilo, ikiwamo kuzitumia asasi zenye mamlaka na ujuzi wa kuhakiki vyeti vya kuhitimu elimu ya sekondari na vyuo.
Miongoni mwa vyanzo hivyo ni askari polisi waliohojiwa na NIPASHE Jumapili, katika maeneo tofauti mkoani Mara.
Wamedai kuwa jeshi hilo limeagiza askari polisi wenye vyeti vya kughushi, wajiondoe wenyewe kabla ya uamuzi wa kuwatimua na kuwachukulia hatua haujafanyika.
Wanaoukosoa mpango huo, wanaeleza kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha wahusika, hususani waliolitumikia jeshi hilo kwa muda mrefu, kuondoka na ili kukidhi mahitaji yao, wakajihusisha na uhalifu.
“Unatarajia nini, nimekaa jeshini kwa miaka mitano au zaidi, nina familia, nina ujuzi wa kijeshi, kisha nifukuzwe kazi kwa sababu ambazo zingetumika katika hatua za awali za ajira yangu,” alihoji mmoja wa askari polisi wa mjini Tarime.
Pia, afisa mmoja wa polisi ambaye hakutaka jina lake kutajwa, alisema hatua hiyo ikitekelezwa inapaswa kufanyika kwa umakini ili kuepuka madhara yanayoweza kuzuiliwa kwa jamii.
“Hoja hapa si kuwafukuza kazi, kwani tayari kosa limefanyika, kilichotakiwa ni kuwataka askari hao sasa kujiendeleza kielimu ili waweze kuendelea kulitumikia jeshi,vinginevyo badala ya kusafisha jeshi tutajikuta tunaongeza shida ndani ya jamii,”alisema.
Afisa huyo alisema hatua za uwajibikaji zinapaswa kuchukuliwa pia dhidi ya kamati za ulinzi na usalama za wilaya na mkoa.
Alisema kamati hizi zilizo juu ya zile za kuanzia ngazi ya kijiji hadi tarafa, zinaongozwa na wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakuu wa idara ya usalama wa taifa katika ngazi hizo.
“Inakuwaje kupitia hatua hizo, ishindwe kubainika mapema kuhusu vyeti vya kugushi hadi watu wajiunge na kupata mafunzo ya kijeshi, ndipo litoelewe agizo la kuwasaka,” alihoji.
IGP: WATAFUKUZWA
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema utaratibu uliopo si wa askari kujiondoa, bali wataondolewa kwa mujibu wa taratibu na kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Tutawaondoa na tukifikia hatua hiyo tutawaambia kama tulivyowaambia kuhusu wale askari wanafunzi tuliowandoa pale Chuo Cha Polisi (CCP) Moshi,”alisema.
Kuhusu tishio la askari walioghushi vyeti kujihusisha na uhalifu, IGP Mangu, alisema hatua ya kuwafukuza kazi haihusiani na ongezeko la uhalifu nchini.
“Tutawaondoa tu, mbona wale askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wanakaa kambini kwa miaka miwili, tena wamejifunza matumizi ya silaha, baadaye wanarudi uraiani, hamhoji kwa hilo, kwanini iwe kwa askari polisi,”alihoji.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment