“Kuna baadhi ya watu tumewabaini wamefanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji wetu ilihali wakitambua kuwa wachezaji hao wana mikataba na ni mali ya Mbeya City, kamwe hao watu hatutawafumbia macho na tutawapeleka kwenye mamlaka husika.
UONGOZI wa klabu ya Mbeya City, umepanga kuwashtaki baadhi ya matajiri wa timu kubwa nchini kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kupata ushahidi wa wao kufanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo wenye mikataba.
Ingawa haijapenda kuwataja kwa majina, lakini Mwanaspoti linajua ni wa Simba. Simba imedaiwa kufanya mazungumzo na wachezaji, Deus Kaseke na Saady Kipanga, ambao wana mikataba isiyopungua mwaka mmoja na nusu kila mmoja kitu ambacho ni kinyume na kanuni za usajili.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Steven Mapunda, aliongeza kuwa timu hiyo haitakaa mezani kuzungumza na timu yoyote ile juu ya mauzo ya wachezaji kwani haina mpango wa kuuza mchezaji yeyote katika dirisha hili la usajili zaidi ya kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao.
“Tunataka kuzifundisha nidhamu timu za Ligi Kuu, msimamo wetu wa mwisho ni kwamba hatuuzi mchezaji yeyote na hatutokaa mezani kuzungumza na timu yoyote ile, waache kutusumbua kwa kutupigia simu, na kiongozi au mpambe yeyote atakayekuja Mbeya atakuwa amepoteza nauli yake bure,” alisema.
“Kuna baadhi ya watu tumewabaini wamefanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji wetu ilihali wakitambua kuwa wachezaji hao wana mikataba na ni mali ya Mbeya City, kamwe hao watu hatutawafumbia macho na tutawapeleka kwenye mamlaka husika.
“Haijalishi mchezaji anataka kuondoka au la, asiyetaka kucheza tutampeleka kwenye kazi nyingine, nawaomba na hawa watu waache kuwasumbua wachezaji wetu kwani hakuna mchezaji atakayeuzwa wala kuondoka kwa wale wote tunaowahitaji, hatubabaishwi na fedha zao.”
Jeuri ya Mbeya City imekuja siku chache baada ya klabu hiyo kupata udhamini wa miaka miwili kutoka kampuni ya Binslum wa Sh360 milioni ili kutangaza bidhaa za kampuni hiyo hivyo kuiongeza uwezo wa kujiendesha. Timu hiyo inamilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Credit:Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment