Waombolezaji wakiwa nyumbani kwa aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo cha Mtakatifu Augustino (Saut), marehemu Nkwabi Ng’wanakilala jijini Mwanza jana. Picha na Michael Jamson
Mwanza. Mhadhiri Mwandamizi Idara ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine Tanzania (Saut), Nkwabi Ng’wanakilala, amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa Bugando.
Akizungumza kwa simu kutoka Dar es Salaam jana, Kaimu Makamu Mkuu wa Saut, Profesa Cassian Magori alisema nguli huyo wa habari alifariki dunia usiku wa kuamkia jana.
“Ni kweli tumepokea taarifa za kushtusha leo (jana) asubuhi kwamba mhadhiri wetu amefariki dunia. Sipo Mwanza hivi sasa kutokana na kukabiliwa na shughuli za kikazi hapa Dar es Salaam, lakini taratibu zote zinaendeshwa na Padri Peter Mwanjonde anayekaimu nafasi yangu,” alisema Profesa Magori.
Naye Padri Mwanjonde alisema Ng’wanakilala ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Redio Tanzania (RTD), alifanyiwa upasuaji, lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya na kuwekwa Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU).
“Nafahamu Jumanne alifanyiwa upasuaji ingawa hakupata nafuu, baadaye alihamishiwa ICU kwa bahati mbaya asubuhi hii (jana) tumepokea taarifa za kifo chake,” alisema Padri Mwanjonde na kuongeza: “Tayari tumeunda kamati itakayojulisha chanzo cha kifo hicho baada ya kupata cheti, au kushauriana na madaktari waliokuwa wakimhudumia.”
Hata hivyo, Padri Mwanjonde alisema ni mapema kuzungumzia shughuli za mazishi, kwa sababu uongozi wa chuo lazima kwanza ushauriane na familia.
Msemaji wa familia
Akizungumza nyumbani kwao Malimbe Nyegezi, Lugendo Ng’wanakilala ambaye ni mtoto wa marehemu, alisema mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa kesho kupelekwa Dar es Salaam kwa maziko.
Alibainisha kuwa baba yake alifariki kutokana na utumbo kujikunja na kufanyiwa upasuaji Bugando.
Mtoto huyo wa marehemu alisema kuwa baba yake alizidiwa mwanzoni mwa wiki hii na kupelekwa hospitali ambapo baada ya kufanyiwa uchunguzi, ilibainika utumbo ulikuwa umejikunja na kutakiwa kufanyiwa upasuaji.
“Jumanne alifanyiwa operesheni baada ya hapo akapelekwa Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU), alikuwa akisaidiwa na mashine kupumulia,” alisema.
Ng’wanakilala alifafanua kuwa Jumatano waliondoa mashine na aliweza kujaribu kuzungumza ingawa kwa tabu.
“Ijumaa tuliandikiwa kwenda kununua dawa kutokana aina hiyo kutokuwa hospitalini hapo, wakati tunajiandaa asubuhi leo (jana) kununua dawa siku ya tukapigiwa simu na mama mdogo kuwa mzee amefariki dunia,” alisema Ng’wanakilala
Ng’wanakilala alizaliwa 1949 Kata ya Buhongwa, mkoani Mwanza na kupata elimu sehemu mbalimbali. Ameacha watoto 11; Wavulana watano na wasichana sita. Naye Mkuu wa Idara ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma Saut, Imane Duwe alisema pengo lililoachwa halitazibika, kutokana na utendaji na umahiri wake kazini.
“Alikuwa mtu mahiri na mweledi wa kutosha, itachukua muda kumpata mtu kama huyu kwenye idara yetu,” alisema Duwe.
Ng’wanakilala amefanya kazi kwenye tasnia ya habari akiwa mhadhiri, mtafiti, mshauri, mchapishaji binafsi na mwandishi. Alijiunga Saut Idara ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, akiwa Mhadhiri Mwandamizi tangu Septemba 1999.
Pia, alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Majaji ya Tuzo ya Mwangosi, ambayo iliratibiwa na Muungano wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).
Mwananchi
No comments:
Post a Comment