JESHI la Polisi mkoani Mwanza, limelazimika kutumia mabomu
ya machozi kuwatawanya wafanyabiashara ndogo (wamachinga) waliokuwa wanapinga
kuondolewa katika eneo la Kempu na eneo la soko la Makoroboi jijini humo.Aidha,
hatua hiyo imesababisha vurugu na kusimamishwa kwa shughuli mbalimbali za
kijamii, ikiwemo kufungwa kwa maduka hadi katikati ya eneo la jiji na baadhi ya
huduma ya usafiri kukosekana kwa muda katika barabara zinazokatiza katikati ya
jiji hilo, ambapo kuanzia nne asubuhi hadi tunaenda hewani mashuhuda wanasema
vurugu hizo bado zinaendelea.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Valentino Mlowola, ameumbia mtandao
huu leo Juni 11, 2014 kuwa Jeshi hilo limelazimika kutumia mabomu hayo ili
kuwatawanya wafanyabiashara hao waliokuwa wakihatarisha amani na kusema bado
hakuna mtu yeyote aliyeripotiwa
kujeruhiwa katika vurugu hizo.
Serikali yatakiwa kuingilia kati migogoro ya wamachinga
Akiomba mwongozo Bungeni mjini Dodoma, Mbunge wa Nyamagana,
Ezekiel Wenje, ameitaka serikali kusitisha zoezi hilo ili kutafuta njia mbadala
ya kushughulikia migogoro kati ya serikali na wamachinga.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na
Bunge), William Lukuvi, amesema kuwa Serikali inashughulikia suala hilo ili
kubaini ukweli na itatoa taarifa Bungeni baada ya kuhakikisha tukio hilo.Katika
mtandao wa JamiiForums, kumekuwepo na mjadala wa tukio hilo ambapo mdau
aliyejitambulisha kwa jina la Mashimba 1, alisema “Mabomu ya machozi yanapigwa
kila kona ya mji kufuatia bomoaboma ya vibanda vya machinga eneo la Makoroboi,
ilikuwa nifanye shughuli zangu hapa lakini naona haiwezekani, huu utawala wa
kibabe siku moja utatufikisha kusikostahili" akionekana kukwazwa na hali
iliyotokea jijini humo
No comments:
Post a Comment