Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipoulizwa kuhusu uamuzi huo unaoikosesha Tanzania mabilioni ya fedha alisema hana taarifa.
Dar es Salaam. Tanzania imeanza vibaya usimamizi wa uwekezaji wa madini ya urani, baada ya kushindwa kesi mahakamani hivyo kukosa karibu Sh340 bilioni.
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilifungua kesi katika Baraza la Kodi ikiituhumu Kampuni ya JSC Atomredmetzoloto (ARMZ) ya Urusi, kwamba imekwepa kiasi hicho cha kodi ambacho ilidai kilipaswa kulipwa kama kodi ya ongezeko la mtaji (Capital Gain Tax).
TRA walishindwa kesi hiyo mara nne na kwa mara ya kwanza ilikuwa katika Baraza la Rufaa za Kodi (Tax Revenue Appeals Board), ambako Kampuni ya ARMZ ilikata rufaa katika kesi namba 26 na 27 za 2011 kupinga malipo ya kiasi cha kodi ilichokuwa ikidaiwa.
Baada ya kushindwa katika hatua hiyo, TRA walikata rufaa mara ya tatu mbele ya Mahakama ya Rufani za Kodi (The Tax Revenue Appeals Tribunal), lakini walishindwa hivyo kutoa uhalali wa ARMZ kutolipa fedha hizo.
TRA katika rufani zake walitaka JSC Atomredmetzoloto (ARMZ) walipe kodi ya ongezeko la mtaji kwa madai kwamba kampuni hiyo ya kigeni ilikuwa imenunua hisa kutoka Kampuni ya Matra Resources Ltd, hivyo ilipaswa kulipa fedha hizo kwa mujibu wa sheria.
Msingi wa madai ya TRA ni Sheria ya Kodi ya Mapato ya 2014 kifungu cha 90 (1) kama kilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Fedha (Finance Act) ya 2012 ambayo ilipitishwa na Bunge ikielekeza kampuni zinazouza hisa zake kwa kampuni nyingine, kutozwa asilimia 20 ya kiasi cha thamani ya hisa, ikiwa ni Kodi ya Ongezeko la Mtaji.
Katika madai hayo, TRA ilitaka ilipwe kiasi cha Dola za Marekani 196 milioni, sawa na asilimia 20 ya thamani ya hisa zilizouzwa kwa ARMZ (Dola za Marekani 980 milioni) na Dola za Marekani 9.8 milioni ambazo ni ushuru wa stempu kwa mujibu wa sheria ya ushuru ya 2008. Katika hukumu zake, mahakama ilisema hakukuwa na uhamishaji wa hisa ndani ya Kampuni za Mantra, kwa sababu Mantra Tanzania ni sehemu ya kampuni tanzu ya Mantra ya Australia.
Kadhalika mahakama ilisema katika uamuzi wake kwamba, TRA haina uwezo wa kisheria kudai kodi kutoka ARMZ kwa kuwa kampuni hiyo haikusajiliwa nchini, bali Urusi ambako inapaswa kulipa kodi zake.
Kauli za TRA, wizara
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipoulizwa kuhusu uamuzi huo unaoikosesha Tanzania mabilioni ya fedha alisema hana taarifa.
“Sina taarifa hiyo, waulize TRA, pengine wanafahamu,” alijibu Profesa Muhongo kwa ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu yake ya kiganjani.
Mkurugenzi wa Elimu na Huduma za Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema hana taarifa rasmi kuhusu suala hilo.
“Sina taarifa rasmi kuhusu suala hilo. Kwanza hilo ni suala la kisheria na linashughulikiwa na wanasheria wetu, hadi watakaponijulisha,” alisema Kayombo.
Alipoulizwa kama TRA ina mpango wa kuendelea kukata rufaa, alisema hiyo ni siri ya ofisi. “Hata kama tuna mikakati yetu ya kisheria, hatuwezi kuviambia vyombo vya habari,” alisema Kayombo.
Katibu wa Baraza la Rufani za Kodi, Respicius Mwijage, alisema kesi hiyo ni mfano mmojawapo wa Tanzania kuendelea kuwa maskini licha ya kuwa na rasilimali nyingi.
“Unajua kwa nini Tanzania inaendelea kuwa maskini?” alihoji na kutaarifu: “Kwanza Serikali haitaki kuongeza wataalamu, pili hata mchango wa wataalamu wachache waliopo hautiliwi maanani na tatu baadhi ya wataalamu siyo waaminifu, wanapotosha mambo kwa makusudi na msingi wa yote hayo ni rushwa.”
Kwa nini TRA ilishindwa
Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria wa Mazingira (LEAT), Dk Rugelemeza Nshala alisema, kifungu cha 9 (1) cha Sheria ya Madini ya 2010 kinaruhusu kampuni kuhamisha hisa zake kwa ruhusa ya mamlaka ya leseni ambaye ni kamishna wa madini.
“Kifungu cha 36(1) cha cha sheria ya Kodi ya Mapato kinaonyesha kuwa Mantra Resources Ltd ilipaswa kulipa kodi (capital gain tax) kwa Serikali ya Tanzania, lakini hilo halikufanyika,” alisema Nshala na kuongeza:
“TRA ikaanza kuishupalia ARMZ kulipa kodi hiyo na ushuru unaofikia Dola za Marekani 200 milioni sawa na Sh340 bilioni.”
Alisema uamuzi wa mahakama za kodi wa kuwapa ushindi ARMZ umezingatia maelezo yaliyotolewa katika mahakama hizo kwamba Kampuni za Mantra Resources Ltd, Uranium One na ARMZ ni kampuni dada na siyo tofauti.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 9(3) cha sheria ya madini, haihitajiki ruhusa ya mwenye mamlaka ya leseni yaani kamishna wa madini au waziri wakati wa kuhamisha hisa kwa kampuni pacha,” alisema Dk Nshala.
Maelezo hayo yanaungwa mkono ofisa mmoja wa Taasisi ya Revenue Watch, Silas Olang ambaye alisema sheria za kodi zina upungufu mwingi ambao hauiwezeshi TRA kuwabana wawekezaji kulipa kodi.
Akizungumzia kesi hiyo, Olang alisema TRA imeshindwa kutokana na upungufu katika sheria.
MWANANCHI
1 comment:
Wajinga waliwao
Post a Comment