| walalamikaji |
WAKAZI
wawili wa kijiji cha Tagamenda mjini Iringa, wameiomba Wizara ya Nishati na
Madini kuwasaidia ili wapate fidia kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
baada ya kupitisha miradi ya umeme kwenye mashamba yao.
Shabani
Mkakato na Kassim Mpingo kwa pamoja walizuiwa kuendelea na shughuli zozote
katika mashamba yao yaliyopo jirani na kituo kidogo cha kuzalisha umeme cha
Tagamenda, mjini Iringa baada ya Tanesco kupitisha miradi hiyo.
Wakizungumza
na habarileo juzi walisema walipeleka maombi ya kufanyiwa tathimini na kulipwa
fidia za mali na mimea iliyokuwa katika mashamba hayo lakini shirika hilo
limewapa masharti yaliyo nje ya uwezo wao.
“Tulipeka
barua kwa meneja wa Tanesco mkoa wa Iringa na katika majibu yake tunahisi haki
yetu itapotea,” alisema Mkakato.
Akifafanua
kuhusu miradi hiyo, Mpingo alisema ni ya umeme unaokwenda Ifunda, Sabasaba,
Isimani na Cotex.
Alisema
wakati nguzo nne zilipitishwa katika shamba lake lenye ukubwa wa ekari moja,
nyingine nne zilipitishwa kwenye shamba la mlalamikaji mwenzake Mkakato.
Alisema
maeneo hayo ambayo hajapimwa walikuwa wanayamiliki kimila lakini walilazimika
kuondoka baada ya kutolewa maagizo hayo ikiwa ni kupisha ujenzi wa miradi hiyo.
“Katika
mashamba hayo kulikuwa na miti ya kupandwa, ya matunda na mazao mengine
mbalimbali kama mahindi, mikunde na maharage,” Mpingo alisema.
Mwenyekiti
wa kijiji cha Tagamenda, Mwagike Mwagike alithibitisha watu hao kumiliki maeneo
hayo kabla miradi hiyo ya Tanesco haijapitishwa.
“Nachofahamu
ni kwamba watu wengine waliopitiwa na miradi hiyo katika eneo hilo walikwishalipwa
fidia zao, sasa sijui wakati wa tathimini na malipo hayo hawa walikuwa wapi?”
alisema.
Katika
majibu yake kwa watu hao aliyoyatoa kupitia barua ya Mei 22, mwaka huu ikiwa na
kumbukumbu Na RM/IRA/CUST/2 Meneja wa Tanesco Mkoa wa Iringa, Mhandisi Sarah
Assey anasema wameshindwa kuyashughulikia madai hayo kwasababu ya maombo ya
walalamikaji hao kutojitosheleza.
“Hujatueleza
ni lini nguzo hizo zimewekwa kwenye eneo husika na zinahusika na mradi upi wa
umeme. Kwa barua hii basi tunaomba utufahamishe ni mwaka gani nguzo hizo
zimewekwa kwenye eneo hilo na zinaelekea wapi ili kama shirika tuweze
kuyafanyia kazi madai yako,” inasomeka barua ya Tanesco iliyoandikwa kwa
Mpingo.
Mpingo alisema mgogoro uliopo na ambao wanaohofia unaweza kukwamisha upatikanaji wa haki zao ni kipengele kilichopo katika barua ya meneja huyo kinachotaka walalamikaji hao waambatanishe kivuli cha hati miliki ya eneo husika, wakati maeneo hayo wao walikuwa wakiyamiliki maeneo hao kimila kwa kuwa hayajapimwa.
No comments:
Post a Comment