
Mbunge wa Mwibara,Kangi Lugola
Wabunge wa Jamhuri ya Muungano hawajalipwa posho za kujikimu walizotakiwa kulipwa Juni 16 na sasa watalipwa wakati Bunge litakapoahirishwa Julai 1, mwaka huu.
Vilevile, NIPASHE imebaini kuwa wabunge hao hawajalipwa pia posho za vikao, ambazo kwa kawaida hulipwa kati ya Jumatatu na Jumanne na haijulikani kama leo watalipwa.
Kila mbunge hulipwa Sh. 80,000 kwa ajili ya kujikimu na Sh. 220,000 kwa kuhudhuria kikao kwa siku.Naibu Spika wa Bunge,Job Ndugai, alithibitisha kuwapo hali hiyo na kwamba, inafanyiwa kazi.
Naibu Katibu wa Bunge hilo, John Joel, alisema kwa kuwa fedha zinazotumika kuwalipa wabunge posho hizo zinatolewa na serikali, yupo kwenye wakati mgumu kujibu sababu za malipo hayo kuchelewa.
Hata hivyo, Joel aliwataka wabunge kutokuwa na wasiwasi kwa sababu suala hilo linashughulikiwa na watalipwa tu, ingawa hakueleza lini.
Naye Kamishna wa Tume ya Maslahi ya Wabunge, ambaye pia ni Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), ingawa hakueleza kinachosababisha kuchelewa kwa malipo hayo, alisema Katibu wa Bunge (Kashililah) hana hatia kwa sababu naye anategemea fedha kutoka Hazina.
Alisema wameshirikiana naye kufuatilia malipo hayo na kusema: “Serikali nayo imekaa kimya tu, sijui inataka wabunge waanze kupiga miayo na kusinzia bungeni badala ya kutoa michango ya kuboresha bajeti?”
Hata hivyo, Lugola alisema malipo hayo yatafanyika na kwamba, wanaotumia benki ya CRDB wanaweza kupokea ndani ya siku tatu, huku wale wanaotumia benki ya NMB wakitarajia kupokea fedha hizo kati ya siku mbili mpaka tatu tangu hundi itakapopelekwa benki.
Alisema ikiwa wabunge wamefikia hatua hiyo katika kuidai serikali, hapati jibu anapofikiria hali waliyonayo watumishi wengine wa umma, hususan serikalini.
Mbunge wa Nkasi, Ally Keissy, alikejeli wanaolalamika kucheleweshewa malipo ya posho kuwa wanasumbuliwa na madeni waliyokopa kwenye taasisi za fedha, akisema wanapolalamikia kucheleweshewa posho ilhali wana mishahara minono wanasahau watumishi serikalini, kama walimu na wauguzi, ambao katika mazingira tofauti wamekuwa wakihamishwa bila kulipwa maslahi wanayositahili.
“Kwanza mimi huwa sifahamu kama posho zimeingizwa kwenye akaunti yangu au la. Hayo mambo kwangu hayana umuhimu sana. Ninachapa kazi. Mambo mengine yanajiseti yenyewe. Siyo wengine wanachojua ni kulaumu watumishi kupikiwa chai wakati nao wanapokuwa kwenye kamati mbalimbali wanakunywa na hawasikiki kuhoji," alieleza Keissy.
Awali, mmoja wa wabunge, bila kufahamu ananukuliwa alisikika akizungumza na mbunge mwenzake, ambaye kwa mujibu wa mazungumzo yao, alikuwa akiulizia kama posho zimelipwa.
“Yaani serikali imefikia kutukopa hata sisi, ngoja tusubiri kesho (jana) wasipolipa siyo siri hali itakuwa mbaya kwa wengi wetu,” alisikika akimjibu mwenzake.
NIPASHE imebaini kwamba, waliocheleweshewa malipo siyo wabunge pekee, bali hata watumishi wa afya, kwenye zahanati ya wabunge hawajalipwa tangu Mei, mwaka huu.
“Watano walianza zamu Mei 5 mpaka Mei 18, mwaka huu na wengine watano wakaanzia tarehe mpaka wiki mbili baadaye tulipoletewa waraka kwamba, tangu hapo tutalipwa na hospitali,” alieleza mmoja wa watumishi hao kwa sharti la kutotajwa jina.
Kila mtumishi anatakiwa kulipwa 840,000, ambayo ni malipo ya wiki mbili sawa na Sh. 8,400, 000 kwa watumishi wote 10 kwa siku 28. Utaratibu huo wa Bunge kuita watumishi wa afya kutoka hospitali ya mkoa, ili kuhudumia wabunge katika zahanati ya Bunge nyakati za mikutano ya Bunge, ulibadilishwa baada ya Bunge kuingia mkataba na Wakala wa Bima ya Afya, Jubilee.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment