ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 24, 2014

Zengwe la Simba SC Mahakama Kuu laiva

Hatimaye wanachama 69 wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, jana wamefungua rasmi kesi wakiomba Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kutoa amri ya kusimamisha Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Juni 29, mwaka huu.

Wanachama watatu Joseph Waryoba, Said Monero na Hassan Hassan ndiyo waliowawakilisha wenzao katika maombi hayo ya zuio la muda la uchaguzi huo dhidi ya Rais Aden Rage na Baraza la Wadhamini la klabu hiyo. Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo kupitia hati ya dharura.

Wakili wa wanachama hao Revocatus Kuuli aliwasilisha maombi kwa nyakati tatu tofauti na kurudishwa kutokana na kuwa na makosa madogo madogo ya kisheria kabla ya kesi hiyo kusajiliwa saa 7:49 mchana.

Kesi hiyo ilipewa usajili namba 291 ya mwaka huu, ambayo wanachama hao wanaomba mahakama kutoa zuio la muda uchaguzi huo kwa kuwa unafanyika kinyume cha katiba ya klabu hiyo.

Mapema katika viunga vya mahakama hiyo, watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa Simba walifurika huku wakiwa wamekaa katika makundi makundi wakijadiliana kuhusu uchaguzi huo.

NIPASHE ilishuhudia Wakili Kuuli akiingia katika masijala ya mahakama hiyo kwa ajili ya kufungua kesi hiyo saa 4:00 asubuhi lakini kutokana na maombi hayo kuwa na upungufu wa kisheria waliamriwa wakarekebishe na kurejea saa 5:30 na kurudishwa kwa mara ya pili. Aidha, saa 7:49 mchana hati ya maombi hayo ilipokewa na kusajiliwa rasmi na sasa inasubiri kupangiwa jaji wa kuisikiliza.

Mapema Ijumaa iliyopita wanachama wanaodaiwa kumsapoti aliyekuwa mgombea wa Urais aliyeenguliwa, Michael Wambura, walidaiwa kupeleka maombi ya kusimamisha uchaguzi huo mahakamani lakini hayakufanikiwa kupokewa kutokana na mapungufu hayo.

Mbali na maombi ya kusimamishwa kwa uchaguzi, wanachama hao pia wameomba walalamikiwa walipe gharama za kesi pamoja na maamuzi mengine mahakama inayoona yanafaa.

Wakati huo huo, Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba jana ilitangaza rasmi majina 27 ya wagombea wanakaowania nafasi saba za uongozi wa klabu hiyo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumapili Juni 29 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Nafasi zitakazowaniwa katika uchaguzi huo utakaowaweka madarakani kwa muda wa miaka minne ni ya Rais, Makamu wa Rais na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji (watano) na huku mmoja wao akiwa ni mwanamke.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo, Damas Ndumbaro, alisema kuwa kamati yake imewapitisha wagombea ambao wana kesi za kimaadili kwa sababu bado hawajahukumiwa na tayari wameshawasilisha malalamiko hayo katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ili yafanyiwe kazi.

Ndumbaro alisema kuwa endapo wagombea hao watashinda na baadaye kukutwa na hatia, watapoteza viti vyao na uchaguzi mdogo utafanyika kujaza nafasi zao.

"Bado hakuna aliyetiwa hatiani, mtuhumiwa hapaswi kuonekana mkosaji mpaka pale atakapobainika kuwa ni mkosaji...kuna kesi sita za maadili na siwezi kuzielezea kwa sababu zilipokewa na sekretarieti ya TFF (Shirikisho la Soka la nchi)," Ndumbaro alisema.

Aliwataja wagombea waliopitishwa katika nafasi ya Rais kuwa ni Evans Aveva na Andrew Tupa wakati wanaowania Umakamu wa Rais ni Bundala Kabulwa, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na Swedi Mkwabi.

Wagombea wengine 18 wanaowania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji kwa upande wa wanaume ni Said Tulliy, Yasini Mwete, Ally Suru, Rodney Chiduo, Said Pamba, Ally Chaurembo, Abdulhamid Mshangama, Chano Almasi, Damian Manembe, Ibrahim Masoud 'Maestro', Iddi Kajuna Noor, Hamisi Mkoma, Alfred Elia, Saidi Kubenea, Idd Mkamballah, Juma Mussa, Maulid Abdallah na Collin Frisch.

Kwa upande wa wanawake wanaowania nafasi hiyo moja ni Amina Poyo, Asha Muhaji na Jasmine Badour.Kamati hiyo ilitangaza kuanza kwa kampeni na kueleza mwisho wa zoezi hilo kuwa ni Jumamosi Juni 28 saa sita kamili usiku.

Kamati hiyo ililazimika kupeleka malalamiko ya kimaadili FIFA kutokana na TFF kukataa Kamati yake ya Maadili kukutana kujadili kesi hizo kama kanuni za uchaguzi zinavyoelekeza kufuatia Simba kutokuwa na kamati hiyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: