Wataka JK awaombe radhi Warioba, wananchi
Sasa wajipanga mgombea mmoja urais 2015
Sharti moja kubwa ambalo ni gumu, wanataka Rais Jakaya Kikwete atumie kile walichokiita ‘uungwana’ kwa kukubali kukosea na kumuomba radhi aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Sharti lingine wanataka Rais Kikwete atumie pia uungwana kuwaomba radhi wajumbe wa tume hiyo pamoja na Watanzania kwa jumla.
Pia wanataka yafanyike marekebisho katika mfumo wa uendeshaji wa Bunge hilo, ikiwamo kurekebishwa kwa taratibu na kanuni zake.
Walitoa masharti hayo kwa nyakati tofauti wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Sita wa Chama cha Wananchi (CUF), ulioanza jana jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa vyama vya siasa, akiwamo Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Philip Mangula.
Wengine waliohudhuria ufunguzi wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe; Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Leticia Mosore; Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa; Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe na Mwenyekiti wa ADC, Said Miraji.
Pia walikuwamo kada wa CCM ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, Hassan Nassoro Moyo, wawakilishi wa balozi zinazowakilisha nchi zao, taasisi za kimataifa pamoja na wadau wa katiba nchini.
Mwenyekiti wa CUF, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, akifungua mkutano huo, alisema vurugu katika Bunge hilo zilizozaa matusi, kejeli, vijembe na maneno ya ubaguzi dhidi ya wajumbe wa Ukawa, zilisababishwa na Rais Kikwete.
Alisema hiyo ni baada ya kuikataa tume hiyo bila kujali hadhi na uzito wa wajumbe walioiunda, kama vile Jaji Warioba, Jaji Augustino Ramadhan, Dk. Salim Ahmed Salim na Joseph Butiku.
“Tukaona tuwaachie Interahamwe waendelee na Bunge lao,” alisema Profesa Lipumba.Hata hivyo, alisema jambo jema ni kwamba, mchakato wa katiba mpya umewaunganisha wale wanaotaka katiba ya wananchi.
Alisema kamwe Ukawa hawawezi kurudi kuendelea na Bunge hilo hadi hapo litakapojadili rasimu ya katiba iliyotolewa na tume hiyo, ambayo msingi wake ni matakwa ya wananchi kuwapo muundo wa Muungano wa serikali tatu nchini.
Mbali na hilo, alisema hakuna binadamu aliyekamilika, hivyo akasema muungwana kama akikosa hukubali na kumuomba radhi aliyemkosea na kwamba, kufanya hivyo siyo udhaifu, bali ni uimara.
“Kwa hiyo, mheshimiwa Kikwete amuombe radhi Jaji Warioba na wajumbe wa tume ya katiba. Pili, awaombe radhi Watanzania,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema ni jambo lisilowezekana Rais Kikwete kuridhia Sh. bilioni 70 kutumika kuendesha mchakato wa katiba halafu dakika za mwisho aruke kimanga na kuikataa kazi iliyofanywa na Tume ya Jaji Warioba.
“Kwa hiyo, udhaifu ni kutokuomba radhi. Ukiomba radhi Watanzania watakupenda na watakuheshimu,” alisema Profesa Lipumba.
KAULI YA MBOWE
Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, akitoa salamu za chama chake alisema licha ya ushirikiano wa wapinzani kupitia Ukawa kubezwa na watani zao, CCM, siyo wa mpito, bali ni wa kudumu.
“Tutakuwa wendawazimu kama hatujajifunza katika historia. Umoja wetu hautaishia kwenye katiba, lazima utuongoze katika mipango yetu ya kulikomboa taifa, kuanzia uchaguzi wa serikali ya mtaa, udiwani, ubunge mpaka urais,” alisema Mbowe.
Alisema ili ushirika wao uwe na nguvu, ni lazima vyama vyao viwe na nguvu na siyo kutegemea tu Ukawa kufikia lengo hilo.
Alimtaka Mangula kupeleka salamu kwa CCM na serikalini kwamba, kamwe katiba haiwezi kupatikana kwa vijembe, matusi, kejeli, ubabe, majeshi mengi na kutisha, bali kwa njia ya maridhiano na kuheshimiana.
Hivyo, akasema kama kweli serikali ina dhamira njema ya kupatikana kwa katiba inayoridhiwa na wananchi, yanahitajika marekebisho.
Alisema ni uwendawazimu kurejea katika Bunge hilo, huku kanuni na taratibu zilizopo zikiridhiwa kuendelea kutumika.
“Tukubaliane maeneo ya msingi ya kurekebisha,” alisema Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Kuhusu kutekwa Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu (Tahliso), Musa Mdede, Mbowe alisema wanahitaji siasa za kistaarabu na siyo za kutekana, kung’oana meno, kupigana mabomu kwa kuwa zimepitwa na wakati. Alisema siasa zinazohitajika ni za kuheshimiana.
PHILIP MANGULA
Mangula akitoa salamu za CCM katika mkutano huo, aliupongeza ushirika wa vyama na kusema anauheshimu.
Alisema hata Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1995 aliwahi kusema: “Siyo vizuri kuwa na utitiri wa vyama dhaifu na kwamba, angependa siku moja CCM ingepasuka na kuwa vipande vipande ili kuwa na upinzani wa kweli.”
Kutokana na kauli hiyo ya Mwalimu Nyerere, Mangula aliwaeleza wapinzani kuwa: “Nikweli mkiweka nguvu ya pamoja ni vizuri kuliko nguvu ya mtu mmoja.”
Aliitaka CUF kuimarisha umoja akisema kama watafanya hivyo watakuwa wameimarisha umoja katika taifa. Pia aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kujifunza kuvumiliana.
Alisema kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) wamekuwa wakitumia fursa hiyo kujadili mambo yanayohusu taifa, hivyo alitaka uvumilivu wa kisiasa kutoishia kwenye ngazi ya juu, bali uwe kwa wote.
Alionyesha masikitiko yake dhidi ya baadhi ya vyama vya siasa, ambavyo tangu vianzishwe havijawahi kufanya mkutano mkuu hata mmoja.
NAIBU MSAJILI
Kuhusu vyama ambavyo havijafanya mikutano mikuu, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alisema ofisi yake inaangalia vizuri sheria ili kuhakikisha demokrasia inakuwapo ndani ya vyama.
PROFESA LIPUMBA
Awali, Profesa Lipumba alionyesha wasiwasi wake juu ya uwezekano wa vitambulisho vipya vya kupigia kura kutolewa kutokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuhitaji Sh. bilioni 293, huku serikali ikiitengea Sh. bilioni 7.07 kufanikisha kazi hiyo na muda uliobaki kufika Uchaguzi Mkuu mwakani.
Aidha, alionyesha wasiwasi wake juu ya kudumu kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar kutokana na kuwapo sekretarieti isiyokuwa na weledi. Vilevile, alisema nchi inakabiliwa na changamoto za kujenga uchumi na kutumia rasilimali kuleta neema na kujenga demokrasia ya kweli.
Mkutano huo, ambao unaendelea leo, unatarajiwa kuhitimishwa Ijumaa, pamoja na mambo mengine kuchagua viongozi wapya ngazi ya taifa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment