
TUNAENDELEA kujifunza kuhusu mapenzi marafiki zangu. Hakuna kitu kibaya kama kukaa na upweke moyoni. Kamwe usijaribu kufikiri kuwa huna haki ya kuwa na mwenzi wa maisha. Ni mawazo potofu.
Hata kama utakuwa umekaa peke yako kwa kipindi kirefu, amini kuwa kuna mahali pengine ulikuwa unakosea ndiyo maana ikawa hivyo na sasa unatakiwa kujitambua na kuanza mambo kwa upya kabisa.
Kama mtakumbuka, wiki iliyopita tuliishia pale niliposema, lazima uanze kwa kujitambua.
Kujipa thamani na kujipenda. Ndugu zangu, hakuna anayependa kuwa na mtu ambaye hana desturi ya usafi, hata kama ni mzuri kisi gani.
Unapokuwa upo rafu sana hakuna mtu ambaye atausumbua moyo wake kuanza kukufikiria wewe usiyejipenda.
Siyo lazima wakati wote uwe safi, kwa kuwa inawezekana wengine wanafanya kazi ngumu ambazo mazingira yake lazima anakuwa mchafu, lakini baada ya kazi unapaswa kuwa msafi kabisa mbele za watu.
Upande wa wasichana siyo lazima uweke nywele dawa au usuke rasta wakati vitu hivyo huna uwezo navyo, unaweza ukasuka vizuri au wakati mwingine ukanyoa mtindo mzuri unaokubalika ambao hautakutafsirisha vibaya kwa jamii.
Anza kujipenda kabla ya kuhitaji upendo kutoka kwa mtu mwingine, hiyo itakusaidia kuwa na mvuto na mwonekano mzuri kiasi cha kuweza kumpagawisha mtu mwingine kuanza kuhisi cheche za moto wa mapenzi katika moyo wake.
LAZIMA UJIAMINI
Hili ni tatizo lingine ambalo kwa kweli ni la kisaikolojia zaidi kwa sababu kuna baadhi ya watu wanakosa kujiamini.
Kuna mwingine anaweza akakaa kwenye kioo kwa saa kadhaa na kuanza kujitoa kasoro katika mwili wake.
Hujiona mbaya asiyevutia na ambaye hana thamani kabisa katika ulimwengu wa mapenzi, hujiona hawezi kupata mpenzi katika maisha yake yote baada ya kujitoa kasoro hizo.
Ndugu yangu kasoro unaziona mwenyewe, acha kujitoa kasoro, unatakiwa kujiamini. Nani amekuambia una kasoro? Mshukuru Mungu kwa kukuumba jinsi ulivyo, amini kuwa Mungu ana makusudi yake kukufanya ulivyo.
Kujitoa kasoro na kutojiamni ni kosa baya kwa kuwa unakuwa unajiathiri kisaikolojia na kujiona hufai kabisa kupedwa mwisho wa yote unakuja kumparamia mtu yeyote kwa nia ya kujiondolea mkosi na akishakutumia anakuacha solemba unabaki na machungu moyoni na kujiongezea matatizo zaidi.
Naamini baada ya kujipenda wewe mwenyewe na kujiamini kuwa unavutia, utakuwa katika hali ya kawaida kisaikolojia na wakati mwingine sasa anaweza akajitokeza akupendaye na kukuomba hifadhi ya moyo katika moyo wako.
ANZA UCHUNGUZI
Sababu ya kukaa muda mrefu bila mpenzi au kutamkiwa kuwa unapendwa isiwe chanzo cha kupata maumivu mapya ya moyo. Acha papara, tulia, pata wasaa wa kumchunguza huyo anayedai anakupenda kwa muda wa kutosha kwa kuwa inawezekana naye akawa ni mmoja kati ya wale wanaotaka kukufanya chombo cha starehe!
Baada ya kukuomba muwe pamoja kimapenzi unatakiwa kumchunguza kwanza na hata baada ya kumchunguza usiruhusu aujue mwili wako kabla ya kuelewa nia yake hasa kwako ni ipi, starehe ya muda mfupi au anakuhitaji kimaisha.
Usifanye mambo kwa papara, unahitaji utulivu wa kutosha ili uweze kumpata yule ambaye ni muhimu kwa ajili yako.
Ukijiamini na kuwa makini ni wazi kuwa utampata yule anayekupenda kwa dhati.
Hadi wiki ijayo katika mada nyingine, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.
GPL
No comments:
Post a Comment