ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 26, 2014

Wakwepa kodi watorosha Sh409 bilioni kila mwaka

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda.PICHA|MAKTABA

Dar es Salaam. Tanzania imekuwa ikipoteza kiasi cha Sh409.2 bilioni (Dola za Marekani 248 milioni) kwa mwaka kutokana na udanganyifu katika uagizaji wa mafuta unaofanywa na baadhi ya kampuni za uchimbaji wa madini na uagizaji wa bidhaa zilizowekeza chini ya mpango wa Kanda Maalumu za Kiuchumi (Export Processing Zones – EPZ).
Hasara hiyo ya mabilioni ya shilingi inatokana na kampuni husika kuongeza thamani za bidhaa zinazoziagiza kutoka nje kinyume na uhalisia, hali inayoathiri tozo za kodi nyingine zinazopaswa kulipa nchini na wakati huo kuhamishia nje kiasi kikubwa cha fedha kwa njia hiyohiyo.
Ripoti ya hivi karibuni ya taasisi ya Global Financial Integrity (GFI) inaonyesha kuwa kutokana na ukwepaji kodi unaofanywa kwa njia hizo, Tanzania imepoteza kiasi cha Sh13.2 trilioni (Dola 8 milioni) kati ya 2002–2011.

Kufichuliwa kwa utoroshaji huo wa kiwango kikubwa cha fedha, kumekuja wakati ambao Serikali inakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo katika bajeti yake ya 2014/15, kiasi cha kusababisha mvutano baina yake na Bunge.
Kati ya zaidi ya Sh533.6 bilioni zilizokuwa zikihitajika kwa nyongeza katika maeneo kadhaa ya bajeti hiyo, Serikali kwa kushirikiana na Kamati ya Bunge ya Bajeti ilifanikiwa kupata kiasi cha Sh225.3 tu, ambazo zilikuwa katika matumizi mengineyo na safari za Rais nje ya nchi.
Kama Serikali ingeweza kudhibiti utoroshaji wa fedha kama ripoti ya GFI inavyoonyesha, kungekuwa na upungufu wa Sh124.6 bilioni pekee.
Ripoti hiyo iliyopewa jina ‘Hiding in Plain Sight - Trade Misinvoicing and the Impact of Revenue Loss’ inaweka wazi athari za utoroshaji wa fedha kwa katika utafiti uliofanywa Ghana, Kenya, Msumbiji, Tanzania na Uganda.
“Uhamishaji wa fedha kwa njia haramu kwenda nje ya nchi unajitokeza kwa kiasi kikubwa katika mchezo wa kuongeza bei za uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, suala ambalo linazua maswali mengi kuhusu jinsi Tanzania inavyoweza kukusanya ushuru wake wa forodha kama sehemu ya mapato katika bajeti yake,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo na kuongeza:
“Rasilimali hizi muhimu zingeweza kutumika kutengeneza ajira zaidi, kugharimia sehemu kubwa ya huduma za jamii kwa ajili ya kubadili maisha ya Watanzania wa kawaida na kuboresha miundombinu ambayo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi.”

Fedha zinavyotoroshwa
Ripoti imeweka wazi jinsi wawekezaji kupitia EPZ na kampuni za uchimbaji wa madini wanavyotumia fursa ya misamaha ya kodi inayotolewa na Serikali kujinufaisha kwa kukwepa kodi na kusafirisha fedha nje ya nchi kinyume cha sheria.
Ikumbukwe kuwa wawekezaji katika ukanda maalumu wa kiuchumi kwa ajili ya mauzo ya bidhaa husika nje ya nchi, hupewa vivutio kadhaa vikiwamo vya kutotozwa ushuru wa forodha kwa malighafi na mahitaji mingine ya uwekezaji wanayoiagiza kutoka nje ya nchi.
Katika mazingira hayo, ripoti hiyo inasema baadhi ya wawekezaji huongeza bei kwenye nyaraka za kibiashara ambazo huzitumia kuagiza bidhaa ambazo zinapoingizwa, bei zake huwa pungufu hivyo kiasi cha fedha kinachosalia hufichwa kwenye akaunti za siri katika nchi ambako zimelipwa.
Ripoti hiyo inafafanua kuwa udanganyifu huo pia ni chanzo cha kuinyima Serikali mapato mengine kutoka kwa kampuni husika, kwani kiasi cha fedha ambacho husomeka kwenye nyaraka za kibiashara za uagizaji wa biashara, huhesabiwa kama sehemu ya gharama za uwekezaji hivyo kuathiri ukadiriaji wa kodi nyingine zinazopaswa kulipwa na kampuni husika ifikapo mwishoni mwa mwaka.
“Mchezo huu wa kuongeza gharama kwenye nyaraka za uagizaji bidhaa nje ya nchi, ulianza kukua kwa kasi 2008, mwaka ambao pia yalianzishwa maeneo haya ya ukanda maalumu wa uwekezaji,” inasema ripoti ya sehemu hiyo.

Dk Kigoda
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda alisema nchi zote duniani zenye maeneo ya aina hiyo hutoa vivutio kwa wawekezaji lengo likiwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya kuuza nje ya nchi na kukuza uchumi.
“Malengo ya viwanda vyote vinavyowekeza katika maeneo ya aina hii huwa ni asilimia 20 tu ya bidhaa zake ndizo huuzwa katika soko la ndani, kiasi kilichobaki cha asilimia 80, kinapaswa kuuzwa nje ili kutupatia fedha za kigeni na kuchangia kukua kwa uchumi wetu,” alisema Dk Kigoda.
Hata hivyo, alisema hakuwa ameona ripoti inayoeleza uozo unaofanywa wawekezaji kupitia EPZ na kwamba Serikali haijapata taarifa wala kufahamu iwapo kuna ukwepaji wa kodi na uhamishaji wa mitaji unaofanywa na viwanda kwa njia hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), Dk Adelhelm Meru alisema: “Hizo takwimu, siyo za kweli. Wamechukua misamaha ya kodi ya madini, sekta binafsi na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kuibambikia EPZA. Nilishajibu hayo maswali kipindi cha nyuma.
“Taarifa ya CAG kwa EPZA mwaka 2014 inaonyesha tumesamehe kodi ya Dola 7 milioni sawa na Sh12.4 bilioni hadi mwaka 2012. Hizo takwimu zao si za kweli. Isitoshe, sisi hatushughuliki na kampuni kongwe kibiashara, tunatoa leseni kwa kampuni mpya zinazoanza.
Kampuni za madini
Udanganyifu pia umetajwa kufanyika kwa kiasi kikubwa katika nyaraka za uagizaji wa mafuta unaofanywa na baadhi ya kampuni za madini, huku sehemu ya bidhaa hiyo ikionekana kutoka Uswisi na Singapore.
“Wachumi wetu wamebaini asilimia 67 ya udanganyifu unaofanywa katika nyaraka za mauzo na uagizaji wa bidhaa unaozihusisha Uswisi na Singapore, lakini ukichunguza zaidi unabaini kwamba udanganyifu kwenye nyaraka za kuagiza mafuta kwa zaidi ya asilimia 25 zilihusu uagizaji wa mafuta kutoka Uswisi pekee,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo nakuongeza:
“Kwa kufanya hivyo, kampuni nyingi zimeweza kupunguza kiwango cha mapato yake yanayotozwa kodi (kwa kuongeza gharama za mafuta kama sehemu ya matumizi ya kibiashara) hivyo kukwepa kulipa kodi nyingine kama vile kodi ya kampuni (corporate tax) Tanzania.”
Uswisi imekuwa ikitajwa kuwa maficho ya fedha nyingi zinazoibwa kutoka Afrika na kwingineko duniani, ikiwamo Tanzania. Taarifa za 2011 kutoka Uswisi zilizoonyesha kuwa kulikuwa na kiasi cha Sh327.9 bilioni za Tanzania zilizofichwa kwenye benki za nchi hiyo, lakini ripoti mpya ya 2012 ya Benki za Uswisi inaonyesha kuwa fedha hizo zimepungua hadi Sh291.96 bilioni.
Tayari Tanzania imeomba msaada kwa taasisi iitwayo International Centre for Asset Recovery – ICAR (Kituo cha Kimataifa cha Urejeshaji wa Mali) ya Uswisi kuchunguza kesi tano zinazohusu watu na taasisi zinazotuhumiwa kuficha mabilioni ya fedha nchini humo.
Gazeti hili lilifuatilia suala hilo hadi nchini Uswisi na kubaini kuanza kwa uchunguzi huo.
MWANANCHI

1 comment:

Anonymous said...

Nyie mawaziri ndiyo mnaotorosha pesa nje na kukwepa kodi and sasa mnasema nini tena ...endeleeni kuiba msidanganye mtu sasa hivi. Au kama mnataka kuwa wakweli basi semeni ukweli simnajuana nani anatorosha pesa