ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 7, 2014

Warioba ataka wazee waondoke madarakani


“Mwalimu Julius Nyerere aling’atuka akiwa na nguvu zake kabisa. Kiasili kung’atuka ni dhana ya kuwapisha vijana kuwa mbele katika kutekeleza majukumu na ninyi wazee siyo kuondoka, bali kuendelea kuwapa ushauri na mwongozo.” Jaji Joseph Warioba. Picha na Maktaba  
Kwa ufupi
Amesema kuwa ni vyema kwa viongozi hao kung’atuka ili
kutoa nafasi kwa vijana wenye nguvu na akili kulitumikia taifa katika uongozi.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amewashauri viongozi wazee na waliokaa madarakani muda mrefu kuacha kung’ang’ania madaraka.
Amesema kuwa ni vyema kwa viongozi hao kung’atuka ili kutoa nafasi kwa vijana wenye nguvu na akili kulitumikia taifa katika uongozi.
Warioba aliyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu na gazeti hili, pamoja na mambo mengine alizungumzia uongozi wa nchi hii.
“Mwalimu Julius Nyerere aling’atuka akiwa na nguvu zake kabisa. Kiasili kung’atuka ni dhana ya kuwapisha vijana kuwa mbele katika kutekeleza majukumu na ninyi wazee siyo kuondoka, bali kuendelea kuwapa ushauri na mwongozo,”alisema Jaji Warioba.
Alieleza kuwa kung’atuka kunamfanya aliyechukua hatua hiyo kuishi maisha ya raha yenye furaha na amani jambo ambalo yeye sasa analifurahia.
Aliongeza: “Haiwezekani mzee ukakaa kundi moja na kijana wako aliyetahiriwa juzi, kwani kwa kawaida, kijana akitahiriwa hupandishwa daraja na kukaa kundi la wakubwa, hapo wewe baba yake hata kama una miaka 40, unahamishwa na kuingia kundi la wazee.”
Alifafanua kuwa hata katika uongozi ni muhimu kung’atuka na kuwapisha vijana ili waweze kutumia akili na nguvu zao kuendeleza taifa huku wakipata maelekezo na mwongozo kutoka kwa wazee.
“Maisha yangu sasa baada ya kuacha uongozi ni ya furaha na amani bila woga kuliko wakati wowote, tofauti na nilipokuwa bado kiongozi katika Serikali,” alisema.
“Ukiwa kiongozi unaweza kuishi kwa hofu na shaka huku ukituhumiwa,” alibainisha Jaji Warioba aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mwaka 1985 - 1990.
Kauli ya Warioba imekuja huku kukiwa na kundi kubwa la viongozi wenye umri mkubwa katika nafasi mbalimbali madarakani muda mrefu, huku wakiendelea kutamani nafasi za juu zaidi. Miongoni mwa viongozi hao, wapo wanaotajwa kuunda makundi ya kusaka urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.
Hii siyo mara ya kwanza viongozi wenye umri mkubwa kutakiwa kung’atuka madarakani.
Januari 14, 2010, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliwashauri wazee watumie busara kupima uamuzi wa kugombea tena nafasi za ubunge kwenye uchaguzi mkuu. Pinda alitoa rai hiyo alipokuwa akijibu maswali ya wahariri katika mkutano alioitisha kujibu maswali yao jijini Dar es Salaam.
Alibainisha kuwa kwa sasa Tanzania haina tena uhaba wa vijana wasomi na wataalamu wa kuitumikia nchi yao katika nafasi mbalimbali.
“Nafikiri Mkoa wa Rukwa umeonyesha mfano. Mzindakaya na Kimiti wametangaza kung’atuka, nafikiri wazee wengine wafuate busara hiyo,” alisema Pinda.
Dk Chrisant Mzindakaya alikuwa Mbunge wa Kwela na mwenzake, Paul Kimiti alikuwa Mbunge wa Sumbawanga Mjini.
Alisema kuwa rai ya kutaka wazee kung’atuka madarakani ina mambo mawili, ikiwamo kupumzika kwa watu waliokaa madarakani kwa muda mrefu na kwa watu walio na umri mkubwa.
Warioba alisema mtazamo wake ni vyema kuwa na ukomo wa mtu kuwa mbunge, ambapo alipendekeza vipindi vitatu vya miaka mitano mitano yaani miaka 15.

1 comment:

Unknown said...

Sawa kabisa Jaji. Hawa wazee wanagombea sinia moja la mpunga na vijana badala ya kwenda kula na wazee wenzao. Aibu tupu. Wanaogopa nini kwenda kula upande wa wazee waliotahiriwa nao pamoja
? Au ndiyo ule uzee wa umri tu lakini akili ya kitoto...? Heko Jaji, leo umewaumbua. Inaonekana hawaondoki mpaka waone masinia ya mpunga hayapiti tena toka jikoni. Iwapo yataendelea kutoka jikoni basi nawao hawaondoki. Nasikiaga wanasemaga "...haondoki ntu hapa..." Duh! Maanake nzi kufia kwenye kidonda...