KLABU ya Yanga imeibua mpya baada ya kudai kwa sasa adui yao mkubwa ni mabingwa wa soka Tanzania Bara, Azam FC.
Kauli hiyo imekuja baada ya hivi karibuni Azam FC kuwapiga bao kwa kuwasajili waliokuwa nyota wao, mshambuliaji Didier Kavumbagu na kiungo Frank Domayo ‘Chumvi’.
Akizungumza makao makuu ya Klabu ya Yanga jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Matawi ya klabu hiyo, Mohamed Msumi, alisema Azam FC kwa sasa ndiye adui yao namba moja huku akidai kuwa Simba wao watataendelea kuwa watani zao tu.
“Azam FC ndiye adui namba moja wa Yanga, lakini Simba ndiye mtani wetu wa jadi, hivyo basi Wanayanga tujiepushe kwenye migogoro ambayo inampa adui nafasi na tukiendelea hivi, hata Mbeya City tutazidi kumpa nafasi,” alisema Msumi huku baadhi ya viongozi wa matawi wakishangazwa na kauli hiyo iliyokuwa nje ya alichotakiwa kuzungumza.
Katika hatua nyingine, Msumi ameutaka uongozi wa Yanga, kuwaandikia barua kwa mujibu wa katiba, wanachama wote ambao wanakiuka katiba ya klabu hiyo na sio kuwafukuza kwa maneno tu.
Hata hivyo, kauli hiyo aliitoa baada ya viongozi wenzake wa matawi, kumwalika ili atoe msimamo wa kile walichokizungumza katika kikao chao cha hivi karibuni na yeye kuanza kuizungumzia Azam.
Credit:Mtanzania Daima
No comments:
Post a Comment