Dar es Salaam. Kikosi cha Usalama Barabarani kimewatimua kazi askari wake 27 kwa madai ya kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Kamanda wa polisi wa kikosi hicho, Mohamed Mpinga alisema jana kuwa askari hao walifanya makosa hayo kinyume cha kanuni na sheria za jeshi hilo.
Mpinga alisema askari hao walifukuzwa kazi kati ya Januari na Juni mwaka huu.
Alisema kuwa askari hao wametimuliwa kazi ili kurejesha imani kwa wananchi waliolalamika kukithiri kwa rushwa barabarani.
“Hatua zimechukuliwa dhidi ya askari 27 waliotuhumiwa kujihusisha na rushwa,” alisema Mpinga.
Wakati huohuo, Mpinga alisema takwimu zinaonyesha kuwa ajali za barabarani zimepungua kwa kiasi kikubwa kulinganisha na zile zilizotokea mwaka uliopita.
Alisema kuwa kupungua kwa ajali hizo kumeleta nafuu kubwa kwa jamii ambayo imekuwa ikiandamwa na mfululizo wa ajali hizo.
Mpinga alifafanua kuwa kufikia Juni mwaka huu, ajali za barabarani zilikuwa 8,405.
Mwaka jana peke yake kulikuwa na ajali 11,311. Alisema kutokana na kupungua kwa ajali hizo, pia idadi ya majeruhi imepungua.
Majeruhi walioripotiwa mwaka jana walikuwa 9,889, lakini kufikia Juni idadi ya majeruhi ilikuwa 7,523.
Alisema ingawa idadi ya ajali na majeruhi imepungua, vifo viliongezeka.
“Mwaka jana kulikuwa na vifo vya ajali za barabarani 1,739 lakini mwaka huu vimeongezeka hadi 1,743.”
Alisema mikoa inayoongoza kwa ajali barabarani kwa kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu ni Kinondoni ikifuatiwa Ilala, Temeke, Morogoro na Kilimanjaro.
Aidha, kati ya Januari hadi Juni mwaka huu, makosa yalikuwa 515,677 na mwaka 2013, 301,404 ikiwa ni ongezeko la makosa 214,273, sawa na asilimia 71.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment