ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 2, 2014

Askofu ajitosa Ukawa

Asema rasimu ikichakachuliwa wananchi waikatae
Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda

Wananchi wameshauriwa kupiga kura ya hapana wakati wa kupiga kura ya maoni ikiwa rasimu ya katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, itachakachuliwa katika Bunge Maalumu la Katiba.

Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tec), Askofu Severin Niwemugizi, ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge, alitoa ushauri huo wakati akitoa salamu za pongezi kwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Taricisius Ngalalekumtwa, ambaye pia ndiye Rais wa Baraza hilo.

Askofu Ngalalekumtwa alikuwa akiadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya uaskofu wake, iliyofanyika jana katika viwanja vya Kanisa Katoliki Kihesa mjini Iringa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo wa kidini, serikali na siasa.

Askofu Niwemugizi alisema wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanapaswa kuhakikisha watakachojadili katika Mkutano ujao wa Bunge hilo, ni rasimu ya katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Warioba, na siyo vinginevyo.

Alisema iwapo hilo halitafanyika, basi wananchi wapige kura ya hapana katika hatua ya mwisho ya mchakato wa mabadiliko ya katiba, ambayo ni upigaji kura ya maoni kwa ajili ya kuipitisha rasimu hiyo au kuikataa.

Alilitahadharisha Bunge hilo na uchakachuaji wowote utakaofanywa dhidi ya rasimu hiyo, ambayo ni maoni yaliyokusanywa n Tume kutoka kwa wananchi.

Pia, aliwataka wajumbe wa Bunge hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurudi bungeni kuendelea kuijadili rasimu ya katiba bila mashariti yoyote.

Alisema huu ni wakati wa kuliombea taifa, kwani nchi imegawanyika, huku watu wachache kuhodhi rasilimali na kujitarisha na kuwaacha waliowengi wakiwa maskini.

Askofu Niwemugizi alisema mchakato wa kuandika katiba mpya umeshatumia fedha nyingi za walipakodi, hivyo akawataka viongozi na wajumbe wa Bunge hilo kuhakikisha wanakaa na kujadili rasimu hiyo, kwani ndiyo itakayotoa mwelekeo wa taifa na wananchi wake.

Ukawa unaoundwa na wajumbe wa Bunge hilo kutoka vyama vya upinzani vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na baadhi ya wajumbe walioteuliwa na rais kupitia taasisi mbalimbali wanaojulikana kwa jina la “kundi la 201” walitoka nje na kususia vikao vya Bunge hilo mjini Dodoma, Aprili 16, mwaka huu.

Katika madai yao, walieleza kutoridhishwa na mwenendo wa Bunge hilo wakidai kwamba wenzao wa chama tawala (CCM) wamepanga kupenyeza kinyemela rasimu mbadala tofauti na ile iliyowasilishwa bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Warioba.

KAULI YA PINDA
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alilitaka kanisa kuliombea taifa ili lipite salama katika mchakato wa kuandika katiba mpya.

Alisema mchakato kama huo umeingiza mataifa mengi katika machafuko na umwagaji damu kutokana na makundi ya wanasiasa wenye maslahi tofauti kushindwa kukubaliana, hivyo kushindwa kuvumiliana.

Askofu Ngalalekumtwa ameadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya Uaskofu wake na miaka 40 ya Upandre tangu alipopewa daraja hilo la upadre mwaka 1973. Baadaye, alisimikwa kuwa Askofu mwaka 1989.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wakiongozwa na Pinda.

Viongozi wengine waliohudhuria sherehe ni Rais mstaafu, Benjamin Mkapa; Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma.

Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi; Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ritha Kabati.
CHANZO: NIPASHE

No comments: