ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 17, 2014

Bakhressa amwaga mamilioni Jumuiya ya Madola

Kampuni ya Bakhressa (SSB) ya jijini Dar es Salaam ambayo pia inamiliki timu ya soka ya Azam FC jana ilikabidhi hundi ya Dola za Marekani 93,000 (Sh. milioni 154) kwa ajili ya kusaidia wachezaji wa Tanzania wanaokwenda katika Michezo ya 20 ya Jumuiya ya Madola ambayo inafanyika Glasgow nchini Scotland.

Timu hiyo ya Tanzania yenye wanamichezo 39, makocha na viongozi wengine iliondoka nchini jana kuelekea Glasgow tayari kushiriki michezo hiyo inayotarajiwa kufanyika kuanzia Julai 23 hadi Agosti 3 mwaka huu.

Akikabidhi fedha hizo, meneja wa kampuni hiyo, Said Mohammed, alisema kuwa wameitikia wito waliopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, wa kusaidia michezo hapa nchini.

Mohammed alisema kuwa fedha ambazo kampuni hiyo inapata zinatokana na jasho la Watanzania hivyo wameona ni wakati sahihi kurejesha sehemu ya pato hilo kwa kusaidia timu ya wanamichezo hao na si kuacha kuwekeza katika soka peke yake.

Alisema kuwa anaamini wanamichezo hao watafanya vizuri kwenye michezo hiyo wanayokwenda na kuliletea sifa taifa.

"Kuna usemi usemao kuwa Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe, tumeamua kusaidia wanamichezo hawa ili kuendeleza michezo nchini na siyo soka, tunajua kuna riadha, netiboli na michezo mingine," alisema Mohammed.

Licha ya kutoa msaada huyo, kiongozi huyo alimweleza Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, kwamba wameiandaa vyema timu yao ya Azam kwa ajili ya kufanya vizuri katika mechi za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara na mashindano ya Klabu Bingwa Afrika watakayoshiriki mapema mwakani.

Akipokea hundi hiyo, Naibu Waziri, Nkamia, alisema kwa niaba ya serikali wanaishukuru kampuni hiyo kwa kiasi hicho cha fedha na kueleza kwamba kitasaidia kukamilisha mahitaji ya wanamichezo hao walioondoka nchini jana.

Nkamia alisema kuwa fedha hizo zitasaidia kununulia baadhi ya vifaa vya wanamichezo na kuwalipa posho na mishahara makocha wa kigeni waliokuwa wakiwanoa nyota hao.

Alisema kwamba wanamichezo hao wanafahamu wanadeni na watahakikisha wanafanya vizuri na kuliletea heshima taifa.

Mara ya mwisho kwa wanariadha wa Tanzania kupata medali katika michezo hiyo ilikuwa ni mwaka 2006. Mara hii, kabla ya kuondoka nchini waliwezeshwa kukaa katika kambi tofauti ikiwamo nchini Ethiopia, New Zealand, China na Uturuki.

Juzi wanamichezo hao walikabidhiwa bendera ya Rais Kikwete katika hafla fupi iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini.
CHANZO: NIPASHE

No comments: