ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 14, 2014

Ballali hakuwa mgonjwa wakati akienda Marekani

“Ndugu za aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Daudi Ballali ambao ni Paschal Ballali (mwenye kofia), Onesmo Ballali na Maura Ballali wakizungumza na Mwandishi wa Mwananchi, Neville Meena (wa pili kushoto) katika Kijiji cha Luganga, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa. Na Mpigapicha Wetu
Na Neville Meena, Mwananchi
Dar/ Marekani. Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania, Marehemu Daudi Ballali hakuwa mgonjwa wakati akiondoka na aliugua kwa takriban miezi kumi kabla ya kukutwa na mauti, Mei 16, 2008 nyumbani kwake, Washington DC nchini Marekani.
Ballali aliondoka nchini wakati kashfa za wizi kwenye akaunti ya EPA zikiwa zimeshamiri na wakati kesi za watuhumiwa zikianza kusikilizwa huku jina la gavana huyo wa zamani likitajwa, ilitaarifiwa kuwa alifariki baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Miezi mitatu baada ya Ballali kuanza kuugua, Rais Jakaya Kikwete alikiri kuwa na taarifa za ugonjwa wake, lakini kakanusha kuwa amekimbia tuhuma za ufisadi zilizokuwa zinaelekezwa Benki Kuu (BoT).
Hata hivyo suala la gavana huyo likaendelea kuwa kitendawili hadi mauti yake, ambayo pia iliamsha mjadala mpya; baadhi wakidai hakuwa amefariki na wengine wakihoji mazingira ya kifo chake.
Lakini uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na kuthibitishwa na baadhi ya ndugu wa marehemu, umebaini kuwa gavana huyo alifariki na kuzikwa nchini Marekani, lakini wakati anaondoka nchini Agosti 2008, Ballali hakuwa mgonjwa kama inavyodaiwa na wengi.
Taarifa kutoka ndani ya BoT alikokuwa akifanya kazi akiwa gavana pia zinasema kiongozi huyo alikwenda Marekani kwa mambo makubwa mawili; Kwanza kufanya baadhi ya kazi zinazohusiana na taasisi hiyo kuu ya fedha nchini na pili kusalimia familia yake ambayo wakati wote imekuwa ikiishi Marekani.
Hata hivyo, Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndulu jana alikataa katakata kuzungumza iwapo taasisi yake ina taarifa iwapo Ballali aliondoka nchini akiwa mgonjwa au la, na badala yake akataka suala hilo waulizwe wanafamilia.
“Hayo mambo yalishaandikwa sana na nyie mmeandika sana. Kila mtu anafahamu kwamba aliondoka akiwa mgonjwa, sasa hizo taarifa nyingine unazoniambia mimi siwezi kuzizungumzia. Kaulize familia yake,” alisema Profesa Ndulu.
Wakati Ballali akiwa gavana, Profesa Ndulu alikuwa mmoja wa manaibu wake na baadaye aliteuliwa kushika wadhifa huo baada ya ‘bosi’ wake kuondolewa kwenye nafasi hiyo baada ya kampuni ya Earnst and Young kubaini ufisadi mkubwa kwenye benki hiyo.
Hata hivyo, dada yake na Ballali, Margaret Mpango alisema kaka yake hakuwa mgonjwa na alitarajia kukaa siku chache nchini Marekani.
“Safari yake ilikuwa ya siku chache tu. Alikwenda Marekani lakini alikuwa amepanga kurejea nchini baada ya muda mfupi maana nyumbani kwake simu zake mbili zilikuwa mezani pamoja na funguo za gari ambalo lilikuwa limeegeshwa nje kwa style (mtindo) ambayo ilionyesha kwamba angerudi mapema,” alisema.
Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake mjini Kigoma, Margaret ambaye ni mke wa askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana, Dk Gerard Mpango, alisema baadhi ya nguo za marehemu zilitumwa Marekani baada ya kuanza kuumwa.
“Kama mtu alikuwa anakwenda kukaa sana kwa maana ya ugonjwa, basi angechukua nguo za kutosha, lakini wakati wifi (mke wa Ballali, Anna Muganda), aliponiomba kwenda kuchukua baadhi ya nguo, vitu vya kaka vilikuwa vimeachwa katika hali ambayo ilionyesha kwamba hakai sana,” alisema Margaret na kuongeza:
“Nakumbuka kwamba hata mikoba yake miwili iliyokuwa na vitu vyake vya kazini ilikuwa imewekwa mahali ambako hapakuwa siri. Na hii ni dalili kwamba alipanga kwamba angekwenda na kurudi baada ya muda mfupi.”
Kuugua kwake
Taarifa zinaonyesha kwamba Agosti 17, 2007 zikiwa ni siku chache tangu alipofika Washington, Ballali alijumuika na familia yake, ndugu wa karibu na marafiki zake akiwamo mtangazaji wa zamani wa Sauti ya Amerika (VOA), Athanas Maijo.
Maijo alialikwa katika hafla hiyo ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Ballali alipotimiza umri wa miaka 65, kutokana na ukweli kwamba, wawili hao waliwahi kuwa marafiki wa karibu na waliwahi kufanya kazi pamoja VOA katika miaka ya 60, wakati Ballali alipokuwa akisoma Chuo Kikuu cha Howard, Washington.
Habari zaidi zilizopatikana mjini Washington zinasema baada ya kumaliza shughuli zilizompeleka Washington, mwishoni mwa Agosti Ballali aliamua kwenda kufanyiwa uchunguzi wa afya na daktari wake aliyeko katika Hospitali ya Massachusetts iliyoko Boston, na baadaye angerejea nyumbani.
Hata hivyo, baada ya kufika hospitalini hapo, daktari wake alishtuka kutokana na matokeo ya vipimo vya tumbo alivyomfanyia, hivyo kuamua alazwe ili apate matibabu zaidi.
“Alikwenda kule na mke wake (Mama Muganda) na hawakuwa hata wamebeba nguo za kutosha kwani hawakujua kama angekutwa na matatizo yaliyosababisha alazwe, kwa hiyo ilibidi nguo pamoja na vitu vingine vipelekwe baada ya kulazwa kwake,” kilieleza chanzo chetu jijini Washington.
Habari kutoka kwa ndugu wa karibu wa gavana huyo zinasema daktari huyo katika vipimo vyake, alibaini kuwapo kwa tatizo kubwa katika utumbo mpana, hivyo aliamua kumfanyia upasuaji mkubwa baada ya kushaurina na madaktari wenzake katika hospitali hiyo, wakishirikiana na daktari wa Ballali aliyekuwa Washington akifanya kazi katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Georgetown.
Upasuaji huo ulikumbwa na changamoto kubwa kwani tatizo aliloliona daktari kupitia vipimo vya kitaalamu, lilikuwa ni tofauti kabisa na tatizo halisi ambalo daktari huyo alikutana nalo wakati akitaka kutekeleza wajibu wake.
“Ilibidi sasa awasiliane na daktari mwenzake yule wa Washington kumwambia tofauti hizo, kwa hiyo alimshauri kwamba atibu matatizo yote mawili, lile alilokuwa akiliona kwenye vipimo na lile alilokutana nalo wakati akitaka kuanza upasuaji,” alidokeza ndugu mwingine wa Ballali ambaye hata hivyo alikataa katakata kutaja aina ya matatizo hayo.
Alisema tiba hiyo ambayo alimsababisha Ballali kulazwa kwa siku kadhaa na kuyeyusha mipango yake ya kurejea Tanzania mapema, ndiyo iliyomwezesha kuishi kwa muda mrefu zaidi, vinginevyo asingevuka 2007.
Wakati wote alipokuwa amelazwa, hakuna kiongozi yeyote wa Serikali kutoka Tanzania wala ubalozini Washington DC aliyefika kumjulia hali.
Juzi Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue, ambaye wakati wa kifo cha Ballali alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani, alikiri kwamba alihudhuria ibada na baadaye mazishi wakati huo.
Hata hivyo, alipoulizwa iwapo aliwahi kumjulia hali Ballali alipokuwa amelazwa, Sefue alisema hakuwahi kufanya hivyo na alipoulizwa sababu za kutokwenda alisema kwa kifupi: “Ndiyo hivyo, haikutokea, lakini ukweli ni kwamba Ballali aliumwa na bahati mbaya alifariki dunia.”
Kutoka hospitali
Desemba 2007, Ballali aliruhusiwa kutoka hospitali na alikaa kwa muda katika hoteli moja mjini Boston na baada ya kupata nafuu alirudi nyumbani kwake Washington ambako aliendelea kuuguzwa, huku afya yake ikielezwa kwamba ilikuwa ikiendelea kuimarika.
Hata hivyo, mwanzoni mwa Aprili 2008, Ballali alilazwa tena, safari hii katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Georgetown ambako alikaa hadi mwanzoni mwa Mei mwaka huo, alipoambiwa na madaktari kwamba asingeweza kupona na kwamba mauti yangemkuta katika wiki mbili.
Habari kutoka ndani ya familia yake zinasema madaktari waliokuwa wakimtibu walimwambia kwamba asingeweza kuishi kwa zaidi ya wiki mbili, hivyo walimshauri ahamie kwenye nyumba maalum ya kusubiri kifo kwa watu ambao magonjwa yao yameshindikana.
Hata hivyo, Ballali alikataa na badala yake kutaka arejeshwe nyumbani kwake, Washington ambako aliendelea kuugua na hatimaye kukutwa na mauti Mei 16, 2008 kisha kuzikwa katika makaburi ya Gate of Heaven yaliyopo Silver Spring, Maryland.
Gazeti hili liliwasiliana na hospitali zote mbili ambako Ballali aliwahi kulazwa, lakini lilijibiwa kwamba taarifa za mgonjwa huyo zinaweza kutolewa tu ikiwa familia yake ndiyo inayozihitaji.
Mkanganyiko wa taarifa
Kilichobainika kinapingana na taarifa kadhaa zilizowahi kupatikana kutoka katika vyanzo mbalimbali serikalini, zikidai kwamba Ballali alikuwa mgonjwa wa kansa ya damu (leukemia) na kwamba kwa muda mrefu alikuwa akitibiwa Afrika Kusini kabla ya kutibiwa Marekani.
Hata hivyo, baada ya kifo chake suala la kansa ya damu lilipotea kabisa na hakuna anayelizungumzia hivi sasa, kwani kila ndugu anayeulizwa anasema hafahamu sababu za kifo chake.
Akizungumza na mwandishi wa Mwananchi katika mahojiano yaliyofanyika Machi 1, mwaka jana, katika Kijiji cha Luganga, Wilaya ya Mufindi, Iringa, Paschal Ballali ambaye ni mdogo wake na marehemu alisema hana kumbukumbu kwamba kaka yake aliwahi kuugua ugonjwa wa kansa.
“Nakumbuka siku chache kabla ya kwenda Marekani nilikutana na kaka akitoka kazini pale BoT na aliniambia kwamba atasafiri kwa siku cheche na atarudi. Lakini hakuniambia kwamba anaumwa, na hata katika kuishi kwake sikumbuki kama aliwahi kusema kwamba anaumwa kansa,” alisema Paschal.
Kuhusu kutibiwa Afrika Kusini, Paschal alisema siku chache baada ya kuanza kazi BoT, Ballali aliwahi kuanguka ghafla akiwa ofisini kutokana na kufanya kazi muda mrefu, na kwamba wakati huo ndipo alipokwenda kutibiwa nchini humo.
“Tena nakumbuka kipindi hicho ni kama 2002 aliporudi baada ya kupona, alituita nyumbani kwake, Dar es Salaam tukashiriki kutoa shukrani kanisani kisha alifanya sherehe ndogo ya tukio hilo, tangu hapo sijawahi kusikia kwamba anakwenda Afrika Kusini kutibiwa,” alisema Paschal.
(Sahihisho: Katika matoleo mawili yaliopita, tuliandika kwamba nyumbani kwa Ballali ni Maryland, usahihi ni kwamba nyumbani kwake alikofia ni Washington DC baada ya kuwa amehama. Pia hospitali alikolazwa mara ya pili ni Georgetown na siyo George Washington. Tunaomba radhi kwa usumbufu - Mhariri).

1 comment:

Anonymous said...

WATANZANIA UJUE UKWELI JUU YA DAUDI BALALI, UFISADI, UGONJWA, KIFO NA COVER UP
Daudi Balali hakuwa raia wa Tanzania tena baada ya kuukana uraia wa Tanzania na kuwa raia wa Marekani miaka kadhaa aliyoishi Marekani akifanya kazi World Bank. Alikuwa ameoa mmarekani na watoto wakubwa tu. Aliolea jimbo la Connecticut. Alipewa kazi na swahiba wake Ben Mkapa ambaye aliivunja katiba aliyoapa kuilinda, kuitetea, na kuihifahi kwa kumpa ajira raia wa nje Bw. Daudi Balali pindi akijua fika alifanyalo. Ben Mkapa aliwahi kuwa balozi wa Tanzania nchini Marekani miaka ya 1980s ambapo aliweza kukutana na Balali na kuwa marafiki wa karibu zaidi. Daudi Balali alipewa kitengo muhimu cha usimamizi wa fedha nchini kama Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, nafasi inayohitaji kushikiliwa na raia halisi. Plan hii si makosa bali ni mkakati mahususi kuihujumu nchi uliopelekea nchi kuporwa mabilioni ya pesa na mafisadi mbali mbali nchini kwa kipindi kirefu cha ongoing wa raia huyu wa kigeni. (Kashfa ya EPA) . Balali alikuwa akiumwa na hivyo alipopata mwanya wa kutoroka kabla ya kufikishwa mahakamani alifanya hivyo. Ikumbukwe nchi ya Marekani haiwezi kumpeleka raia wake nje ya nchi ashitakiwe ili miradi hajavunja sheria za Marekani. Balali alikuwa akibeba pass mbili za kusafiria, moja ya kimarekani na nyingine ya kidiplomasia (diplomatic passport) ya Tanzania kinyume na Sheria ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Hapo 2008 Wakati wa sakata hilo, balozi Ombeni Sefue akiwa Washington DC kama balozi wa Tanzania Marekani alitoa kauli zenye utata juu ya mtuhumiwa Daudi Balali kutorudiswa nyumbani kujibu tuhuma nzito za wizi wa mabilioni Benk kuu BOT aliouidhinisha, alijibu kwa kusema Serikali ya Tanzania ilikuwa imebatilisha diplomatic passport yake na hivyo hakuwa halali nchi Marekani. Pia siku chache alitoa kauli yanye utata kuwa Bw. Balali alikuwa mgonjwa amelazwa hospitalini Boston, jimboni Massachusetts na familia yake wanaomba privacy. Baada ya siku chache ikatangazwa bwana huyu amefariki dunia na mazishi yake yatakuwa ni ya familia tu, swala lililoushangaza umma wa watanzania wote duniani. Taarifa iliyotolewa baadaye ni kuwa mwili wa marehemu Balali ulizikwa makaburi ya Gate of Heaven, mjini Silver Spring jimboni Maryland chini ya maili moja na maskani yangu. Mpaka leo hakuna Mtanzania yeyote anayejua ukweli wa hili kwani "cover up" kuficha ukweli kwa makusudi kumeendelea. Mabilioni ya fedha ya umma yametoweka na Siri nzima alitokomea nayo mmarekani huyu Daudi Balali. Balozi Sefue anajua ukweli lakini ameendelea kuudanganya umma kwa niaba ya serikali. Rais Mstaafu Mkapa na wengine wengi wana case kubwa za kujibu. Siku za usoni haki itatendeka. Watanzania popote walipo watakapopata nafasi ya kujua ukweli na sheria kuchukua mkondo wake.