ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 31, 2014

BONDIA MTANZANIA MADOLA AKIMBILIA CHOONI WAKATI ALITAKIWA APANDE ULINGONI

Nasser Mafuru

Tumbo la 'kuendesha' lililomshika bondia Nasser Mafuru wakati wa Michezo ya Jumuiya ya Madola na kuchelewa kupanda ulingoni kucheza pambano dhidi ya bondia kutoka Ghana, Jessie Lartey linaweza kusababisha matatizo makubwa kwa shirikisho la ngumi nchini (BFT), baada ya lile la kimataifa (AIBA) kutaka maelezo ya kina.

Nasser alichelewa kupanda ulingoni katika pambano la uzito wa light dhidi ya bondia Lartey, na hivyo majaji kumpa Mghana huyo ushindi wa pointi 3-0.

Muda wa kupanda ulingoni ulipowadia bondia Mafuru alielekea chooni, ambako alikaa kwa muda na kuchelewa kupanda ulingoni.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari baada ya tukio hilo, maafisa usalama walianza harakati za kumuhoji Mafuru kujua chanzo cha tatizo lake muda mfupi kabla ya pambano kuanza.

Chanzo kilizidi kueleza kuwa, baada ya bondia huyo kuhojiwa alitoa maelezo ya kuwa alishikwa na tumbo hilo, baada ya kuingiwa na woga, kutokana na mabondia wenzake waliotangulia akiwamo nahodha Seleman Kidunda kupigwa katika hatua za awali za mashindano hayo.

Hata hivyo, chanzo kilieleza kuwa Mafuru huenda alimuhofia bondia huyo kutoka Ghana kutokana na kuwa na rekodi nzuri katika mchezo wa ngumi, tofauti na rekodi yake yeye.

Huku kukiwa na tuhuma za baadhi ya vyama vya michezo kuwabeba wanamichezo ambazo hawajafuzu viwango vya kuchuana katika michezo hiyo, AIBA sasa inataka maelezo kutoka kwa BFT.


Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya shirikisho hilo kutokana na kosa la Mafuru, BFT inaweza kupewa adhabu kali kama wasipotoa maelezo ya kujitosheleza, ikiwamo mchezaji mwenyewe kufungiwa kushiriki katika mashindano hayo.

"Bondia na shirikisho wanaweza kupata adhabu kali kutokana na uzembe wa mchezaji," kilieleza chanzo. NIPASHE ilipomtafuta Katibu wa BFT, Makore Mashaga alisema kuwa taarifa za Mafuru kuhojiwa mara kwa mara na maafisa wa usalama mjini Glasgow kutokana na kuchelewa kupanda ulingoni ni za kweli, lakini hawawezi kuzizungumzia hadi timu hiyo itakaporejea nchini ikitokea katika mashindano hayo ya 20 ya Michezo ya Jumuiya ya Madola.

"Ni kweli nimepata taarifa ya kuwa Nasser amehojiwa, tunasubiri viongozi walioandas timu watuletee taarifa ndiyo tujue tunafanya nini," alisema Mashaga.

Michezo ya Jumuiya ya Madola, inayotarajia kufikia ukingoni Agosti 3 mjini Glasgow, Scotland huku Tanzania ikitolewa katika michezo yote ambako haijaambulia medali yoyote.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Hii aibu tu.