ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 12, 2014

CCM KUMEKUCHA: Karume ajitosa kuwania Urais

  Apiga debe Rais wa 2015 atoke Zanzibar
  Bosi wa January Makamba naye atajwa
Balozi Ali Abeid Amani Karume

Nguvu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuzuia wimbi la wanachama wake kutangaza nia ya ‘kumrithi’ Rais Jakaya Kikwete, wakati akiwa bado madarakani, zinaonekana kufifia.

Baada ya Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kufikia hatua hiyo, Balozi Ali Abeid Amani Karume (pichani) ambaye ni mtoto wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, ametangaza nia ya kuwania Urais kupitia CCM.

Kwa muda mrefu sasa, CCM imekuwa na utaratibu wa kumuachia fursa ya utawala Rais aliyemaliza muda wake.

Kutokana na hali hiyo, kitendo cha kutangaza nia kabla ya muda unaotambulika kisheria kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu, kimekuwa kikichukuliwa kuwa chenye kukiathiri chama hicho.

Lakini baada ya Makamba na Sumaye, Balozi Karume, amezungumza na NIPASHE Jumamosi mjini hapa, na kusema ameshajiandaa kuiomba CCM impitishe kuwania kiti hicho kwa sababu ana uwezo na sifa zinazostahili.

“Kweli nategemea kuwania Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,” alisema Balozi Karume.

Ikiwa atafanikiwa kuliingiza jina lake katika kinyang’anyiro hicho, itakuwa ni mara ya pili kwa Balozi Karume, kufikia uamuzi huo.

Kwa mara ya pili kwa Balozi Karume ambaye ni kaka wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, aliomba ridhaa ya kuteuliwa na CCM kuwania nafasi mwaka 2005, lakini hakufanikiwa.

Pia wakati kaka yake, Amani Abeid Karume, akistaafu mwaka 2010, Balozi Karume alijitokeza kutaka kuwania Urais wa Zanzibar mwaka 2010, lakini nafasi hiyo ikachukuliwa na Rais wa sasa, Dk Ali Mohamed Shein.

Akijielekeza katika kuitambua fursa hiyo, Balozi Karume, alisema kuna uwezekano kwa mgombea Urais kupitia CCM kwa Uchaguzi Mkuu ujao, akatokea Zanzibar.

Alisema, kutokana na ‘utabiri’ wake huo, miongoni mwa wana-CCM watano (akiwamo yeye) waliotangaza nia ya kuwania Urais wa Zanzibar 2010, atapewa nafasi hiyo.

BOSI WA JANUARY MAKAMBA NAYE YUMO
Hata hivyo, Balozi Karume hakuwataja watu wengine wanaowania nafasi hiyo, lakini NIPASHE Jumamosi limebaini majina yanayotajwa visiwani hapa kuwa ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa.

Tayari January Makamba ambaye ni Naibu wa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia (inayoongozwa na Mbarawa), ameshatangaza nia, akieleza kujipima na kubaini kuwa na asilimia 90 za kufikia uamuzi huo.

Wengine wanaotajwa katika kinyang’anyiro hicho kutoka Zanzibar ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Ali Mwinyi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha.

Balozi Karume alisema kuwa hakuna kitu kigumu duniani kama kujipima mwenyewe, lakini watu aliozungumza nao (hakuwataja) wamemwambia anafaa kugombea na jambo hilo limempa faraja ya kutangaza nia.

Alisema hana nia ya kugombea Urais wa Zanzibar, kwani angependa nafasi hiyo aendelee nayo rais wa sasa, Dk Ali Mohamed Shein.

HEKAYA ZA UJANA NA UZEE
Balozi Karume, alisema katika suala la Urais hakuna hoja ya ujana wala uzee inayoweza kupata nguvu, bali ni kutimiza vigezo vya kisheria na utaratibu wa CCM unaoainisha sifa 13 na kuwa na afya bora.

Alisema ana imani sifa hizo anazo, hivyo hana pingamizi lolote kuhusu `safari ya kueleka Ikulu’ ya jijini Dar es Salaam.

Balozi Karume ni mtoto wa pili wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, ambaye kwa muda mrefu alikuwa akifanya kazi ya ubalozi katika nchi za Ulaya na badaye mwaka 2005 alijitokeza kutaka kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano.

Pamoja na kujitokeza kwa viongozi kadhaa tamko la hivi karibuni la Makamba (January) kwamba anafaa kugombea nafasi ya Urais, imeibua mjadala na kufungua mlango unaowafanya wanaohusishwa rasmi na kuwania nafasi hiyo kufikia watatu.
Pamoja na hao, Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, aliwahi kutangaza kuanza safari ya matumaini kwa Watanzania, alipowaalika watu waliokadiriwa kuwa zaidi ya 3,000 nyumbani kwake, Monduli Januari Mosi mwaka huu.

Safari hiyo aliyoiita kuwa ya matumaini na kuwataka wanaomuunga wajitokeze hadharani, ilitafisiriwa kuwa yenye kutangaza kuwania Urais baada ya kipindi cha Rais Kikwete kufikia ukomo wake 2015.

Mbali na Zanzibar, majina ya wanasiada kadhaa yanatajwa upande wa Tanzania Bara, yakihusishwa na mbio za Urais wa 2015.

Miongoni mwa wanaotajwa ni Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, Waziri wa Afrika Mashariki, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Akizungumzia hali hiyo ya kujitangaza kwa wanachama wa CCM, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema kwenye mapana na marefu ya demokrasia suala hilo haliwezi kudhibitiwa.

Dk. Bana alisema sio vizuri kuwekewa pingamizi katika suala hilo kwani kila mtu ana haki ya kusema anachokitaka bila kuvunja sheria.

“Mwanachama kama ana nia ya kugombea sio jambo baya watu kutangaza nia zao na sio kukaa kimya kama mtu unaguswa na una sifa unaweza kujitangaza bila kuvunja sheria,” alisema Dk. Bana
Hata hivyo, alisema jambo baya ni watu hao kuvunja kanuni za kupiga kampeni huku wakitumia fedha nyingi kufanya suala hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: