Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akifungua mkutano wa siku moja wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo siku nzima ya Alhamisi liLIjadili ajenda ya uwekezaji kwa Afrika na mchango wake kwa Maendeleo endelevu. Katika hotuba yake, Ban Ki Moon alisema Afrika isiridhike na ukuaji wa jumla wa uchumi wake ambao umekuwa ni mzuri bali inahitaji kuwekeza zaidi ili uwekezaji huo uweze kuchangia katika kuleta maendeleo endelevu, kuwaondolea watu wake umaskini, kukuza ajira na kipato na kwamba Afrika ilihitaji kuwekeza zaidi katika miundombinu, kilimo na nishati endelevu pamoja na mambo mengine.
Muwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Tuvako Manongi akizungumza wakati wa mkutano kuhusu uwekezaji katika Afrika. Katika mchango wake, alisisitiza kuwa pamoja na Afrika kuchagizwa kuvutia uwekezaji zaidi pamoja na ukusanyaji wa mapato ya ndani Jumuiya ya kimataifa inatakiwa kutoa ushirikiano usio na shaka katika udhibiti wa ukwepaji mkubwa wa kodi, utoroshwaji na biashara harafu ya fedha na ambayo inazinyima nchi za Afrika mapato ambayo yangeweza kutumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na hivyo kuwaondoelea wananchi wake umaskini uliokithiri.
Na Mwandishi Maalum,
Wakati ni jambo lisilopingika na linalokubalika na waafrika wenyewe na washirika wa maendeleo kwamba uchumi Afrika unakua vizuri. Hata hivyo ukuaji huo unaelezwa bado haujaweza kupunguza au kuondoka changamoto mbalimbali za kimaendeleo zinazolikabili bara hili na watu wake.
Na kwa sababu hiyo imeelezwa kwamba ili afrika iwe na maendeleo endelevu na jumuishi basi inahitaji kuongeza kasi ya kuvutia uwekezaji na mitaji kutoka ndani ya Afrika yenyewe na nje.
Hata hivyo suala kubwa na ambalo limekuwa likiwafikirisha waafrika wenyewe na wataalamu wa masuala ya uchumi na maendeleo ni hili , je ni aina gani ya uwekezaji na wenye tija ambao Afrika inauhitaji.
Katika siku nzima ya Alhamisi Baraza kuu la Umoja wa Mataifa lilikuwa na majadiliano ya kina yaliyojikita katika eneo la Uwekezaji na umuhimu wake kwa maendeleo ya bara la Afrika na watu wake ni vile vile mchango wake katika mchakato mzima wa maendeleo endelevu baada ya 2015.
Mkutano huo ulifunguliwa na katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ambaye katika hotuba yake, pamoja na kusifia namna Afrika ilivyopiga hatua nzuri katika ukuaji wa Uchumi, akaeleza kuwa kama kweli Afrika ilikuwa inataka maendeleo yamfikie kile mtu basi ilikuwa inahitaji kufanya mambo matatu.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, mambo hayo ni kujiwekea mazingira mazuri yatakayovutiwa wawekezaji , aina sahihi ya miradi/ uwekezaji inayotakiwa kuwekezwa na udhibiti mzuri wa mapato yatokanayo na uwekezaji huo ili hatimaye yaweze kuhimili maendeleo endelevu.
Katika Mkutano huo na ambao washiriki mbalimbali walipata fursa ya kuchangia mawazo yao, Ban Ki Moon pamoja na kuelezea maeneo hayo matatu, alianisha pia mafanikio kadhaa na changamoto kadhaa ambazo anasema Afrika inaendelea kukabilina nao, akazitaja baadhi ya change moto hizo kuwa ni uwekezaji duni katika miundombinu, kilimo, ajira kwa vijana, utaalam na teknolojia anuai na tatizo kubwa la nishati ya uhakika na ambayo haiwafikii watu wengi.
Katibu Mkuu alisifu mikakati na mipango mbalimbali ya kimaendeleo, kiuchumi na kijamii, ambayo ama Viongozi wa Afrika tayari wameshaanza kutekeleza au ilikuwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Alipopata nafasi ya kuchangia maoni ya Tanzania kuhusu umuhimu wa uwekezaji na maendeleo kwa Afrika, Muwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi yeye alieleza kuwa pamoja na kwamba Tanzania ilikuwa inakubaliana na umuhimu wa uwekezaji kwa maendeleo, uwekezaji huo unahitaji ushirikiano wa pamoja, uwazi na utawala bora.
Akaeleza kwamba kama ilivyoelezwa na wazungumzaji wengine, sura ya Bara la Afrika imebadilika sana, Afrika ya sasa si ile iliyokuwa ikidharauliwa na kuonekana kama ni bara lisilo na muelekeo wowote.
Akasema anakubaliana pia kwamba uchumi wa afrika unakua vizuri na kuwa ukuaji huo umechangiwa na mambo mengi baadhi yake ni pamoja na sera na mipango mizuri ya kiuchumi, uwepo wa mazingira ya amani na usalama katika maeneo mengi ya Afrika na ukuaji ya kada ya watu wenye kipato cha kati pamoja na wimbi kubwa la vijana ambao nao ni mtaji wa aina yake.
Balozi Manongi pia akagusia umuhimu wa uwekezaji katika miundombinu, afya, elimu na kilimo kuwa ni baadhi ya maeneo ambayo kama yakiwafanyiwa kazi vizuri yatasaidia katika kuifanya Afrika isonge mbele.
Hata hivyo Muwakilishi huyo wa Tanzania akasema kasi ya ukuaji wa uchumi wa Afrika, pamoja na ule wa nchi moja moja na jitihada kubwa na nzuri zinazofanywa na viongozi wakuu wa nchi na serikali pamoja wakishirikiana na wananchi wenyewe, zinaweza kukwamishwa au zinakwamishwa na baadhi ya na changamoto kadhaa zinazohitaji ufumbuzi wa pamoja.
Moja ya changamoto hizo na ambazo amesema ni tatizo kubwa la linalochangia kurudisha nyuma juhudi za nchi nyingi za Afrika kujiletea maendeleo yao ni tatizo la utoroshwaji wa fedha au biashara ya fedha haramu zinazofichwa nje ya Afrika na kusababisha ukwepaji mkubwa wa kodi.
Akasema utoroshwanji huo wa fedha na ambazo hazilipiwi kodi zinazinyima nchi zinazoendelea mapato ambayo yangetumia kujenga hospitali, shule, barabara na miradi mingineo ya maendeleo pamoja na utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya millenia.
Changamoto nyingine alizosema zinarudisha nyuma maendeleo ya Afrika ni pamoja na uvunuaji holela wa maliasili, biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na za kati na rushwa.
Balozi Manongi akasema ni kwa sababu hiyo na nyingine nyingi ndiyo maana Tanzania imekuwa ikiunga mkono malengo ya maendeleo endelevu ambayo kwayo yatachangia siyo tu kuwahakikisha maendeleo jumuishi kila mtu lakini pia yatakayoweza kukabiliana na changamoto alizozitaja.
Baadhi ya wawakilishi kutoka mataifa yaliyoendelea waliozungumza katika mkutano huo walijipambanua zaidi kwa kuelezea ni kwa namna gani nchi zao zimekuwa zikichangia katika maendeleo ya Afrika kwa kutoa misaada mbalimbali ya kimaendeleo yakiwamo pia masuala ya teknolojia.
Muwakilishi wa Marekani katika mkutano huyo naye pamoja na kuelezea ushirikiano uliopo kati ya Marekani na Bara la Afrika kwa maana ya maendeleo ya kiuchumi, alitangaza katika mkutano huo kwamba, Serikali ya Rais Obama ilikuwa inaadaa mkutano kati ya Marekani na Afrika. Mkutano huo utaojadili ushirikiano wa kibiashara na unarajiwa kufanyika mwanzoni mwa wezi Agosti mwaka huu.
No comments:
Post a Comment